Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kaimu Mkurugenzi Mkuu REA Atoa Angalizo kwa Wakandarasi wa Umeme Vijijini

Zahanati ya Mwamakiliga wilayani Nyang’hwale ni moja ya sehemu za huduma za kijamii zinazosambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III)

Na Teresia Mhagama, Geita

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga ameeleza kuwa wakandarasi wa umeme vijijini wanaosuasua katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III) hawatapewa kazi katika miradi inayofuata.

Aliyasema hayo wilayani Mbogwe, Mkoa wa Geita mara baada ya  ya Bodi ya REA ikiongozwa na Mwenyekiti wake  Wakili Julius Kalolo kufanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini wilayani Bukombe na Mbogwe.

Wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), watendaji kutoka kampuni ya Whitecity Guangdong JV na TANESCO na REA wakiangalia jinsi kazi ya kuvuta nyaya inavyofanyika katika Kijiji cha Mlange wilayani Mbogwe Mkoa wa Geita. Aliyenyoosha mkono ni Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili Julius Kalolo

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo (kulia) akizungumza na watendaji kutoka kampuni ya Whitecity Guangdong JV na TANESCO wakati alipofanya ziara ya kukagua kazi ya kusambaza umeme kwenye Kijiji cha Mwamakiliga wilayani Nyang’hwale.

” Tuko katika ziara hizi si kutoa maelekezo tu bali pia tunafanya tathmini za wakandarasi kwani tutakuwa na kanzidata itakayoonesha wakandarasi wanaotekeleza miradi kwa wakati na viwango vinavyotakiwa na wale wanaosumbua katika utekelezaji wa mradi unaoendelea.” Alisema Mhandisi Maganga.

Aliongeza kuwa, kanzidata hiyo itasaidia kuwatambua wakandarasi wote wasiofaa kupewa tena nafasi ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini inayofuata  hivyo aliwataka wakandarasi hao wajipange kufanya kazi vizuri.

Aidha, aliwataka wakandarasi wote kuzingatia agizo la Serikali la kuhakikisha kuwa ifikapo Disemba 31 mwaka huu,  vijiji vyote vilivyo katika mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza vinapelekewa umeme.

Kuhusu mkandarasi anayesambaza umeme mkoani Geita, kampuni ya Whitecity Guangdong JV, alimuagiza kuwa ifikapo tarehe 31 Disemba awe amepeleka umeme kwenye vijiji alivyopangiwa na kuwasilisha mpango kazi utakaoonesha pia kazi alizopanga kufanya katika kila Wiki.

Bodi ya REA kwa upande wake, ilimuagiza mkandarasi huyo kutekeleza ratiba za upelekaji umeme katika maeneo yote ambayo Bodi hiyo imetembelea mkoani Simiyu na Geita na kumweleza kuwa haitaacha kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo ili wananchi wapate nishati ya umeme.

Aidha, Bodi hiyo ilimuagiza mkandarasi kuhamasisha matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili kuwaondolea wananchi gharama kufanya wiring ndani ya nyumba na kwamba kipaumbele kiwe ni wajane, wazee na walemavu.

Pia Bodi hiyo iliwaasa viongozi wa vijiji katika maeneo mbalimbali nchini ambapo miradi ya umeme vijijini inaendelea kutekelezwa, kuwahamasisha wananchi ili waunganishiwe na huduma ya umeme hivyo miradi hiyo kuwa na tija.

Bodi hiyo pia ilikagua kazi ya usambazaji umeme wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ambapo mkandarasi alieleza kuwa ndani ya Wiki hii atawasha umeme katika Vijiji Saba.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama