Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Milambo Waomba Radhi Kwa Utovu wa Nidhamu Uliofanywa na Wenzao.

Na: Tiganya Vincent, RS – TABORA

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Milambo wameiomba radhi Serikali kwa vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyosababisha baadhi wamefikishwe Mahakamani na wengine kulazimishwa kuhamishwa shule hiyo kwa makosa ya kutoroka shuleni nyakati za usiku.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) ambaye pia ni Makamu Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo Baraka Fundo kwa niaba ya wanafunzi wenzake waliobaki shuleni hapo wakati Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alipopita kukagua miradi mbalimbali ya shule.

Alisema kuwa matukio mawili yaliyofanywa na wenzao yamechafua jina zuri la Shule hiyo ya Milambo ambayo ina historia ya kutoa vijana wengi wanaojiunga na vyuo vikuu hapa nchini na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

Fundo alisema kuwa wanafunzi waliobaki shuleni ni safi na wako pale kwa ajili ya kusoma na kuendelea mbele zaidi ili waweze kutoa mchango wao kuliendeleza Taifa hilo katika sekta mbalimbali na kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Tanzania ya viwanda.

“Mkuu wa Mkoa tunaomba radhi kwa matukio yaliyofanywa na wanafunzi wenzetu ya kufanya fujo mitaani na kujeruhi watu  na hatimaye wamefikishwa Mahakamani…na wale waliotoroka usiku na kukutwa kuwa wamelala nje…sisi tuliobaki tunakuahidi kuwa ni wanafunzi safi na hatuwezi kushiriki katika vitendo viovu ili kulinda heshima ya Shule yetu” alisema Fundo.

Alisema kuwa ili kuhakikisha wanaondoa dosari iliyojitokeza kupita wanafunzi wenzao ambao hawapo tena shuleni hapo watajitahidi kufanya vizuri katika mitihani ijayo ya Kidato cha Sita ikiwa ni sehemu ya kujutia makosa ya wenzao.

Akizungumza na wanafunzi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri alisema kuwa matukio  yaliyofanywa na baadhi ya wenzao ambao hivi sasa hawapo shuleni hapo  viliitia doa shule hiyo ambayo ina historia nzuri hapa nchini.

Aliwataka wanafunzi ambao wamebaki baada ya kuwaondoa wale waliokuwa na matatizo wazingatie kilichowapeleka Shuleni na watii sheria na taratibu za Shule na zile za nchi ili waweze kutimiza ndoto zao na za wazazi wao.

Mwanri alisema kuwa jambo lolote litakalowafanya washindwe kumaliza masomo yao litakuwa limelisababishia hasara Taifa kwa kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi ili kuhakikisha watoto wanasoma ili waweze kuwa wataalamu katika sekta mbalimbali katika ujenzi wa Taifa.

Matukio ya utovu wa nidhami katika Shule hiyo yalitokea hivi karibuni ambapo yalipelekea wanafunzi 22 kupandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka 12; matano yakiwa ya kujeruhi na saba ya kuharibu mali. Wanafunzi wengine 37 walilazimika kuhamia  Shule nyingine baada ya kupatikana na kosa la kutoroka usiku na baadaye kusamemehewa na Bodi  ya Rufaa ya Mkoa huo.

53 thoughts on “Milambo Waomba Radhi Kwa Utovu wa Nidhamu Uliofanywa na Wenzao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *