Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola kufanya Ziara Nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Dkt.Aziz Mlima akizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani, kuhusu ujio wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Convention Center Jijiji Dar es Salaam.

Na: Thobias Robert- MAELEZO

Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola Mh. Patricia Scotland anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini.

Hayo  yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima wakati alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Madola  atafanya ziara  ya siku tatu nchini kuanzia  Agosti 10 hadi 12 mwaka huu, ambapo atakutana na viongozi wa juu wa serikali ya Tanzania.

“Lengo la ziara hiyo nchini  ni kuelezea viongozi wa ngazi za juu wa Tanzania kuhusu mageuzi yanayofanywa na Sekrtarieti ya Jumuiya ya Madola na  vipaumbele  vya Jumuiya hiyo  kwa sasa, hatua zinazochukuliwa ili kuimarisha kazi za Jumuiya hiyo na kutoa taarifa kuhusu  Mkutano wa Wakuu wa Nchi na serikali wa Jumuiya unaotarajiwa kufanyika jijini  London nchini Uingereza  mwakani mwezi April” alisema Dkt. Mlima.

Alifafanua kuwa mageuzi yanayotarajiwa kufanywa na Jumuiya hiyo ni pamoja na kuondoa vyeo vya Naibu Makatibu wakuu watatu na kupunguza idadi ya Wakurugenzi kutoka 12 hadi 6, kuanzisha nafasi tano za Maafisa Waandamizi kutoka maeneo ya kijiografia ya Jumuiya hiyo kwa maana ya Afrika, Ulaya, Amerika, Karibeani, Asia na Pacific Kusini kwa lengo la kuziba nafasi ya Makatibu Wakuu.

“Mageuzi haya yataiwezesha Jumuiya ya Madola kuokoa kiasi cha Pauni milioni 3 kwa mwaka ambazo zitafanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo,” alifafanua Dkt. Mlima.

Katika ziara yake nchini,  Katibu Mkuu huyo  wa Jumuiya ya Madola anatarajiwa kukutana na  kufanya  mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,  Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mbali na kukutana na Rais Magufuli,  Katibu Mkuu Scotland  atafanya mazungumzo  na Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba.

Jumuiya ya Madola ilianzishwa karne ya 20 kwa lengo la kuikutanisha Uingereza na yaliyokuwa makoloni yake duniani kwa jukumu la kuhakikisha wanachama wanajikwamua  katika nyanja za Kisiasa, Kiuchumi, kijamii, Michezo na Burudani huku Malkia wa Uingereza ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo.

Mpaka sasa Jumuiya  hiyo ina  nchi wanachama 53, huku Tanzania ikiwa ni moja ya wanachama   ambapo imeshika nyadhifa mbalimbali, kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015 Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa kundi la Mawaziri la Utekelezaji la Jumuiya ya Madola likiwa na jukumu la kusimamia misingi mikuu ya Jumuiya hiyo.

Aidha, Tanzania ni mjumbe katika Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) ambapo mwaka 2007 hadi 2014 Marehemu Dkt. William F. Shija aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge hilo.

Hivi karibuni katika kikao  cha Maspika wa Bunge la Jumuiya ya Madola Afrika kilichofanyika mjini  Abuja nchini Nigeria, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na kuwa Spika wa kwanza  kutoka Tanzania kupata nafasi hiyo.

49 thoughts on “Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola kufanya Ziara Nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *