Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Jumuiya za Watumia Maji Zaaswa Kufanya Kazi kwa Uadilifu

Mwakilishi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhaidrolojia Mkuu, Bernad Chikarabani akizungumza na washiriki katika warsha ya Jumuiya ya Watumia Maji.

Jumuiya za Watumia Maji nchini zimeaswa kufanya kazi kwa uadilifu ili kuweza kulinda na kuhifadhi rasilimali za maji kwa ajili ya manufaa ya taifa katika warsha ya siku mbili iliyoshirikisha Jumuiya za Watumia Maji zinazotoka kwenye mabonde matano ya Pangani, Wami-Ruvu, Rukwa, Ruvuma na Rufiji iliyoandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo IWaSP-GIZ, UNDP, WWF, IUCN, 2030 WRG, SNV, Shahidi wa Maji, Waridi na mashirika mengine.

Warsha hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Salinero, mkoani Kilimanjaro ilishirikisha viongozi wa jumuiya hizo na maafisa Maendeleo wa Jamii, ambao kimsingi ndio wenye jukumu kubwa la kuhakikisha ufanisi katika usimamizi wa rasilimali maji kwenye ngazi ya jamii, ililenga kufikia makubaliano ya pamoja kwenye masuala muhimu yatakayowezesha kupata ufumbuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali zinazozikabili jumuiya za watumia maji, na kutoa fursa kwa wadau kujadiliana na kupeana uzoefu kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo katika maeneo ya utendaji kazi ya jumuiya hizo.

Akizungumza katika kuhitimisha warsha hiyo mwakilishi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhaidrolojia Mkuu, Bernad Chikarabani amesema kuwa wizara inawashukuru wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa katika kutunza na kuhifadhi rasilimali za maji nchini kwani mafanikio ya jambo hilo yanahitaji ushirikiano na wadau wote na si la wizara pekee.

 Mmoja wa wawezeshaji akitoa mada kwa washiriki katika warsha ya Jumuiya ya Watumia Maji.

Washiriki wa warsha ya Jumuiya ya Watumia Maji wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Vilevile, aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutengeneza mwongozo utakaosaidia jumuiya kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, lakini pia utaisaidia wizara kupata maoni kutoka kwa wahusika kwenye ngazi ya jamii na kuyaingiza katika sera na miongozo mbalimbali katika usimamizi wa rasilimali za maji na jinsi ya kuimarisha jumuiya hizo.

Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii toka Bonde la Pangani, Patrice Otieno amesema warsha hiyo imelenga kubadilishana uzoefu kwa lengo la kutatua changamoto zinazozikabili jumuiya hizo ambazo zimetofautiana kulingana na maeneo husika. Huku akisisitiza nia ya Serikali ni kuona jumuiya hizo zikiimarika na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili  rasilimali za maji zitunzwe na kunufaisha taifa kwa miaka mingi ijayo.

Baadhi ya matokeo ya msingi yatayotokana na warsha hiyo ni pamoja na uandaaji wa mpango kazi wa utekelezaji kitaifa iliyoshirikisha wadau wa maendeleo na pia mipango kazi katika ngazi za Jumuiya za Watumia Maji ambayo itatoa fursa katika kuandaa miongozo ya uundwaji na utendaji kazi wa Jumuiya za Watumia Maji.

Uundwaaji wa Jumuiya za Watumia Maji ni matokeo ya ushirikiano baina ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali ya usimamizi wa rasilimali za maji. Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na kuzipatia jumuiya hizo mafunzo mbalimbali na vitendea kazi pamoja na kuandaa warsha na majukwaa ya kubadilishana uzoefu.

 

122 thoughts on “Jumuiya za Watumia Maji Zaaswa Kufanya Kazi kwa Uadilifu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *