Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kiwanja cha Ndege Msalato Kuanza Kujengwa

Serikali imewatoa wasiwasi wafanyabiashara na watumiaji wa usafiri wa anga kwa kuahidi kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Msalato jijini Dodoma mara baada ya taratibu zilizobaki kukamilika.
 
Akizungumza mjini humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege na sehemu ya maegesho ya ndege, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kurahisisha usafirishaji kwa kuruhusu mashirika mengi zaidi kutumia kiwanja hicho.
 
“Niwahakikishie watanzania kuwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitajengwa na kwa wakazi wa Dodoma ambao wanadai fidia, Serikali itahakikisha wanalipwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
 
Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi ya ndege ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
  
Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha usafiri wa anga nchini kwa kuendelea na miradi mikubwa ya uboreshaji wa viwanja vya ndege zaidi ya kumi na moja nchi nzima vikiwemo vya Lindi, Songea, Shinyanga, Musoma, Songwe na Mtwara.
 
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amesema mradi umefikia zaidi ya asilimia 70 na kuahidi kuendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha viwango vinazingatiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *