Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mama Tarishi Astaafu Ukatibu Mkuu, Ashauri Utumishi wa Umma wa Kibiashara

Aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Bi. Maimuna Tarishi, akimkabidhi taarifa ya makabidhiano ya Ofisi hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Bi. Dorothy Mwaluko, tarehe, 9 Septemba, 2019, Jijini Dodoma.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Bi. Maimuna Tarishi, ambaye amehudumu katika  ofisi hiyo tangu, tarehe 4 Aprili, 2017, amestaafu rasmi  utumishi wa umma, huku akiwashauri watumishi wa umma wanaobaki katika utumishi huo kutekeleza majukumu ya  utumishi wa umma kibiashara.

“Ninapozungumzia Utumishi wa Umma wa kibiashara siimanishi kuuza na kununua bidhaa fulani, kimsingi ninachokusudia hapa ni kuwa watumishi wa umma wanaobaki katika utumishi huo nawashauri utendaji wao wa majukumu uwe unajikita katika kuwezesha na sekta nyingine zinastawi ili kupata matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa watanzania wanao wahudumia” amesema Tarishi

Bi.Tarishi amefafanua kuwa katika kuhakikisha kuwa utumishi wa umma wa kibiashara  unatekelezwa lazima watumishi wa umma watekeleze majukumu yao kwa wakati na   kasi inayotakiwa,  kutumia weledi na ubunifu pamoja na  kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pia kuhakikisha viwango bora vya huduma na lazima matokeo chanya yanapatikane kwa huduma wanazo zitoa kwa wananchi.

Akiongea wakati akiwaaga rasmi, watumishi wa Ofisi hiyo, tarehe 9 Septemba 2019, jijini Dodoma, Bi.Tarishi alieleza kuwa utumishi wa umma ndiyo injini ya kufanyika kwa shughuli zote katika nchi yoyote duniani. Ameeleza kuwa bila utumishi wa umma sekta  nyingine zikiwemo sekta binafsi haziwezi kustawi,  hivyo utumishi wa umma ukitekelezwa  kibiashara huduma zinazotolewa na serikali zitawafikie wananchi wanao wahudumia  na zitakuwa na matokea chanya.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Bi. Maimuna Tarishi, akiongea na watumishi wa Ofisi hiyo wakati akiwaaga rasmi baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria, tarehe, 9 Septemba, 2019, Jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine, Bi Tarishi amemshukuru Rais wa Jamhuri yas Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kulitumikia Taifa kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Aidha, amemshukuru Mhe. Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, kwa miongozo na maelekezo yaliyomsaidia kutekeleza majukumu yake. Bi Tarishi hakusita kushukuru ushirikiano mzuri aliopata kutoka kwa Mawaziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Mhe. Jenista Mhagama na Mhe. Angellah Kairuki pamoja na Katibu Mkuu anayeendelea kuhudumu kwenye ofisi hiyo, Bi. Dorothy Mwaluko,  pia na watumishi wa ofisi hiyo.

Akiongea katika mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Bi. Dorothy Mwaluko alifafanua kuwa watumishi wa Ofisi hiyo hawana budi kuwa wabunifu, watiifu na waaminifu na kutumia weledi  katika kutekeleza majukumu yao ili kuweza kuhakikisha aliyoyasisitiza Katibu Mkuu mstaafu yanakuwa katika vitendo.

Katibu Mkuu Mstaafu, Bi Maimuna Tarishi aliaza rasmi utumishi wake wa umma tarehe 6 Mei, 1985 na amestaafu utumishi huo tarehe, 7 Septemba, 2017. Awali kabla ya kuwa  Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu amewahi pia kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kabla ya kuhamia Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge).

Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Waziri Mkuu), Bi. Maimuna Tarishi,(hayupo pichani) wakati alipokutana na watumishi hao kuwaaga rasmi baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria, tarehe, 9 Septemba, 2019, Jijini Dodoma.

208 thoughts on “Mama Tarishi Astaafu Ukatibu Mkuu, Ashauri Utumishi wa Umma wa Kibiashara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama