Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kwandikwa Ataka Kiwanja cha Ndege Mtwara Kukamilika Mwezi Machi

Na Mwandishi Wetu – WUUM

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering kukamilisha kazi ya kuongeza urefu wa barabara ya kurukia na kutua ndege kutoka mita 2,258 za sasa hadi mita 2,800 katika Kiwanja cha Ndege cha Mtwara ili kiweze kuhudumia ndege kubwa za aina zote.

Amesema kuwa ongezeko la abiria wanaokwenda nchi za nje limefanya Serikali kuendelea kuboresha Viwanja vya Ndege vingi vya kikanda hapa nchini.

Amezungumza hayo mkoani Mtwara, wakati akikagua hatua za maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho na kuridhishwa na kasi yake ambapo pamoja na mbo mengine amesisitiza uboreshaji wa njia za kuruka na kutua ndege kuwa  ni wa kipaumbele ili kufungua Kiwanja hicho mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

“Mkandarasi na wasimamizi  mmenisikia hadi kufikia mwezi Machi watu waweze kushuka hapa na kupanda ndege kubwa kama Dreamliner katika uwanja huu”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Aidha, Kwandikwa ameongeza kuwa jumla ya fedha zinazotarajiwa kutumika katika ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho ni kiasi cha shilingi bilioni 50.366 na  kazi zote zinatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2020.

Naibu Waziri huyo ameeleza ukarabati mwingine unaoendelea katika kiwanja hicho ikiwa ni kujenga barabara ya magari ya kuingia kiwanjani pamoja na maegesho yake, kupanua njia ya kurukia na kutua ndege kutoka na upana wa mita 30 za sasa hadi mita 45, kujenga upya matabaka ya barabara ya kurukia na kutua ndege,  kujenga maegesho mapya ya ndege katika eneo jipya la ‘Master Plan’.

Kazi nyingine ni kujenga uzio wa usalama kuzuguka kiwanja, kuweka taa pamoja na alama za kuongozea ndege, kuweka mfumo wa umeme wa akiba, kuweka vifaa vya zimamoto na kujenga matenki ya kuhifadhi maji, kujenga barabara moja ya kiungio (Taxiway) katika eneo jipya la ‘Master Plan’.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda, ameishukuru Serikali kwa jitahida za kuboresha kiwanja hicho kwa kuwa hapo awali walikuwa hawanufaishwi kutokana na kuwa uwanja huo kuwa mdogo lakini sasa Mtwara inaendelea kufunguka kwa upande wa baharini,  nchi kavu na angani.

“Kukamilika kwa upanuzi wa Kiwanja hichi kutaisaidia kukuza uchumi wa Mtwara kwani utarahisisha sana usafirishaji wa mazao na bidhaa kwenda nchi za nje na nchi jirani kama visiwa vya Comoro”, amesema Bw. Mmanda.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mtwara Mhadisi Doto Chacha,  amesema kwa ujumla utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 30 na amemhakikishia Naibu Waziri huyo kukamilisha haraka na kwa viwango ongezeko la urefu wa mita 542 wa barabara ya kurukia na kutua ndege kabla ya mwezi Aprili mwaka huu.

Ukarabati na Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara unatarajiwa kutoka katika Daraja Code 3C ya sasa kwenda Code 4E (kwa mujibu wa ICAO) ambao utaweza kuhudumia ndege kubwa kama vile Boeing 787-8 (Dreamliner) na ndege zingine za nje ya nchi zinazotua katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

150 thoughts on “Kwandikwa Ataka Kiwanja cha Ndege Mtwara Kukamilika Mwezi Machi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama