Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuimarisha operesheni katika mipaka, bandari, na viwanja vya ndege, na kutoa elimu kwa jamii hususan vijana ili kupunguza matumizi ya dawa za kulevya zimeendelea kutishia usalama wa nguvu kazi nchini.
Rais Mwinyi aliyasema hayo leo, Aprili 2, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, uliofantika katika Uwanja wa mpira wa miguu Chake Chake, Kusini Pemba, Zanzibar.
Amesema mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni miongoni mwa ujumbe muhimu unaoambatana na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026.
Aidha Rais Mwinyi, ameeleza kuwa kuanzia Desemba 2025, waraibu 18,970 walipatiwa matibabu katika vituo 16, huku zaidi ya waraibu 19,000 wakihudumiwa katika vyumba 77 vya upataji nafuu. Aidha, waraibu 728 walipatiwa huduma katika kituo cha tiba na marekebisho ya tabia cha kidini Zanzibar.
Rais Mwinyi alisisitiza kuwa juhudi za kudhibiti matumizi na biashara ya dawa za kulevya haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi, hivyo ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo, ikiwemo kufichua kilimo, biashara na matumizi ya dawa hizo kupitia namba ya bure 119.
"Kupitia hadhara hii, natoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kufichua vitendo hivi ili kulinda taifa letu,” amesisitiza Rais Mwinyi.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amesema ujumbe wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI unaendelea kuwa ajenda ya kudumu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru tangu ulipotangazwa mwaka 2021.
Amesema janga hilo linaathiri zaidi vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, ambao wanachangia asilimia 33 ya maambukizi mapya, huku wasichana wakichangia asilimia 75 ya maambukizi hayo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na VVU na UKIMWI kwa kuongeza upatikanaji wa dawa za ARV bila malipo na kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema kuwa vijana sita wameandaliwa kikamilifu kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mikoa 31 na halmashauri 195 kote nchini.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, Wazo Mang’onda, alipokea rasmi mwenge huo uliowashwa kutoka kwa Rais Mwinyi, na kuahidi kuongoza mbio hizo kwa siku 195 mfululizo, akisimamia utekelezaji wa malengo ya Mwenge wa Uhuru ikiwemo kuhimiza amani, mshikamano, mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na ulinzi wa rasilimali za taifa.