Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua jumla ya minara 758 ya mawasiliano pamoja na kukamilika kwa maunganisho ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, akisema hatua hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidigital na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Uzinduzi huo uliofanyika Aprili 10, 2026, Jijini Dodoma unaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, hususan wale waishio vijijini, visiwani na maeneo ya mipakani ambayo kwa muda mrefu yamekuwa nyuma katika huduma hiyo muhimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kukamilika kwa minara hiyo kutaongeza upatikanaji wa mawasiliano kwa maelfu ya wananchi na hivyo kufungua fursa mpya za kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.
“Kukamilika kwa minara 758 tunayozindua leo kunaongeza upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi zaidi ya 8,000, hususan katika maeneo ya vijijini na mipakani,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza “ Mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kisasa, akibainisha kuwa kupitia huduma bora za mawasiliano, wananchi wataweza kushiriki kikamilifu katika biashara za mtandaoni, elimu ya kidigital, pamoja na huduma za kifedha kwa njia ya simu.”
Aidha, Rais Samia ameendelea kusema kuwa uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano ni daraja la kufungua fursa za uwekezaji na ubunifu, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.

Katika hatua nyingine, ameziagiza halmashauri nchini kuacha urasimu usio wa lazima unaochelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya mawasiliano, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa wakati.
Awali, akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi wa sekta ya mawasiliano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 hakuna eneo litakalobaki bila kufikiwa na huduma za mawasiliano nchini.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, sekta hiyo imepata mafanikio makubwa, ambapo matumizi ya laini za simu yameongezeka kutoka milioni 52.8 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 106.8, sawa na ongezeko la asilimia 102.

Aidha, ameeleza kuwa matumizi ya intaneti pia yameongezeka kwa kasi, yakitoka watumiaji milioni 29.7 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 58.8, jambo linaloonyesha ongezeko la takribani asilimia 100.