Wakati Magonjwa mbalimbali ya moyo yakiendelea kuwa tishio kwa watu wengi na kusababisha vifo vingi duniani Tanzania inajivunia kuwa kinara dhidi ya mapambano ya magonjwa ya moyo Afrika.
Mkurugenzi Mtendajiwa wa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge, amesema magonjwa ya moyo yakiendelea kusababisha vifo vingi duniani nchi nyingi za Afrika JKCI imeendelea kuyakabili magonjwa hayo na kuibuka kinara barani Afrika.

Dkt. Kisenge ameyasema hayo leo Aprili 9, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO Mtumba Dodoma ambapo amesema huduma za kibingwa za tiba ya magonjwa ya moyo JKCI zimeimarishwa
"Ukiangalia kwenye takwimu utaweza kuona nchi za Misri, Ghana, Nigeria, Uganda, Zambia na Rwanda ndo zimetengeneza taasisi hizi na ukizilinganisha na JKCI utataweza kuona JKCI inaongoza na ndiyo maana nchi hizi zimekuwa zikiitumia sana JKCI" Amesema Dkt. Kisenge.
Amesema JKCI inaongoza kwa upasuaji wa tundu dogo, ikifanya mara 200 zaidi ya Kenya, mara 500 zaidi ya Uganda, na mara 300 zaidi ya Zambia kwa mwaka.

Aidha ameongeza kuwa JKCI hufanya zaidi ya upasuaji mkubwa wa kufungua kifua kwa wagonjwa 800 kila mwaka, pamoja na taratibu ngumu (complex procedures) kama TAVI ambazo bado hazijaanza hata katika hospitali kubwa za Misri.
Aidha Dkt. Kisenge amesema mafanikio hayo ni matokeo ya maono na uwekezaji wa hali ya juu uliofanywa na Serikali, kiasi cha kuifanya taasisi hiyo kuwa kivutio cha wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanaotafuta tiba ya uhakika.

"Kwa hiyo tuchukuwe nafasi hii kwanza kumpongeza Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye taasisi hii hadi nchi zingine za Afrika kutaka kuhudumiwa na taasisi hii ya JKCI" Amesema Dkt. Kisenge

Amehitimisha kuwa pamoja na kwamba Afrika ina hospitali chache zinazotibu magonjwa ya moyo lakini hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete ndio taasisi pekee ya Serikali inayoongoza kwa matibabu ya moyo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Jangwa la Sahara.