Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Maafisa Utumishi Waaswa Kuzingatia Weledi Katika Kutekeleza Majukumu Yao

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha kujadili masuala ya Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara , Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichoandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora kinachofanyika Mjini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa Maafisa Utumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuongeza tija katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa hiyo ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Musa Iyombe akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha siku mbili cha kujadili masuala ya Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara , Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichoandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora kinachofanyika Mjini Dodoma.

                                                                       Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma

Waziri  wa Nchi  Ofisi ya  Rais TAMISEMI  Mhe. Selemani Jafo amewataka Maafisa Utumishi wa  Mikoa na Halmashauri zote nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuongeza ari ya watumishi wa umma katika kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi.

Akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi cha Siku mbili kilichowahusisha Wakurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Maafisa Utumishi wa Halmashauri zote hapa nchini mapema leo mjini Dodoma Waziri Jafo amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kuona changamoto za Watumishi wa Umma zinatatuliwa kwa wakati.

“Maafisa Utumishi mnalo jukumu kubwa lakuwasaidia watumishi katika maeneo yao kwa kufanya kazi zenu kwa kuzingatia weledi, kuepuka rushwa, vitendo vya upendeleo na mambo yote yanayoweza kuchafua taswira ya Serikali kupitia huduma mnazotoa” Alisisitiza Mhe.  Jafo

Akifafanua zaidi Waziri Mhe. Jafo amesema kuwa wajibu wa Maafisa Utumishi ni kuwa Kiungo kati ya Wakurugenzi na watendaji wa Taasisi  hali itakayosaidia kupunguza au kuondoa malalamiko yanayofikishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Aliongeza kuwa Maafisa Utumishi wanajukumu kubwa katika kuhakikisha watumishi wanapandishwa madaraja kwa wakati, wanathibitishwa  kazini kwa wakati  ili kuwaongezea morali kwa watumishi hali itakayoongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Pia aliwaasa  Maafisa Utumishi kuhakikisha kuwa  Wanatunza taarifa zote za Watumishi kwa kuzingatia sheria , Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kulinda maslahi mapana ya nchi.

Kwa upande Wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhandisi Musa Iyombe amewataka Maafisa Utumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuleta mabadiliko kwa wananchi kwa kuwapa huduma bora.

Sehemu ya washiriki wa Kikao Kazi cha siku mbili cha kujadili masuala ya Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara , Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichoandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora kinachofanyika Mjini Dodoma.

Aidha, Mhandisi Iyombe aliwaasa kuacha kufanya kazi kwa mazoea  hali inayopelekea kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa watumishi na hivyo kuzorotesha kasi yakuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Bw. Mathias Kabunduguru akizungumza katika Kikao Kazi hicho amesema kuwa baadhi ya masuala yanayoleta kero kwa watumishi wa Umma ni pamoja na Mamlaka za Ajira kukataa kuidhinisha au kupitisha barua za watumishi kuhama, hivyo aliwaasa Maafisa hao kutozuia maombi ya watumishi wanaoomba kuhama.

“Mamlaka husika inaweza kuweka maoni yakuomba mbadala wa Mtumishi anayeondoka na sikuzuia barua yake yakuomba uhamisho kwa kuwa uhamisho  wa watumishi unajengwa kwa Misingi ifuatayo, kwanza mtumishi anayohaki ya kufanya kazi popote,Uhamisho hujenga Afya ya Utumishi kwa ujumla na pia swala hilo husaidia Kujenga umoja wa Kitaifa.

Aliongeza kuwa Kikao Kazi hicho kitakuwa chachu ya kuimarisha Uadilifu,Uwajibikaji,Uwazi, na misingi mingine ya Utawala Bora.

’’Pamoja na Kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Vyeti vya Kidato cha nne, Sita, Ualimu na Vyuo Vikuu bado wapo waajiri aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya wameendelea kuwafumbia macho watu wenye vyeti bandia ambapo wiki iliyopita tulilazimika kuchukua hatua kali dhidi ya Maafisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kutokana na kuficha watu wenye vyeti Bandia” Alisisitiza Bw. Kabunduguru.

Akizungumzia swala la kutambua mchango wa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii Bw. Kabunduguru amesema linaongeza ari yao katika kutekeleza majukumu yao hivyo ni vyema utaratibu wa kuwatambua hata kwa kuwaandikia barua za kutambua mchango wao na pia kuwaadhibu watumishi wazembe wasiotekeleza majukumu yao.

Kikao Kazi  hicho cha siku Siku mbili kilichowahusisha Wakurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Maafisa Utumishi wa Mikoa, Halmashauri zote hapa nchini  kinafanyika mjini Dodoma kimeandaliwa kwa ushirkiano wa Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala bora na Ofisi ya Rais TAMISEMI kikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha utendaji na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

 

169 thoughts on “Maafisa Utumishi Waaswa Kuzingatia Weledi Katika Kutekeleza Majukumu Yao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *