Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mawakili Watakiwa Kujikita Vijijini

Mgeni Rasmi Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (wanne toka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji na Mawakili wapya mara baada ya kuwaapisha mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.(Picha na: Eliphace Marwa)

Na. Eliphace Marwa

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya uwakili na kutumia taaluma zao kwa kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.

Aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za 56 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 248 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Mgeni Rasmi Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akifuatilia jambo wakati wa sherehe za 56 za kuwakubali na kuwasajiri, Mawakili wapya 248 mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Aidha Kaimu Jaji Mkuu amewahimiza Mawakili wapya kujiendeleza kitaaluma kwa sababu kuwa wakili sio mwisho wa taaluma kwani wanahitajika kusoma sheria za nchi mbalimbali Duniani ili kuweza kuingia mikataba ya kimataifa.

Alisema mawakili wapya wanatakiwa washiriki katika kutoa haki, wawe waaminifu kwa mahakama na wateja kwani wakienda kinyume haki itapotea.

“Mawakili wote wanatakiwa kuwa waaminifu kwa wateja wanaowahudumia na kushirikiana na mahakama katika kutoa haki na wasiwe mawakala wa rushwa bali wawe mawakala wa kutenda haki,” alisema Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim.

Baadhi ya ndugu wa Mawakili wapya wakisubiri zoezi la kuapishwa kwa ndugu zao mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Aidha Kaimu Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao kufika maeneo ya nje ya mji ili wasaidie upatikanaji wa haki kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya mawakili katika maeneo ya nje ya miji.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) Tundu Lissu amewataka Mawakili hao kutumia taaluma hiyo katika kuisaidia jamii kujua haki zao na utawala wa sheria japo kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya sheria nchini.

Baadhi ya Mawakili wapya wakisubiri zoezi la kuapishwa mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

“Napenda kuwatakia kila la kheri mawakili hawa wapya ila niwaombe watumie taaluma hii kwa kuisaidia jamii kujua haki zao pamoja na utawala wa sheria,” alisema Mh. Tundu Lissu.

 Idadi ya mawakili walioapishwa leo imepelekea Tanzania kuwa na idadi ya zaidi ya mawakili 6300.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail