Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mpina Amsimamisha kazi Mtumishi Kagera

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiangalia maboksi ya samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 yaliyokamatwa katika kituo kikuu cha mabasi cha mjini Kagera hapo jana.

Na.Mwandishi Wetu, Kagera.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana  Budeba kumsimamisha  kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki.

Kwa mujibu wa Waziri Mpina, samaki waliotoroshwa ni kilo 2,530 wenye thamani  ya  Tsh. 20,850,000/=  ambao walitoroshwa kwenda nchini Burundi.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akitoa tamko la kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma kwa tuhuma za kushiriki katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.

Akizungumza katika ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina  alisema  mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00  asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.

“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na  barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja.” Alisisitiza Mpina

Aidha, Waziri alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo,  na kuongeza kwamba samaki hao walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.

 

Moja ya boti inayotumika kwenye doria katika ziwa Viktoria na Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera.

Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa  walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50.

Taratibu nyingine zilizokiukwa ni, msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.

Waziri Mpina  alisema samaki hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.

Alisema  kazi hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele.

Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na  kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama,pamoja na kukamatwa  kwa uduvi kilo 5000.

Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia  katika  uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Waziri Mpina  alitoa wito kwa Halmashauri zote nchini kushiriki kikamilifu katika kulinda raslimali za majini  na baharini kwa kuwa  licha ya  raslimali hizo kutoa mchango  mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake ni makubwa kwao.

46 thoughts on “Mpina Amsimamisha kazi Mtumishi Kagera

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *