Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Majaliwa: Serikali Kuimarisha Masoko ya Mazao

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kupata tija.

 Aliyasema hayo jana (Februari 2, 2018) wakati akikagua Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha masoko.

 Alisema kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imedhamiria kuimarisha masoko  ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kujikwamua kiuchumi.

 “Kupitia Wizara ya Kilimo tunataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini. Wakati umefika kwa wakulima nchini kuona tija ya mazao wanayolima.”

 Alitoa mfano wa zao la pamba ambalo wakulima walikuwa wanaingia mikataba na wanunuzi, mfumo ambao ulikuwa unawanyonya badala ya kuwanufaisha.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX, Bw. Godfrey Malekano alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamejipanga vyema kuanza minada ya mazao.

“Tutaanzia na zao la ufuta mwezi Mei 2018 na kuendelea na mazao mengine kwa kadiri ya misimu ya mazao hayo ilivyo.”

Alisema kufanikiwa kwa Soko la Bidhaa na Mfumo wa stakabadhi ghalani kunategemea sana msaada wa Serikali.  “Soko la Bidhaa la Ethiopia linalotajwa sana kwa mafanikio, limefikia malengo yake kutokana na mkono wa Serikali.”

 Bw. Malekano alisema kutokana na umadhubuti wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli wanamatumaini makubwa kwamba soko hilo  litatimiza malengo yake.

 IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAMOSI, FEBRUARI 3, 2018.

159 thoughts on “Majaliwa: Serikali Kuimarisha Masoko ya Mazao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama