Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Majadiliano Sekta ya Umma na Binafsi Chachu Ukuaji wa Uchumi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (kulia) pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dkt. Godwill Wanga (kushoto) baada ya uzinduzi wa Muongozo wa majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi ya Mikoa na Wilaya uliofanyika leo jijini Dodoma.

Na Jacquiiline Mrisho

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa majadiliano ya mabaraza ya biashara yanayofanyika katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya yameendelea kusaidia uchumi wa nchi kuimarika.

Waziri Mhagama ameyazungumza hayo leo Jijini Dodoma wakati akizindua Muongozo wa majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi ya Mikoa na Wilaya uliofanyika jijini humo ambapo amesema kuwa inawezekana mabaraza ya biashara  yalikuwa hayafanyiki vizuri kwa sababu watu walikuwa wanashindwa kutumia mazingira waliyonayo kujipanga kuendesha mabaraza haya lakini, muongozo huo utasaidia watu kukutana kwa ajili ya majadiliano yenye tija.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia) akikabidhiwa kitabu cha Muongozo wa Majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi za Mikoa na Wilaya na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dkt. Godwill Wanga (kushoto). Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa muongozo huo.

“Ili kuwa na utendaji unaotukuka lazima tuwe na muongozo wa nini kifanyike, wakati gani, kwa utaratibu upi na kwa rasilimali zipi, hatuwezi kuzungumza uchumi wa viwanda wala utekelezaji wa Dira ya Maendeleo bila sekta binafsi hivyo kuna kila haja ya kutengeneza mazingira wezeshi yatakayoifanya sekta ya umma isaidiane na ishirikiane kwa karibu na sekta binafsi ili yaliyopangwa yaweze kutekelezwa”, alisema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesisitiza wahusika kutoa mrejesho wa majadiliano ya mabaraza ya biashara katika ngazi za mikoa na wilaya kwani kama yatafanyika maamuzi na kujiwekea malengo ambayo hayatekelezeki hakutakuwa na maana ya vikao hivyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amesema kuwa muongozo huo ni kitendea kazi katika ngazi zetu za mikoa na wilaya kitakachowezesha uendeshaji wa mabaraza haya ambayo kwa kiasi kikubwa yataleta tija.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kitabu cha Muongozo wa Majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi za Mikoa na Wilaya.Amepokea kitabu hicho kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchi nzima.

“Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Mikoa 26 ni mikoa 16 pekee ambayo ilifanya mabaraza hayo, sasa muongozo umeshatolewa hivyo miongoni mwa taarifa za wakuu wa Mikoa zinazoletwa TAMISEMI lazima taarifa ya Uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara  katika mikoa yenu iwepo”, alisema Waziri Jafo.

Vile vile, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dkt. Godwill Wanga amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia majadiliano kati ya sekta hizo mbili ambapo inasimamia kwa karibu majadiliano hayo kama njia muafaka ya kufikia maridhiano yatakayoboresha uchumi na maendeleo endelevu ya nchi.

“TNBC tunatoa wito kwa wadau wote kutumia majadiliano haya kuainisha matatizo ya miradi ya pamoja kati ya sekta hizi mbili inayolenga kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini”, alisema Dkt. Wanga.

Akiishkuru Serikali ya Awamu ya Tano, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPFS), Rehema Mbogi amesema kuwa Serikali imeonesha umakini katika masuala yanayohusu majadiliano kati ya Sekta Binafsi na Umma katika ngazi zote kwani sekta binafsi imekua ikishirikishwa katika mabaraza ya biashara pamoja na kupata nafasi za kujadiliana masuala mbalimbali viongozi wa Serikali.

“Mnamo mwaka juzi nilishiriki katika mkutano nchini Afrika Kusini uliohusu mfumo wa majadiliano katika nchi za Kusini mwa Afrika nilifurahishwa kuona kwamba nimesimamishwa kuelezwa kwamba nchi yetu Tanzania ina mfumo bora wa majadiliano unaoeleweka kuanzia ngazi ya Taifa hivyo hii ni fursa nzuri ambayo tukiitumia vizuri tunaweza kufika mbali katika nchi”, alisema Bi.Rehema.

 

123 thoughts on “Majadiliano Sekta ya Umma na Binafsi Chachu Ukuaji wa Uchumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama