Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

JPM: Kipaumbele ni Kuhuisha Teknolojia ya Viwanda nchi za SADC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli akihutubia katika ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya Viwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, akiandika anayoyasikia katika hotuba za utangulizi kabla ya kufungua Maonesho ya Wiki ya Viwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), leo , kutoka kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Ally na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Bara, Innocent Bashungwa, kulia mwisho kwa Rais ni Mwenyekiti wa Taasisi binafsi (TPSF), Salum Shamte, kulia kwa Rais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Paramagamba Kabudi.

Na.Paschal Dotto-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli amefungua maonesho ya wiki ya viwanda kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).

Akizungumza katika hafla hiyo ya Wiki ya Viwanda ya SADC jana, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa ili kufikia uchumi wa kati viwanda ni kichochea muhimu katika sekta nyingi kwani uwepo wa viwanda utasababisha uhakika wa uzalishaji na uchakataji wa bidhaa na kufanyabiashara kwa nchi wananchama.

Rais Magufuli amezitaka nchi wanachama wa SADC kuweka kipaumbele kwenye kuhuisha teknolojia katika viwanda vilivyoko ndani ya jumuiya ya Maendelea kusini mwa afrika (SADC) pamoja na kushughulikia kwa haraka zaidi vikwazo vinavyochelewesha ukuaji wa viwanda.

“Viwanda ni Sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yeyote, kuondoa umasikini, kuongeza ajira na Sekta hii imeziletea Maendeleo makubwa nchi zilizoendelea, kwa hiyo mkutano huu ni dhahiri kuwa sasa nchi za SADC zimeanza kuchukua hatua madhubuti za kukuza sekta hii na ikiwa mkakati huu utatekelezwa utasaidia kukuza uchumi wa nchi zetu”, Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli ( wa kwanza kulia waliokaa) akifuatilia maelezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara wa
Innocent Bashungwa, katika ufunguzi wa Wiki ya Viwanda kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) leo, wengine ni Katibu Mtendaji SADC, Dkt.Stagomena Tax, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Paramagamba Kabudi na Mwenyekiti TPSF, Salumu Shamte.

Washiriki wa Maonesho ya Viwanda kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), wakifuatilia hutoba ya Rais Magufuli( hayupo Pichani), katika ufunguzi wa Maonesho hayo ya wiki, yanayofanyika nchini Tanzania kambayo pia yako Karimjee na Gymkana.

Akielezea suala la teknolojia Rais Magufuli amesema kuwa ukuzaji wa teknolojia na ubunifu kwenye sekta ya viwanda ni silaha muhimu kwa nchi za SADC kuendelea na kutegemeana kwani utazalisha ajira, biashara kubwa, na kuepuka kuuza malighafi kwa wingi nje ya Afrika kama ilivyosasa.

Vilevile, mchango wa sekta ya viwanda kwa nchi za SADC bado ni mdogo kwani Sekta hiyo inachangia wastani wa asilimia 10 ya pato la taifa na katika Jumuiya ya SADC sekta hiyo muhimu inachangia asilimia 11 tu. Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alizitaka nchi wanachama wa SADC kujikita zaidi katika kukuza ubunifu na teknolojia rahisi kwenye sekta ya viwanda kwa kuwaendeleza vijana na kuimarisha viwanda vidogo vidogo vilivyoko kwenye jumuiya, kwa hiyo wiki ya viwanda ni fursa muhimu kwa nchi zote wananchama.

Bendi ya Jeshi la Polisi (Brass Band), wakiwa kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya Wiwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), yanayofanyika nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli akiwa kwenye picha ya pamoja na Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), Baada ya ufunguzi wa Maonesho hayo katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere.

“Wiki ya Viwanda ya SADC ni fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau kuhusu utekelezaji wa mikakati ya miaka 49 ya uendelezaji wa viwanda katika jumuiya yetu, bado tunasafari ndefu kuhakikisha sekta ya viwanda inazidi kukua na kuleta mageuzi ya kiuchumi katika nchi zetu”, Amesema Rais Magufuli

Rais Magufuli amesisistiza kwa kusema kuwa katika kuimarisha mashirikiano ndani ya Jumuiya ya Maendeleo (SADC) ni lazima kuimarisha sekta ya uwekezaji kwani nchi hizo zina fursa nyingi kwenye uwekezaji ikiwemo viwanda vya madini, kilimo, uvuvi na ufugaji kwa hiyo wananchi kutoka SADC wanatakiwa kuchangamkia fursa kwenye soko la takribani watu milioni 344.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Innocent Bashungwa amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati wenye viwanda ni mkubwa na matokea yake yanaonekana sasa. Hivyo, maonesho haya ni moja ya njia muhimu ya kuimarisha sekta ya viwanda nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Taasisi kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), Baada ya ufunguzi wa maonesho ya wiki ya viwanda ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) yanayofanyika nchini Tanzania.

Katibu Mtendaji kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), Stagomena Tax, akitoa hutuba katika ufunguzi wa maonesho ya wiki ya viwanda ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) yanayofanyika nchini Tanzania.

“Maonesho haya ya wiki ya viwanda yanawawezesha wanachama wa SADC kuona namna nchi wenyeji inavyotekeleza uwekezaji kwenye sekta ya Viwanda. Aidha, tunaamini wazalishaji, wafanyabiashara, na wananchi kwa ujumla watachangamkia fursa mbalimbali zitazotokana na mkutano huu wa SADC.”, Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa alisema kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye biashara ndani ya SADC kwani takwimu zinaonyesha kuwa mauzo ya Tanzania kwenda SADC mwaka 2018 yalikuwa dola za kimarekani milioni 999 ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 875 mwaka 2017 ikiwa na ongezeko la asilimia 12.16.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Ally amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli wa kuendeleza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl . Julius Nyerere kwa kujenga bwawa Kubwa la kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni hatua kubwa kwa maendeleo ya sekta ya viwanda.

Balizo Amina alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi yote inayofanywa na Serikali suala muhimu ni uwepo wa amani kwa Tanzania na ndiyo maana ikachaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho ya SADC yakifuatiwa na Mkutano mkuu wa viongozi wakuu wa nchi za wanachama wa SADC.

“Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani na kwa tukio hili itaendelea kudumisha amani na utilivu kwani mpaka sasa maonesho na mkutano mkuu unaofanyika hapa unaonesha kuwa tanzania ni nchi ya amani”, Waziri wa Viwanda Zanzibar, Amesema Balozi Amina Ally.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt.Stagomena Tax, amesema kuwa juhudi za Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi mkubwa wa kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni moja ya njia madhubuti katika kuimarisha na kukuza sekta ya viwanda kwa Jumuiya ya SADC.

12 thoughts on “JPM: Kipaumbele ni Kuhuisha Teknolojia ya Viwanda nchi za SADC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *