Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Lukuvi Azindua Baraza la Taifa la Ushauri wa Ardhi

Na Jonas Kamaleki – Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amezindua Baraza la Taifa la Ushauri wa Ardhi leo jijini Dodoma na kuwataka wajumbe wa baraza hilo kufanya kazi kwa kujitolea badala ya kusubiri vikao.

Akizindua Baraza hilo, Waziri Lukuvi amewataka wajumbe waishauri Serikali juu ya matumizi bora ya ardhi ikiwemo upimaji na upangaji kila kipande cha ardhi kwa matumizi bora na endelevu.

“Natoa rai kwenu mtushauri namna ya kupunguza gharama za upatikanaji wa hati na kwa uharaka ili hata mtu wa kipato cha chini aweze kumiliki ardhi salama”, alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kubadili muundo wa usimamizi wa ardhi ambao una lengo la kuondoa urasimu katika kushughulikia masuala ya ardhi kwani hayo yote yatakuwa chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tofauti na ilivyo kuwa awali.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, atua hii itaharakisha upatikanaji wa hati kwa wananchi na kwa gharama nafuu.

“Kanda kwa sasa hazifai kwa utoaji hatimiliki za ardhi kwani ni vigumu mtu mmoja kuhudumia mikoa mitatu hadi minne kwenye Kanda, napendekeza masuala ya ardhi yashughulikiwe mikoani ili kupunguza gharama zisizohusiana na taratibu za utoaji ardhi, kwa mfano kusafiri mwendo mrefu kufuatilia hati kwenye Kanda, hii haifai tena”alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema Serikali itahakikisha sehemu kubwa ya ardhi nchini imepimwa na kupangiwa matumizi sahihi kuliko ilivyo sasa ambapo asilimia 20 tuya ardhi nchini ndiyo imepimwa.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi, Waziri Lukuvi amesema kuwa utatuzi huo hasa vijijini haufanyiki vizuri na kuongeza kuwa inabidi mabadiliko yafanyike ikiwemo kuwajengea uwezo watutuzi wa migogoro hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Fidelis Mutakyamilwa, amesema Baraza lake liko tayari kufanya kazi kwa moyo na kufanya utafiti wa masuala ya ardhi pasipo kusubiri vikao.

Amemshukuru Waziri kwa kuteua Baraza hilo kwani litafanya kazi ya kuishauri Serikali katika masuala ya ardhi ambayo ni maisha ya watu.

Hili baraza la kwanza kuteuliwa kwa ajili ya kuishauri Serikali kwa masuala ya ardhi tangu kuatungwa kwa Sheria ya Ardhi inayotumika sasa.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail