Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mkutano wa Nishati kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Waanza Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Utawala, Christopher Bazivamo, akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, Juni 3, 2019 jijini Arusha.

Na Veronica Simba – Arusha

Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeanza leo Juni 3, 2019 jijini Arusha.

Akifungua Mkutano huo katika siku ya kwanza ambao unahusisha ngazi ya wataalamu wa sekta husika; Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Utawala, Christopher Bazivamo, amewataka kujadili kwa uwazi changamoto zinazokabili nchi wanachama hususan upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kuainisha mikakati ya kuzitatua.

“Jamii zetu bado hazijawa na umeme wa uhakika ukilinganisha na sehemu nyingine za Dunia. Hii ni changamoto ambayo tunahitaji kuitafutia ufumbuzi. Tujadili kwa uwazi ili tuone wapi tunakwama na namna gani tutatue,” amesisitiza.

Akifafanua zaidi, Bazivamo amesema changamoto za nishati kwa nchi za Afrika Mashariki zinahusisha mambo mbalimbali ikiwemo nishati ya kupikia ambayo ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wanajamii wa ukanda husika wangali wanatumia kuni na mkaa; hali inayochangia uharibifu wa mazingira.

Amesema haitoshi kuwaonesha wananchi kuwa nishati ipo isipokuwa kuchukua hatua za kuifanya ipatikane kwao na kwa bei wanayoweza kuimudu.

Wajumbe wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ngazi ya wataalamu, wakishiriki ufunguzi wa Mkutano huo Juni 3, 2019 jijini Arusha.

Aidha, Bazivamo amewashauri wataalamu husika, kuhakikisha wakati wanahamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa umeme, wahamasishe pia uwekezaji katika usambazaji wa nishati hiyo ili kuwezesha hali ya upatikanaji wake kwa jamii.

Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo wa 14 unatarajia kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi na programu katika sekta ya nishati pamoja na maagizo yaliyotolewa katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati.

Aidha, Mkutano utapokea Rasimu ya Makubaliano ya Awali (MoU) iliyoandaliwa na Sektetarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Mradi wa Umeme wa Nsongezi katika Mto Kagera unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirika wa nchi za Tanzania, Uganda na Rwanda ili ipitiwe na nchi husika.

Mkutano ngazi ya Mawaziri utafanyika Juni 7 mwaka huu, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya mkutano husika.

Tanzania inawakilishwa na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusiana na nishati kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

120 thoughts on “Mkutano wa Nishati kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Waanza Arusha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama