Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface watatu kutoka kushoto akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya timu ya Madaktari Bingwa kutoka China, kulia kwake ni Dkt. Meng Yong (Kiongozi wa timu ya madaktari bingwa hao, kushoto kwake ni Dkt. Zhang Bo na wa kwanza kulia ni Dkt Lou Yanhua. Wengine ni Muwakilishi wa Wizara ya Afya, Dkt Vumilia Liggyle wa kwanza kulia na Mkurugenzi wa tiba MOI, Dkt. Samuel Swai wapili kushoto.
Na Mwandishi wetu MOI
Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepokea timu ya madaktari bingwa kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambao watatoa huduma za kibingwa katika Taasisi za MOI, MNH, JKCI na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) kwa kipindi cha miaka miwili.
Mnamo mwezi Septemba mwaka 2021, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya iliingia mkataba namba 26 wa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China, mkataba huo pamoja na mambo mengine ulijikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuleta madaktari bingwa kutoka China kutoa huduma katika hospitali za kibingwa hapa nchini.
Akizungumza katika hafla ya kupokea madaktari bingwa hao katika Taasisi ya MOI, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface amesema ujio wa madaktari bingwa hao ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za kibingwa ambapo pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa madaktari hao watafundisha wanafunzi.