Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Makamu wa Rais Aagiza Kupitiwa Upya Usajili wa Meli

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)leo Jijini Dar es Salaam kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kukamatwa kwa Meli zenye Bendera ya Tanzania zikiwa zimebeba Silaha na Madawa ya kulevya katika maeneo ya Ubelgiji na Jamhuri ya Dominican Republic

Na: Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba kuunda Kamati ya pamoja ya wataalam kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kupitia upya usajili wa meli nchini.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo mbele ya Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya meli zilizokamatwa zikiwa na Bendera ya Tanzania.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kukamatwa kwa Meli zenye Bendera ya Tanzania zikiwa zimebeba Silaha na Madawa ya kulevya katika maeneo ya Ubelgiji na Jamhuri ya Dominican Republic mapema hivi karibuni. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Usajili wa Meli kutoka Sumatra (jina halikufahamika), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Meli Zanzibar (ZMA) Bw. Abdallah Kombo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba.

Mhe. Samia amesema kuwa suala la usajili wa meli za nje ni la kawaida na linafanywa na nchi nyingi duniani hivyo Serikali inaendelea kushughulikia taarifa juu ya meli za nje zilizosajiliwa Tanzania zenye tuhuma za kusafirisha silaha na dawa za kulevya kwa sababu ni kinyume cha sheria za usajili wake.

“Kwa kuwa uendeshaji wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari kubwa kwa Taifa letu na kuharibu sifa njema kwa nchi yetu, tumeona ipo haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalam kutoka Tanzania Bara na Zanzibar itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitia upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili na hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali”, alielezaa Makamu wa Rais.

Kamati itakaundwa pia itapitia sheria za usajili wa meli ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili huo hivyo kamati itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania.

Aidha, Mhe. Samia amsema agizo lakupitiwa upya sharia za usajili wa meli baada ya kubainika kuwa wamiliki wa meli wanapenda kusajili meli zao nje ya nchi zao kukimbia ukubwa wa kodi na sheria zinazobana pia wakala aliyekuwa akifanya kazi hizo kwa niaba ya taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) alishavunjiwa mkataba lakini bado anaendelea kufanya usajili kwa kuiba bendera ya Tanzania.

Kutoka kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Meli Zanzibar (ZMA) Abdallah Kombo na Mkurugenzi wa Usajili wa Meli toka Sumatra wakimsikiliza Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. (Frank Shija)

Amefafanua kuwa Sheria na Kanuni zote za usajili zinamlazimu mimiliki wa meli kujaza fomu ya kiapo cha kutovusha biashara za dawa za kulevya wala silaha kinyume na utaratibu hivyo Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa kukamatwa kwa meli hizo sio makosa ya Tanzania ila nchi inahusishwa kwa kuwa usajili wa meli hizo umefanyika Tanzania.

Meli mbili, Kaluba yenye namba za usajili IMO 6828753 na Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 zilizosajiliwa Tanzania kupitia taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zilikamatwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya na silaha ambapo hadi sasa tayari zimeshachukuliwa hatua ya kufutiwa usajili.

Tanzania ina aina mbili za usajili wa meli ambao ni usajili wa meli zenye asili ya Tanzania na zisizo asili ya Tanzania, usajili huo ni kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS wa mwaka 1982 ambapo kila nchi imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi husika.

SUMATRA inaruhusu usajili wa meli zinazomilikiwa na Watanzania au kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine ambapo jumla ya meli 88 zimesajiliwa wakati meli za kimataifa zinasajiliwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) ambazo hadi Disemba 31, 2017 jumla ya meli 457 za nje zimesajiliwa.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail