Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mgalu aonya matapeli miradi ya REA

Sehemu ya wakazi wa kata Zogoali katika wilaya ya Ilala wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani).

Mmoja wa wakazi wa kata ya Bomba Mbili iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, Dkt. Isaya Madama akitoa kero yake mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani).

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kwa matapeli wanaojitokeza kwa kujifanya maafisa wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuwatoza wananchi fedha kama malipo ya kuunganishiwa huduma ya umeme.

Mgalu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki  katika  mikutano aliyoifanya wakati wa ziara  yake katika  katika kata za Bomba Mbili, Mbondole,  Kiboga, Zogoali,  Kigezi Buyuni na Chanika zilizopo katika wilaya ya  Ilala nje kidogo ya Jiji la  Dar es Salaam.

Lengo la ziara yake lilikuwa ni kutembelea maeneo  ambayo hayajafikiwa  na miundombinu ya umeme, kuzungumza na wananchi na kuweka mikakati ya  namna ya kumaliza changamoto hizo kwa kushirikiana na REA na  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akinukuu maswali mbalimbali yaliyokuwa yanauliuzwa na wakazi wa kata ya Bomba Mbili iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) Kulia ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na sehemu ya wakazi wa kata ya Zogoali iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara katika kata hiyo.

Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kata husika walilalamika kuwepo kwa  tabia ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijitambulisha kwao kama maafisa kutoka REA na  TANESCO na kuwachangisha  fedha nyingi  ili wawaunganishie huduma ya umeme kinyume na taratibu.

Walisema kuwa baada ya kufanya malipo kwa watu hao walishangaa kuona wametoweka na fedha hizo pasipo kuwapatia huduma ya aina yoyote.

Akifafanua kero hiyo, Mgalu alitoa wito kwa wananchi kutoa  taarifa katika vyombo vya usalama pindi watu wasiofahamika wanapojitokeza na kudai michango kwa ajili ya kuwaunganishia huduma ya umeme.

Aliongeza kuwa wakandarasi kabla ya kuanza kazi ya kuweka miundombinu ya umeme katika kata husika, wanatakiwa kujitambulisha kwa viongozi wa mtaa ili waweze kutambulishwa kwa wananchi.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya umeme Serikali imetoa punguzo kubwa ambapo kila mwananchi aliyepo ndani ya miradi ya REA atatakiwa kuchangia  gharama ya shilingi 27,000 tu.

Vilevile aliwataka wananchi kujiandaa kwa kuunganishiwa na huduma ya umeme kupitia REA kwa kutandaza nyaya za umeme kwenye nyumba zao kupitia wakandarasi wanaotambulika na TANESCO

107 thoughts on “Mgalu aonya matapeli miradi ya REA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *