Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Majaliwa Kufunga Mkutano Mkubwa wa Wadau Sekta ya Madini

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari Nchini (hawapo pichani) leo katika ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano mkubwa wa madini utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 21 hadi 23,2020.

Na.Mwandishi wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mkutano mkubwa wa sekta ya madini utakaoambatana na utoaji wa cheti cha umahiri kwa madini ya bati utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam Jumamosi wiki hii.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema mkutano huo wa aina yake utafungua fursa kwa wadau wa madini wakiwemo wafanyabiashara ,watafiti na hata wawekezaji wakubwa kuja kuchangamkia fursa zilizosheheni katika sekta hiyo hapa nchini.

“Mkutano huo wa wadau ni muhimu sana kwani utaambatana na maonyesho ya shughuli mbalimbali za sekta ya madini na utatoa fursa kwa wadau kuongeza wigo wa kupanua biashara ya madini, na pia utafanyika uzinduzi rasmi wa cheti cha umahiri kwenye madini ya bati” Alisema Naibu Waziri.

Alisema cheti cha umahiri ni nyenzo muhimu katika sekta ya madini, kwani nchi yetu itatambulika rasmi duniani kama wazalishaji wa madini hayo hivyo kuwa na utambulisho mahsusi hasa madini hayo yanapokuwa yameuzwa katika nchi za nje.

Naibu Waziri Nyongo amesema kupatikana kwa cheti hicho ni kutokana na Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini  pamoja na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha rasilimali madini zinalinufaisha taifa na wananchi wake kwa ujumla.

 Amesema Tanzania iliridhia itifaki ya kimataifa ya udhibiti wa uuzaji wa madini ambapo madini yanatakiwa yajulikane yalikochimbwa, yalivyosafirishwa na hata thamani yake ili kudhibiti vitendo vya kuibuka kwa vikundi vyenye silaha, vinavyopambana na serikali hasa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwingineko ambapo madini imekuwa chanzo kikubwa cha fedha za kununulia silaha na kufadhili vikundi hivyo.

Mkutano huo wa siku mbili utaambatana pia na kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zinazohusu sekta ya madini zitakazowasilishwa na wadau na wasomi mahiri katika sekta ya madini akiwemo Profesa Shukrani Manya, Profesa Hamis Mruma pamoja na Profesa mahiri kutoka nchini Kenya katika chuo Kikuu cha Nairobi P.L.O Lumumba.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano Kuingia Madarakani mwaka 2015 sekta ya madini imeanza kuzaa matunda kwa kuliingizia taifa fedha nyingi kutokana na udhibiti wa utoroshaji wa madini, ujenzi wa ukuta katika machimbo ya Tanzanite Mirerani mkoani Manyara , pamoja na ujenzi wa masoko ya madini katika kila mkoa na baadhi ya Wilaya.

 

397 thoughts on “Majaliwa Kufunga Mkutano Mkubwa wa Wadau Sekta ya Madini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama