Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Miaka 4 ya JPM: TANAPA Yapasua Anga na Kuongeza Watalii na Mapato

 

Kamishna Mkuu wa Uhifadhi (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi, Akizungumza na Waandishi wa Habari( hawapo pichani), Kuhusu mafanikio ya TANAPA kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Jijini Dar es Salaam.

Na.Paschal Dotto

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limesema limejizatiti katika kutekeleza sera ya Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo kwa Miaka minne sasa tangu Serikali ya Dkt.John Pombe Magufuli iingie madarakani TANAPA imepiga hatua katika mikakati yake mbalimbali  mikubwa iliyofanikisha kuinuka kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Uhifadhi, Dkt. Allan Kijazi amesema kuwa TANAPA imeongeza hifadhi za taifa kutoka 16 zilizokuwepo hadi 22, ambapo katika Miaka minne  imeongeza hifadhi sita zikiwemo za Burigi – Chato; Ibanda – Kyerwa; Rumanyika – Karagwe.

Kadhalika, juhudi mbalimbali zinaendelea kufanywa ili kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Selous na kuongeza hifadhi nyingine mpya za Nyerere, Kigosi na Mto Ugala, ambapo zitakuwa zimekamilishwa hifadhi sita za taifa, za  eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 104,559.1

“TANAPA imeweza kufanya mambo makubwa likiwemo la upandishwaji wa mapori kuwa hifadhi za taifa na kukamilisha kuwa na hifadhi 22 nchini, lakini tumeweza kubadili mfumo wa kiutendaji kutoka ule wa Kiraia kwenda Jeshi-Usu, ambapo   muundo mpya wa Shirika letu uliidhinishwa na Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Novemba, 2018.”alisema Dkt. Kijazi.

Akaongeza, “hadi kufikia leo jumla ya watumishi 1,919 ambao ni asilimia 86 ya watumishi 2,230 ambao ni kuanzia ngazi ya Kamishna wa Uhifadhi hadi Askari wa Uhifadhi wa kada mbalimbali, wamepatiwa mafunzo ya mabadiliko ya mfumo.”

Katika kipindi cha miaka minne, TANAPA imeweza kuongeza mapato kutoka shilingi 175,089,696,000 kwa mwaka wa fedha 2015/16; shilingi 207,587,218,000  kwa mwaka 2016/17 na shilingi 254,794,242,000 mwaka 2017/18 na kufikia kiasi cha shilingi 279,406,200,806 mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni ongezeko la shilingi 566,697,964,806 kwa miaka mitatu sawa na asilimia 60.

Dkt. Kijazi alisema kuwa ongezeko la mapato ya Shirika limetokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa ndani na nje ya nchi ili kuyafikia masoko mapya ambapo liliwezesha kuwa na ongezeko la watalii kutoka wageni 957,576 mwaka 2015/16 hadi 1,141,462 mwaka 2018/19 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.2, hii ni kutakana na juhudi kubwa ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikizifanya ili kuinua uchumi kupitia utalii.

 

Kamishna Mkuu wa Uhifadhi (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi, Akizungumza na Waandishi wa Habari (pichani), Kuhusu mafanikio ya TANAPA kwenye miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi cha miaka minne TANAPA imeongeza kuchangia mapato kwa serikali kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2016/2017, hadi kufikia shilingi bilioni 42 kwa mwaka wa fedha 2018/2019, pia imeweza kutenga fedha kiasi cha shilingi 111,374,526,023.00, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni uimarishaji wa huduma za utalii, ikiwemo ujenzi wa maeneo ya malazi ya gharama nafuu (mabanda na hosteli), miradi ya kuongeza bidhaa za utalii, nyumba za wafanyakazi, vifaa vya kazi kama boti, magari na ndege kwa lengo la kuongeza watalii ndani na nje ya nchi.

Aidha TANAPA imetekeleza agizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kukomesha ujangili ambapo katika kipindi hiki cha miaka minne, TANAPA imeweza kuimarisha mifumo ya ulinzi wa wanyamapori na ustawi wa wanyama adimu na kupelekea ongezeko la wanyama adimu jamii ya faru kwa asilimia 10 katika Hifadhi za Taifa, na kudhibiti vitendo vya ujangili kwa zaidi ya asilimia 90. Aidha Majangili 14,464 wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo mbalimbali ya dola nchini.

“Ongezeko la wanyama kutokana na kuimarisha ulinzi limeleta mafanikio makubwa sana kwa upande wa watalii kwa sasa wameongezeka kutoka 518,457 hadi 715,314 kutokana na kuongezeka kwa wigo wa soko la utalii katika masoko mapya katika Bara la Asia na Mashariki ya Mbali, hususani Israeli, Uturuki, China na Urusi, na hii imesababisha kuwepo na mahitaji makubwa ya malazi”, Alisema Dkt. Kijazi.

Alio ngeza kuwa katika ongezeko hilo la watalii mpaka sasa vitanda vimeongezeka kutoka 2400 hadi kufikia vitanda 5,829 vya watalii wa nje (international tourists), na vitanda 3,601 hadi kufikia 4,970 vya wageni wa ndani (domestic tourists) na kufanya jumla ya vitanda vyote kufikia 10,799.

262 thoughts on “Miaka 4 ya JPM: TANAPA Yapasua Anga na Kuongeza Watalii na Mapato

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama