Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kahawa Yawakomboa Wananchi wa Tarime Kiuchumi

Sehemu ya miche ya kahawa ikiwa tayari kwa matumizi ya wakulima wa zao hilo wilayani Tarime, mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza zao hilo hapa nchini.

Na Jonas Kamaleki –  Tarime

Kahawa  ni moja ya mazao ya kimkakati zao ambalo limebadili maisha ya wakazi wa Tarime, Mkoa wa Mara kwa kuwaongezea kipato hivyo kuwaletea maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tarime, Apoo Castro Tindwa akizungumza na maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) katika mahojiano maalum amesema juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kufufua zao la kahawa zimewanufaisha wananchi wa Tarime.

“Zao la kahawa limeibuka upya kupitia Serikali ya Awamu ya Tano na kahawa ya Tarime imeonekana kuwa kahawa bora Afrika, jambo ambalo sisi wakazi wa maeneo haya tunajivunia sana”, alisema Tindwa.

Juhudi za kukuza kilimo hasa cha kahawa Tarime ni pamoja na kuandaa wataalam wakubwa na wadogo, kutenga fedha zaidi ya  Shilingi milioni 55 kwa ajili ya kilimo, kutafuta masoko na kujenga kiwanda cha kubangua kahawa.

Mkulima wa Kijiji cha Bwitirio wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, Bw. Boniface Gamo akionesha namna ya kuandaa miche ya kahawa kwa njia ya vikonyo ili kupata miche bora ya zao hilo.

Wilaya ya Tarime imejiwekea lengo la kuzalisha kahawa hadi kufikia tani 5000 kwa mwaka.

Naye mkulima mkufunzi wa kahawa, Petro Mwita Burungo anayefahamika kwa jina la Nyeusi amesema kuwa kahawa inayolimwa kisasa imemuongezea kipato ambacho kimemuwezesha kusomesha watoto shule, kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi na kupata fedha ya kuweka akiba benki.

Kwa mujibu wa Bw. Mwita ukulima wa kisasa kwa mche mmoja anapata kilo 5 za kahawa ambapo zamani kwa kilimo cha mazoea alikuwa akipata kilo 2 tu za kahawa kwa mche, hivyo maisha yake yamebadilika na maendeleo ni dhahiri.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufufua vyama vya ushirika, AMCOS ambavyo vinanunua kahawa na kutulipa kwa wakati”, anasema Mwita.

Mwita ameendelea kusema kuwa Serikali imemuinua mkulima wa chini na kumpandisha juu kuliko ilivyokuwa kwa vipindi vilivyopita ambapo baadhi ya wananchi walianza kung’oa mibuni na kupanda mazao mengine kwani zao hilo lilionekana kukuso tija.

Mkulima huyu anazalisha mbegu za kisasa za kahawa kwa njia ya vikonyo ambavyo vikishapandwa vinatoa mazo mengi na hukomaa kwa muda mfupi ikilinganishwa na mbegu za kizamani.

Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Nyarero, Wilaya ya Tarime, Joyce Mwita amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imewajali sana wakulima wadogo na kuwainua kwa kuwaletea wataalaam wa kilimo ambao wamewapatia mafunzo ya kilimo bora cha kahawa.

“Kwa kweli namshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kupitia wataalaam wake kufufua zao la kahawa, kwa sasa hata tunapozalisha miche tunapata wateja na tunapouuza kahawa tunapata fedha yetu pasipo usumbufu ikilinganishwa na zamani tulivyokuwa tukiumizwa na walanguzi”, anaongeza Joyce.

Eneo la uzalishaji wa miche ya zao la Kahawa kwa njia ya kikonyo kama ilivyokutwa katika Kijiji cha Bwitirio wilayani Tarime , mkoani Mara.
(Picha zote na MAELEZO)

Mkulima mwingine wa kahawa aliyenufaika na zao hilo ni Bw. Boniface Gamo ambaye licha ya kulima anazalisha miche ya kahawa. Anasema kuwa zao hilo limemuongezea kipato kwa kiwango kikubwa na hivyo kumuweza kusomesha watoto na kufanya maendeleo mengine.

“Tunazalisha miche ambayo tunaiuza kwa wakulima na kujipatia fedha nyingi, kwa sasa tumezalisha zaidi ya miche 350,000 na kuisambaza kwa wananchi, hakika Serikali ya Rais Magufuli imetujali sisi wakulima”, ameongezea Gamo.

Zao la kahawa ni kati ya mazao yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni kwa maana soko lake liko ndani na nje ya nchi.

Serikali ya Awamu ya Tano imefufua zao hilo kwa kuanzisha taasisi za utafiti wa kilimo kwa ajili ya kulipa nguvu zao la kahawa.

Mfano Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TACRI) – Maruku inafanya utafiti wa kahawa na kuzalisha mbegu bora, inaotoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbegu bora, kilimo cha kutumia mbolea na kupambana na magonjwa ya zao la kahawa.

Wakulima wanopata mafunzo ya utafiti wa kahawa na kuzingatia kanuni bora za kilimo, maisha yao kiuchumi yamebadilika na wanapongeza juhudi za makusudi za Serikali za kufufua na kutilia mkazo zao hilo muhimu katika uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Muonekano wa zao la kahawa baada ya hatua za kufufua zao hilo hapa nchini kama ilivyokutwa kwa mmoja wa wakulima wa Wilaya ya Tarime, Bw. Boniface Gamo ambapo Wilaya hiyo ni moja ya maeneo yaliyonufaika na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kufufua uzalishaji wa mazao ya biashara hapa nchini ambapo miche zaidi ya 350,000/ imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima.

Katika kuongeza thamani ya mazao na kuendeleza mapinduzi ya kilimo nchini, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeainisha mazao manne ya kimkakati kama vipaumbele kuanzia mwaka 2020.

Kahawa ni mojawapo ya mazao hayo yaliyowekewa nguvu baada ya kufanyiwa utafiti wa namna ya kuyaongezea thamani. TADB kwa miaka minne imevifikia vyama vya msingi 99 na mikoa 22 kwa kuvipatia mikopo.

Hapa Tanzania kahawa inalimwa kwa wingi katika mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Mara na Ruvuma. Zao hili ni la kibiashara katika mikoa tajwa na maeneo mengine ya nchi ambalo linawanufaisha wananchi kiuchumi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni, hivyo halina budi kutiliwa mkazo.

Kitalu cha kuzalisha miche ya zao la kahawa wilayani Tarime, mkoani Mara ikiwa ni moja ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kufufua uzalishaji wa mazao ya biashara hapa nchini, hatua hiyo inalenga kufikia uzalishaji wa tani 5000 katika Wilaya hiyo.

Kilimo cha kahawa kinachofanyika Tarime na maeneo mengine hapa nchini ni katika kutekeleza Ilani ya Chama Tawala ambayo ilijikita katika kugundua na kutathmini mbegu bora za mazao mbalimbali zenye sifa ya kutoa mavuno mengi na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali kwa kushirikiana na taasisi za umma na binafsi ili kutosheleza mahitaji ya uzalishaji wa mbegu bora nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *