Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Jeshi la Magereza Kujitegemea kwa Kutumia Rasilimali Zake

Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Magereza, Uwesu Ngarama akitoa taarifa fupi katika Kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma.

Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee, amesema kuwa Jeshi hilo limeanza kuyafanyia kazi maagizo mbalimbali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuhakikisha linatekeleza mikakati ya kuanza kujitegemea ikiwemo kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Amesema hatua hiyo inaanza mara moja kwani Jeshi hilo lina uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zilizopo ndani ya Jeshi ambazo zinaweza kuliwezesha kujitegemea bila kutegemea bajeti ya Serikali.

Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema hayo leo jijini Dodoma katika kikao kazi cha maafisa waandamizi wa Jeshi hilo kutoka mikoa yote Tanzania Bara ambacho kililenga kupeana mikakati ya namna ya kufanikisha mpango wa kujitegemea.

Baadhi ya Wakuu wa Magereza Mikoa pamoja na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee(hayupo pichani)katika Kikao kazi kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma.

“Magereza kujitegemea inawezekana kwani tunazo rasilimali nyingi ikiwemo mashamba ya kilimo, mifugo, wataalam wakutosha na nguvu kazi ya wafungwa ambapo tukizisimamia vizuri na kuachana na ubinafsi tutaliwezesha Jeshi letu la Magereza kujitegemea”, alisema Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Suleiman Mzee ametoa maelekezo kwa wakuu wote wa Magereza Mikoa yote Tanzania Bara kuhakikisha kuwa wanaanza kujitegemea kwa asilimia mia moja kwa chakula cha wafungwa na huduma nyinginezo kwani kila mkoa unazo fursa nyingi za kuliwezesha Jeshi hilo kujitegemea.

“Kuanzia mwezi ujao, Machi 1, 2020 kila Mkuu wa Magereza Mkoa(RPO) lazima ahakikishe kuwa anajitegemea katika mkoa wake na lazima mkubali kufanya mabadiliko haya bila visingizio. Atakayeshindwa kujitegemea nitamwajibisha mara moja”, amesisitiza Jenerali Suleiman Mzee.

Wajumbe wa Sekretarieti wakifuatilia kikao kazi hicho kilichoongozwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza leo Februari 19, 2020 katika Ukumbi Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.

Aidha, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee ameongeza kuwa tayari ameanza maandalizi ya ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza pamoja na nyumba za watumishi wa Jeshi hilo jijini Dodoma kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo Jeshini.

Kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Magereza ndicho kikao cha juu cha uongozi ambacho huwakutanisha Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu, Wakuu wa Magereza wa Mikoa, Wakuu wa Vyuo, Mkuu wa Kikosi maalum na Mkuu wa Sekondari Bwawani. Kikao hicho hulenga kuwekeana mikakati mbalimbali ya namna ya kuboresha utendaji kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao waliokabidhiwa.

14 thoughts on “Jeshi la Magereza Kujitegemea kwa Kutumia Rasilimali Zake

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama