Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Hotuba ya waziri wa maliasili na utalii mheshimiwa Dkt. Hamisi a. Kigwangalla (mb) wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa fedha 2018/2019

 

HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHESHIMIWA

DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA (MB) WAKATI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA

MWAKA WA FEDHA 2018/2019

UTANGULIZI

 1. Mheshimiwa Spika, Ninaomba kutoa hoja kwamba kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

 1. Mheshimiwa Spika, Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena. Aidha, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, Hotuba ya Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Kwa upekee, ninamshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuniteua kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Vilevile, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa maelekezo anayoyatoa ambayo yanatoa dira ya uhifadhi, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi. Pia, ninawashukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kwa miongozo wanayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu kikamilifu.

 1. Mheshimiwa Spika, Ninapenda kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb); na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Bunge kwa weledi mkubwa.

 1. Mheshimiwa Spika, Ninachukua fursa hii pia kuwashukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb); Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota (Mb); na Wajumbe wote wa Kamati kwa kuendelea kutupatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Wizara.

 1. Mheshimiwa Spika, Ninawapongeza Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel (Mbunge wa Jimbo la Siha), Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro (Mbunge wa Songea Mjini), Mheshimiwa Maulid Mtulia (Mbunge wa Jimbo la Kinondoni), Mheshimiwa Justine Joseph Monko (Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini), na Mheshimiwa Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa (Mbunge wa Longido), kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge walioteuliwa kuwa Mawaziri na Naibu Mawaziri. Niruhusu pia kuwashukuru Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb), Naibu Waziri; Meja Jenerali Gaudence S. Milanzi, Katibu Mkuu; na Dkt. Aloyce K. Nzuki, Naibu Katibu Mkuu; kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Vilevile, ninawashukuru Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo, Wakuu wa Mashirika na Taasisi, watumishi na wadau kwa ushirikiano wanaotupatia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake.

 1. Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Nzega Vijijini kwa kuendelea kuniunga mkono kwa dhati katika kutekeleza majukumu yangu kama Mbunge na Waziri wa Maliasili na Utalii. Ninapenda kuwahimiza kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya Jimbo letu na Taifa kwa ujumla. Aidha, nitakuwa mchoyo wa shukran bila kumshukuru kwa dhati mke wangu Dkt. Bayoum Kigwangalla na familia yangu kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekekeleza majukumu yangu.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Bunge lako Tukufu liliondokewa na Mheshimiwa Leonidas T. Gama, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini. Aidha, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kushambuliwa na wanyamapori; ajali za vyombo vya usafiri kama vile mabasi na ndege; maradhi na majanga, kuna Waheshimiwa Wabunge, wananchi, watumishi na watalii waliojeruhiwa, waliopata ulemavu wa kudumu na waliofariki. Hivyo, ninaungana na wenzangu kuwapa pole wote waliopatwa na majanga na kufiwa na ndugu, jamaa na wapendwa wao. Ninamuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema waliojeruhiwa na azipumzishe roho za Marehemu Wapendwa Wetu mahala pema peponi – Amina.

 1. Mheshimiwa Spika, Baada ya utangulizi, ninaomba kuwasilisha Hotuba yangu ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tano. Kwanza: Dira, dhima na majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii; Pili: umuhimu wa  maliasili, malikale na utalii; Tatu: maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii; Nne: utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018; na Tano: Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

DIRA, DHIMA NA MAJUKUMU YA WIZARA

 1. Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni “Maliasili na Malikale Zilizohifadhiwa kwa Manufaa ya Watanzania Wakati Ikiongoza Kuchangia Ukuaji wa Uchumi”. Aidha, Dhima ya Wizara ni Uhifadhi Endelevu wa Maliasili na Malikale na Kuendeleza Utalii kwa Manufaa ya Taifa”.

 1. Mheshimiwa Spika, Ili kufanikisha Dhima hiyo, Wizara imedhamiria kulinda maliasili, malikale na kuendeleza utalii; kujenga uwezo wa kutekeleza majukumu yake; kuhakikisha wananchi na wadau wanashirikishwa; kukusanya maduhuli; na kuhakikisha Sekta ya Utalii inachangia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza Pato la Taifa. Malengo hayo yanatekelezwa kupitia Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati, Programu na Miongozo.

UMUHIMU WA MALIASILI, MALIKALE NA UTALII

Maeneo ya Maliasili na Malikale

 1. Mheshimiwa Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na maeneo ya maliasili na malikale yenye umuhimu mkubwa kimazingira, kiuchumi, na kijamii. Ufafanuzi wa kina kuhusu maeneo ya hifadhi za wanyamapori, misitu, ufugaji nyuki, na malikale; na ustawi wa sekta ya utalii; yameainishwa katika Aya ya 12 hadi 15 katika Kitabu cha Hotuba, Uk. 6 – 7.

Mchango wa Maliasili, Malikale na Utalii katika Mazingira na Uchumi

 1. Mheshimiwa Spika, Huduma za maliasili kwa mazingira zimeainishwa katika Tathmini ya Mazingira ya Millenia (Millennium Ecosystem Assesment). Huduma hizo zinajumuisha: Moja, utoaji wa huduma kwa mazingira (Provisioning Services); Mbili, huduma za kusaidia mazingira (Supporting services); Tatu, huduma za udhibiti wa mazingira (Regulating Services); na Nne, huduma za kitamaduni (Cultural Services).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa maliasili, malikale, mazingira na utalii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda maliasili za nchi, kuongeza jitihada za kupambana na ujangili na upotevu wa mazao ya misitu, kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi, kutumia utalii kujenga uchumi, na kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato.

 1. Mheshimiwa Spika, Huduma za usafiri wa anga na utangazaji ni muhimu katika kuendeleza utalii. Kutokana na umuhimu huo, Mheshimiwa Rais ametoa msukumo wa kuimarishwa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), na ameelekeza kuanzishwa kwa Chaneli maalum ya kutangaza utalii kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1). Juhudi hizo zinaenda sanjari na azma ya kukuza utalii, kuongeza wigo kijiografia, na kutangaza fursa za uwekezaji. Aidha, jitihada nyingine za Serikali zinazoelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja, viwanja vya ndege, na TEHAMA zimeendelea kujenga mazingira wezeshi katika kukuza utalii wa kimataifa na wa ndani. Ninayapongeza mashirika ya ndege, televisheni nyingine na wadau kwa kutambua umuhimu na kushiriki katika kusafirisha wageni, kuwekeza na kutangaza vivutio vya utalii.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika jitihada za kuendeleza uhifadhi wa maliasili na mazingira na manufaa yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais, amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha, kuwaelimisha na kuwashirikisha wananchi. Aidha, Mheshimiwa Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka katika ngazi mbalimbali kutayarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi, mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, na kudhibiti uvunaji holela na ufugaji usio endelevu.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kutatua migogoro kati ya wananchi na hifadhi na kukuza utalli, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo kuhusu umuhimu wa kutambua chimbuko la migogoro ya ardhi na kuitatua kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Aidha, ameendelea kusisitiza kuhusu kuimarisha sekta ya utalii kwa kuwavutia wawekezaji zaidi; kuimarisha miundombinu ya maeneo ya utalii; na kuhamasisha utalii wa ndani ukiwemo utalii wa fukwe, mambo ya kale, na kihistoria katika miji ya kihistoria ya Bagamoyo, Kilwa na Mikindani.

 1. Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia maagizo ya Viongozi Wakuu wa Nchi, Wizara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya ili kuhakikisha maliasili na malikale zinahifadhiwa na kulindwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Ninapenda kutoa rai kwa wananchi tuendelee kujenga mtazamo chanya na kushirikiana katika kuhifadhi maliasili, malikale na kuendeleza utalii kwa ajili ya uhai na maendeleo ya Taifa letu na Dunia kwa ujumla.

 

MAONI NA USHAURI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII

 1. Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, Kamati ilichambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kutoa maoni na ushauri uliolenga kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa ushauri wa Kamati umezingatiwa katika Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ninayowasilisha leo hapa Bungeni.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

 1. Mheshimiwa Spika, Ninaomba kutoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Sehemu hii inafafanua vipengele vya ukusanyaji maduhuli, na matumizi ya kawaida na maendeleo katika kutekeleza kazi zilizopangwa.

Ukusanyaji Maduhuli

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara na Taasisi zilizo chini yake iliidhinishiwa kukusanya maduhuli ya Shilingi Bilioni 63.6. Hadi kufikia Machi 2018, jumla ya Shilingi Bilioni 32.0 sawa na asilimia 50 ya makadirio zilikusanywa. Kiasi kilichokusanywa ni ongezeko la asilimia 128 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 14 zilizokuwa zimekusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka 2016/2017. Aidha, Mashirika ya TANAPA, NCAA, TAWA na TFS yaliwekewa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 456.1. Hadi Machi 2018, Mashirika hayo yamekusanya Shilingi Bilioni 430 sawa na asilimia 94 ya makadirio. Baadhi ya sababu za kuongezeka kwa makusanyo hayo ni kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji maduhuli ya Serikali, kutangaza vivutio vya utalii, na kuboresha miundombinu.

Matumizi ya Kawaida na Maendeleo

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara iliidhinishiwa kutumia Shilingi Bilioni 0 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa matumizi ya kawaida ni Shilingi Bilioni 97.2 na Shilingi Bilioni 51.8 zilitengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Machi 2018, jumla ya Shilingi Bilioni 72.9 sawa na asilimia  49 ya bajeti iliyoidhinishwa zilipokelewa. Kati ya fedha zilizopokelewa, fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi Bilioni 45.0 na fedha za maendeleo ni Shilingi Bilioni 27.9.

Mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukamilisha mapitio ya Sera za Taifa za Misitu (1998) na Utalii (1999). Hadi Machi, 2018 Wizara imekamilisha rasimu za Sera hizo. Aidha, maandalizi ya kupitia Sheria ya Misitu yanaendelea sambamba na kutunga Sheria mpya ya Malikale ili ziendana na mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii yanayotokea ndani na nje ya nchi. Vilevile, Wizara inatunga Sheria mpya za Uhifadhi wa Wanyamapori na zinazosimamia TANAPA, NCAA na TAWA ili ziendane na Sheria mama za uhifadhi.

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa Kanuni mpya za Usimamizi wa Shoroba na Maeneo ya Wazi yenye wanyamapori na kukamilisha mapitio ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii. Aidha, Kanuni za Biashara ya Nyara na Wanyamapori Hai, WMA, na Mkataba wa CITES zinapitiwa. Mapitio hayo yanalenga kuhakikisha kuwa biashara hizo zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu; na kudhibiti biashara ya wanyamapori na mimea iliyo hatarini kutoweka.

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeboresha Kanuni ya Ada na Tozo za Utalii kwa kushusha kiwango cha malipo kutoka Shilingi za kitanzania sawa na Dola za Marekani 2,000 kwa gari tano hadi kufika Shilingi sawa na Dola za Marekani 500 kwa gari moja hadi tatu. Aidha, Wizara imekamilisha rasimu ya Kanuni za kusimamia watoa huduma katika sekta ya utalii na ukarimu ili kuboresha huduma zitolewazo kwa watalii.

Majukumu ya Wizara na Taasisi zake

Sekta Ndogo ya Wanyamapori

 1. Mheshimiwa Spika, Jukumu kuu la Sekta Ndogo ya Wanyamapori ni kuhifadhi wanyamapori ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.  Jukumu hilo linatekelezwa na Idara ya Wanyamapori, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks – TANAPA); Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority – NCAA); Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tanzania Wildlife Management Authority – TAWA); Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tanzania Wildlife Research Institute – TAWIRI); Mfuko wa Kuhifadhi  Wanyamapori (Tanzania Wildlife Protection Fund – TWPF); Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori – Mweka, Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi na Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga. Katika kutekeleza jukumu hilo; wananchi, sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na wadau wengine wameshirikishwa kikamilifu.

Utekelezaji wa Masuala Mahsusi ya Sekta Ndogo ya Wanyamapori

 

Mkakati wa Usimamizi wa Pori Tengefu Loliondo

 1. Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuunda chombo maalum kitakachosimamia Eneo la Pori Tengefu Loliondo kwa malengo mapana ya uhifadhi, maendeleo ya wananchi, wawekezaji wa shughuli za utalii na maendeleo ya sekta nyingine muhimu za kiuchumi bila migongano. Kwa kuzingatia agizo hilo, Wizara imeandaa rasimu ya Mkakati wa Usimamizi wa Pori Tengefu Loliondo unaoonesha muundo wa chombo cha kusimamia eneo husika na majukumu yake. Rasimu hiyo itawasilishwa kwa Mawaziri wanaohusika ili waidhinishe na kuiwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Usimamizi wa Biashara ya Wanyamapori Hai

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali ilisitisha biashara ya wanyamapori hai Mei, 2016. Kwa kuzingatia ahadi ya Wizara katika hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara imeendelea kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuandaa mpango madhubuti wa kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa biashara ya wanyamapori hai. Mpango huo unahusisha uwekaji wa mfumo wa ki-elektroniki wa utoaji wa vibali, ukusanyaji wa maduhuli na ufuatiliaji wa biashara ya wanyamapori hai. Aidha, Wizara inarekebisha Kanuni husika kwa lengo la kuweka wazi utoaji huduma na kuanzisha utaratibu wa kusimamia kwa karibu kazi ya ukamataji wa wanyamapori hai.

 1. Mheshimiwa Spika, Sambamba na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuimarisha mifumo ya usimamizi, Serikali imeridhia kuwarudishia wafanyabiashara walioathirika kutokana na usitishwaji huo fedha ambazo walizitumia kufanya malipo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali. Kiasi cha Shilingi milioni 173.3 zinatarajiwa kulipwa baada ya uhakiki kukamilika. Hatua inayofuata ni kufanya utafiti utakaoonesha hali halisi ya wanyamapori na kushauri kuhusu biashara ya wanyamapori hai.

 

Uwindaji wa Kitalii

 

 1. Mheshimiwa Spika, Biashara ya uwindaji wa Kitalii inasimamiwa na TAWA ambayo inagawa vitalu na kutoa leseni kwa kampuni ambazo zimesajiliwa. Vitalu vya uwindaji vipo 159 ambavyo kati yake vitalu 78 vimekodishwa kwa kampuni na vitalu 81 vipo wazi. Katika msimu wa uwindaji (Julai hadi Desemba 2017), wawindaji wa kitalii 473 na wasindikizaji 291 walishiriki katika uwindaji. Aidha, kumekuwepo na changamoto ya vitalu kurejeshwa kwa sababu mbalimbali. Kufuatia hali hiyo, Wizara imeanza kufanya yafuatayo: i) kuimarisha ulinzi katika Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ili kurejesha hadhi yake; ii) kuangalia uwezekano wa kuongeza muda wa kumiliki vitalu ili kuvutia uwekezaji wa muda mrefu; iii) kuruhusu shughuli za utalii wa picha kufanyika baada ya msimu wa uwindaji kwisha ili kuongeza muda mrefu wa kufanya biashara; na iv) kupitia upya viwango vya tozo na ada za leseni mbalimbali ili kuvutia wageni zaidi wa uwindaji wa kitalii.

 1. Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa tasnia ya uwindaji wa kitalii katika kukuza uchumi wa nchi, Wizara kupitia TAWA imeendelea kurekebisha muundo wa uwekezaji na utaratibu wa kugawa vitalu vya uwindaji. Hatua hiyo inahitaji marekebisho ya Sheria ya Wanyamapori ambayo imeanza kufanyiwa kazi.

Kuzuia na Kupambana na Ujangili

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu operesheni za kuzuia na kupambana na ujangili kupitia Kikosikazi cha Kuzuia Ujangili (National Anti-poaching Task Force). Kikosikazi hicho kinatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na TANAPA, NCAA, TAWA na TFS. Kazi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia taarifa za kiintelijensia na TEHAMA ikiwemo ndege zisizokuwa na rubani (drones) na mbwa wa kunusa.

Udhibiti wa Mifugo kwenye Maeneo ya Hifadhi

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia Sheria ili kudhibiti uingizaji wa mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu kinyume cha sheria. Kutokana na hatua hiyo, uoto wa asili umeanza kurejea kwenye maeneo mbalimbali na ustawi wa wanyamapori umeendelea kuimarika. Mafanikio hayo yameanza kuonekana katika Mapori ya Akiba ya Burigi, Biharamulo na Kimisi. Aidha, Wizara imewasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ili kuoanisha na kurahisisha utoaji wa adhabu kwa makosa yatokanayo na kuingiza na kuchunga mifugo ndani ya hifadhi.

Ulinzi wa Wananchi na Mali zao Dhidi ya Wanyamapori Wakali na

Waharibifu

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kulinda maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu. Aidha, zoezi la kuhakiki athari zitokanazo na uharibifu wa wanyamapori huchukua muda mrefu. Vilevile, uhaba wa fedha za kuhakiki na kulipa waathirika umekuwa ni changamoto. Ili kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Wizara kupitia TANAPA, NCAA, na TAWA imeendesha doria katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwalinda wananchi na mali zao. Pia, Wizara imeanza kutekeleza mpango wa kutumia teknolojia na mbinu mbalimbali. Mathalan, ndege zisizo na rubani (Unmanned Aerial Vehicle) na kuendelea kuhamasisha matumizi ya pilipili na ufugaji nyuki kuzuia wanyamapori hususan tembo kuingia maeneo ya wananchi. Aidha, Wizara inaandaa mabadiliko ya Sheria na taratibu zinazolenga kuongeza ufanisi katika uhakiki na upatikanaji wa fedha za kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Sanjari na hatua hizo, Wizara imeanza maandalizi ya ujenzi wa vituo vya askari (ranger posts), kwenye maeneo yenye matukio ya mara kwa mara ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile Wilaya za Bunda, Tarime, Itilima, na Serengeti. Aidha, Wizara imeendelea kuchangia katika kusogeza huduma za kijamii (maji, afya, na elimu) karibu na wananchi. Hatua hizo zinachukuliwa ili kuwanusuru wananchi kutokana na madhara ya wanyamapori wakali ikiwemo mamba wakati wakitafuta maji. Majukumu hayo yanatekelezwa na Wizara kupitia Mashirika ya TANAPA, NCAA, TAWA, na kwa ushirikiano na Mamlaka nyingine za Serikali.

 

Usimamizi wa Pori Tengefu Kilombero

 

 1. Mheshimiwa Spika, Bonde la Kilombero ambalo linajumuisha ardhioevu inayotambuliwa kimataifa (Ramsar site) na Eneo la Pori Tengefu ni eneo la lindimaji linalochangia maji katika Mto Rufiji. Bonde hilo lina utajiri wa kuwepo na aina zaidi ya 400 za ndege na mnyamapori aina ya Sheshe (Puku) ambaye ni adimu. Aidha, Bonde hilo ni chanzo muhimu cha maji kwa shughuli za kibinadamu na maendeleo ikiwemo Mradi wa uzalishaji wa Umeme wa Maji Rufiji (Rufiji Hydropower Project). Pamoja na umuhimu huo, Bonde hilo linakabiliwa na changamoto za uvamizi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu. Kutokana na hali hiyo, Wizara imeunda kamati maalum ili kuishauri Serikali hatua za kutatua changamoto hizo.

 

Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA)

 

 1. Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Wanyamapori (2007) inaelekeza ushirikishaji wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori na kuwanufaisha. Katika kutekeleza azma hiyo, Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) uhifadhi wa wanyamapori nje ya maeneo ya hifadhi kwa kuwahamasisha wananchi kuanzisha maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs). Jumla ya WMAs 22 zimesajiliwa na kupewa haki ya matumizi (user rights) na 16 zipo katika hatua mbalimbali ya uanzishaji. Madhumuni ya kuanzisha WMA ni: i) Kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo ya shoroba na mtawanyiko; ii) Kuhakikisha WMA zinakuwa na nguvu ya kisheria; na iii) Kuwanufaisha wananchi.

 1. Mheshimiwa Spika, Dhana ya WMA imeendelea kupata mafanikio licha ya changamoto zinazojitokeza ambazo ni pamoja na ujangili, uvamizi wa ardhi kwa matumizi mengine na uongozi dhaifu. Kati ya WMA 22 zilizosajiliwa, baadhi ya Jumuiya zinazofanya vizuri ni Mbarang’andu (Namtumbo), Burunge (Babati), Enduiment (Longido), Ikona (Serengeti), Ipole (Sikonge), MAGINGO (Liwale), Makao (Meatu), Ngarambe/Tapika (Rufiji), Uyumbu (Urambo), na RANDILEN (Monduli). Aidha, Jamii zimeendelea kuhamasika katika kushiriki kwenye uanzishaji na usimamizi wa WMA. Vilevile, wananchi wameweza kuhifadhi na kunufaika na WMA zilizoimarishwa kimfumo na kujengewa uwezo wa usimamizi. Kupitia uhifadhi wa wanyamapori, wananchi wameweza kupata huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, ajira za muda mfupi na mrefu pamoja na soko la bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa katika maeneo hayo.

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuzijengea uwezo Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori kwa kutoa mafunzo ya namna ya kuziendesha.Mafunzo hayo yametolewa kwenye WMA za Mpimbwe (Mlele), Makame, Waga (Mufindi, Iringa na Mbarali), JUHIWANGUMWA (Rufiji), Ziwa Natron (Longido), ILUMA (Ulanga na Kilombero) na Kidoma (Mvomero na Kilosa).

Majukumu Mengine Yaliyotekelezwa na Idara, Mashirika, Vyuo na Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori kwa kufanya kazi ambazo ni pamoja na: kuimarisha ulinzi na kudhibiti ujangili kwa kuendesha doria na kulinda maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu. Aidha, maandalizi ya kupandisha hadhi maeneo ya shoroba za Litumbandyosi na Gesimasowa yaliyopo Mkoa wa Ruvuma kuwa Mapori ya Akiba

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na juhudi za kuendeleza utalii, kwa kujenga na kukarabati miundombinu; na kuboresha huduma za malazi na kutangaza utalii. Aidha, jengo la kitega uchumi la NCAA katika Jiji la Arusha limekamilkishwa ili kuwa kituo kimoja cha kutoa huduma za utalii (Tourism One Stop Centre). Vilevile, katika kujenga uwezo wa kitaasisi, nyumba 30 za watumishi zimejengwa kwenye Hifadhi za Taifa 11; na mafunzo ya aina mbalimbali yametolewa kwa watumishi 200 wa TAWA. Aidha, magari 53, pikipiki 15 na boti nne, zimenunuliwa na magari 10 yamepokelewa kutoka kwa wahisani.

 1. Mheshimiwa Spika, Miradi 126 ya utafiti imeratibiwa na TAWIRI ambapo miradi 119 inatekelezwa na watanzania. Aidha, miradi 34 inayohusu utafiti wa mbwa mwitu; na utafiti wa magonjwa ya kimeta, homa ya vipindi na kifua kikuu inatekelezwa. Vilevile, Utafiti umeendelea kufanyika jinsi mfumo ikolojia – Serengeti unavyofanya kazi na manufaa yake kwa jamii, kwenye nyanja za: mahusiano ya nyuki na mimea; na sensa za wanyamapori.

 1. Mheshimiwa Spika, Baadhi ya matokeo ya utafiti yaliyotolewa taarifa yanahusu uwezo wa mfumo ikolojia – Serengeti kuhimili idadi ya mifugo ikiwa ni pamoja na magonjwa. Aidha, utafiti kuhusu mfumo ikolojia – Serengeti umebaini kuwepo idadi kubwa ya mifugo ambayo haiendani na malisho katika eneo la magharibi mwa mfumo wa ikolojia hiyo. Hivyo, inashauriwa kuwa mifugo ipunguzwe katika eneo hilo. Vilevile, kutokana na kuwepo kwa taarifa za vifo vya mifugo 236,437 katika Hifadhi ya Ngorongoro, uchunguzi umefanyika na kubaini kuwa vifo hivyo vimesababishwa na ukame, magonjwa na wingi wa mifugo kuliko uwezo wa eneo. Uchunguzi huo unadhihirisha kuwa kuna madhara makubwa ya mwingiliano kati ya binadamu, wanyamapori na mifugo. Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imechukua hatua ya kutoa chanjo kwa mifugo yote na kuwaelimisha wafugaji. Matokeo ya utafiti kuhusu ongezeko la tembo yatatolewa katika mwaka wa fedha 2018/2019 na yatasaidia kuandaa Mpango Kabambe wa Kuhifadhi Tembo katika mfumo ikolojia – Serengeti.

 1. Mheshimiwa Spika, Utafiti wa mimea na nyuki wanaouma na wasiouma umeendelea kufanyika katika wilaya 120. Matokeo ya awali ya utafiti huo yametumika kuchora ramani ya kiikolojia inayoonesha kanda muhimu za ufugaji nyuki nchini. Aidha, matokeo yameainisha aina za asali katika kanda na maeneo mbalimbali.

 1. Mheshimiwa Spika, Wadau wamendelea kushirikishwa kwenye uhifadhi wanyamapori ikiwa ni pamoja na kuwanufaisha na raslimali hizo. Programu ya Ujirani Mwema imetekelezwa katika vijiji 33 vinavyozunguka Hifadhi za Taifa kwa kuchangia miradi 89. Wilaya zilizofaidika na Programu hiyo ni Korogwe, Mwanga, Meru, Karatu, Makete, Same, Mlele, Lushoto, Bagamoyo, Kigoma Vijijini, Geita, na Moshi Vijijini. Aidha, miradi ya maji kwa ajili ya binadamu na mifugo imekamilika katika maeneo ya Mbitini, Ndepesi, Olduvai, Oldonyogol na Ngoile iliyopo kwenye Hifadhi ya Ngorongoro. Vilevile, jamii zimeshirikishwa katika kusimamia maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (38) na maeneo manne ya Ardhioevu (Ramsar Sites).

 1. Mheshimiwa Spika, Sensa ya watu, makazi na mifugo imefanyika katika Tarafa ya Ngorongoro ili kubaini idadi ya wakazi halali na mifugo ndani ya Hifadhi. Asilimia 60 ya wenyeji wanaoishi ndani ya Hifadhi wamepewa vitambulisho vya Taifa.  Aidha, ili kudhiti uingizaji holela wa mifugo ndani ya Hifadhi, ng’ombe 201,203 kati ya 238,845 wamewekwa alama ya utambulisho.

 1. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya taaluma ya wanyamapori (Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori – Mweka, Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori – Pasiansi, Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii, Likuyu –Sekamaganga) vinatekeleza majukumu yao kwa kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalam na kufanya utafiti kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na uendeshaji utalii. Vyuo vimedahili jumla ya wanafunzi 992, Mweka (551) na Pasiansi (441) katika ngazi ya Shahada, Stashahada na Astashahada.

Sekta Ndogo ya Misitu na Nyuki

 1. Mheshimiwa Spika, Jukumu kuu la Sekta Ndogo ya Misitu na Nyuki ni kuhifadhi na kusimamia misitu iliyopo ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuendeleza ufugaji nyuki. Utekelezaji wa kazi hizo umefanyika kupitia Idara ya Misitu na Nyuki; Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS); Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA); Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI); Chuo cha Misitu, Olmotonyi (FTI); Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora (BTI); Chuo cha Viwanda vya Misitu, Moshi (FITI); na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF). Aidha, wananchi, sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na wadau wengine wameshirikishwa kikamilifu.

Utekelezaji wa Masuala Mahsusi ya Sekta Ndogo ya Misitu na Nyuki

 

Kupandisha hadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza maandalizi ya kupandisha hadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuwa Mamlaka ya Misitu Tanzania. Uamuzi huu unalenga kuimarisha usimamizi wa misitu ya asili inayomilikiwa na Serikali Kuu, Halmashauri za Wilaya, na Serikali za Vijiji. Aidha, utekelezaji wa azma hii unazingatia haja ya kujenga mfumo madhubuti wa usimamizi wa misitu na ufugaji nyuki; kupitia miundo ya mamlaka mbalimbali za usimamizi wa misitu na nyuki; matumizi bora ya ardhi vijijini; na kuwa na chombo kimoja kitakachosimamia misitu ya hifadhi. Vilevile, tathmini inafanyika ili kuainisha misitu inayopaswa kupandishwa hadhi kuwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu.

 

Kuongeza Mashamba ya Miti

 1. Mheshimiwa Spika, Wakala umeanzisha Mashamba mapya manne yenye ukubwa wa hektari 76,967. Mashamba hayo ni: Chato-Biharamulo, hektari 50,000 (Chato); Mpepo, hektari 2,017 (Mbinga); Iyondomsimwa, hektari 12,000 (Ileje); na Pagale, hektari 12,950 (Mvomelo). Katika mashamba hayo mapya jumla ya hektari 1,335 zimepandwa miti. Hatua hii imeongeza idadi ya mashamba ya Serikali kutoka 18 hadi 23. Mashamba haya yametoa ajira 90,000 za moja kwa moja na 50,000 zisizo za moja kwa moja kwa wananchi.

 

Kuboresha Miundombinu ya Utalii Ikolojia

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kuboresha utalii ikolojia kwenye maeneo ya misitu, ujenzi wa ngazi na eneo la kupumzika katika maporomoko ya mto Kalambo unaendelea. Aidha, njia za kutembea kwa miguu katika hifadhi za mazingira asilia ya Mlima Hanang, Mlima Uluguru, Mkingu na Rondo zimejengwa. Vilevile, ujenzi wa majengo ya ofisi sita za wahifadhi na vituo (Ranger outposts) 15 unaendelea katika hifadhi za Chome, Mlima Rungwe, Magamba, Mkingu, Minziro na Uzungwa Scarp, ambapo ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 80. Pia, Hifadhi 12 zimepatiwa vifaa vya kisasa vya mawasiliano na usafiri. Wakala umeandaa  mipango ya usimamizi wa bioanuai na uendelezaji utalii. Pia, Misitu ya Hifadhi za Kalambo, Ituli na Uvinza inapandishwa hadhi kuwa Misitu ya Hifadhi Asilia.

Nishati Inayotokana na Kuni na Mkaa

 

 1. Mheshimiwa Spika, Zaidi ya asilimia 85 ya nishati yote nchini inatokana na kuni na mkaa ambapo takribani asilimia 90 ya wananchi wote hutegemea nishati hiyo. Hali hiyo inatokana na utegemezi mkubwa wa misitu ya asili kama chanzo kikuu na rahisi cha nishati na mapato kupitia biashara ya utengenezaji na uuzaji mkaa, kuni, mbao, na nguzo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kupunguza utegemezi huo, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuchukua hatua zifuatazo: kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama gesi na briquetes; kufundisha namna ya utengenezaji wa majiko banifu ya kutumia kuni na mkaa; kubaini maeneo ya misitu yenye miti inayofaa kwa utengenezaji wa mkaa; kufundisha mbinu bora za utengenezaji wa mkaa; na kuandaa maeneo maalum ya uuzaji wa mkaa (kwa mfano, vituo vya Maguha na Berega kwenye barabara kuu ya Dodoma – Morogoro); kuwatambua watengenezaji na wauzaji wa mkaa, na kuhamasisha wananchi na makundi mbalimbali ya watu kupanda miti kwa ajili ya kuzalisha kuni na mkaa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhimiza taasisi zenye matumizi makubwa ya nishati ya kuni na mkaa kwa mfano, Hospitali, Shule na Vyuo, na Majeshi (Polisi, Magereza, JKT na JWTZ) kutumia nishati mbadala na teknolojia zinazobana matumizi ya nishati.

Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mufindi (Mufindi Paper Mills)

 1. Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha kuzalisha karatasi cha Mufindi (Mufindi Paper Mills – MPM) kilibinafsishwa mwaka 2004 kwa Kampuni ya RAI Group ya Kenya. Kabla ya ubinafsishaji, Kiwanda hakikufanya kazi kwa miaka 14. Hali hiyo ilisababisha miti iliyokuzwa kwa ajili ya karatasi kufikia umri wa miaka 25 ambayo inafaa zaidi kwa ajili ya uzalishaji wa magogo ya mbao.  Aidha, wakati ubinafsishaji wa kiwanda unafanyika mkataba wake uliainisha kuwa Serikali itahakikisha kuwa kiwanda kinapata kiasi cha malighafi ya miti kisichozidi meta za ujazo 500,000 kila mwaka. Mkataba wa mauziano ya kiwanda haukuainisha viwango vya tozo na ada za malighafi ya kiwanda.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza mkataba huu, kumekuwepo na changamoto ya kukosekana kwa miti inayofaa kuzalisha miti ya tetefya (pulpwood), inayofaa kwa karatasi. Hivyo, kulazimika kutumia miti inayofaa kuzalisha magogo ya mbao ambayo tozo na ada zake ni kubwa kuliko zile za miti ya tetefya. Aidha, Kampuni haikuweka mkakati wa kuzalisha malighafi yake ya kutosha kutokana na eneo la kuotesha miti kwa ajili ya matumizi ya kiwanda kuvamiwa na vijiji jirani. Kutokana na hali hiyo, Kampuni haipo tayari kununua malighafi kwa tozo na ada za miti inayofaa kuzalisha magogo ya mbao. Katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, Wizara yangu imeunda kikosikazi kitakacho chambua na kushauri kuhusu masuala yafuatayo: mtiririko wa mahitaji na matumizi halisi ya kiwanda, viwango vya tozo na ada za malighafi ya kiwanda, uwezo wa shamba la Sao Hill kuhudumia kiwanda na wateja wengine, na kupitia mkataba kati ya Serikali na kiwanda.

Majukumu Mengine Yaliyotekelezwa na Idara, Wakala, Taasisi na Mfuko wa Misitu Tanzania

 

 1. Mheshimiwa Spika, Kazi zilizofanyika katika kulinda na kuendeleza misitu na ufugaji nyuki ni pamoja na: kuzuia uharibifu wa misitu; kudhibiti uvunaji wa mazao ya misitu usioendelevu; na kusimamia manzuki (apiaries). Kutokana na jitihada hizo, uoto wa asili umeanza kurejea kwenye maeneo hayo. Aidha, asali yenye uzito wa kilo 6,519 na nta yenye uzito wa kilo 281 imevunwa kutoka katika manzuki 143 zinazomilikiwa na TFS. Vilevile, vyanzo vipya vya mbegu za miti ya asili (mkongo na mkangazi), misindano, na mikaratusi vimeanzishwa ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mbegu za miti ya mbao.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kujenga uwezo wa watumishi na Taasisi, miundombinu na mazingira ya kazi yameboreshwa. Kazi zilizofanyika ni: kujenga ofisi mbili; kukarabati nyumba 40 za kuishi watumishi katika vituo mbalimbali; ujenzi wa jengo la maktaba katika Chuo cha Viwanda vya Misitu, Moshi – FITI na ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Misitu Olmotonyi. Aidha, ukarabati wa miundombinu ya kitalu cha miti umefanyika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo katika Chuo cha Misitu Olmotonyi. Vilevile, kilomita 1,329 za barabara zimesafishwa; na kilomita 99 za barabara mpya zimetengenezwa kwenye mashamba ya miti.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Utafiti wa misitu umefanyika kwenye nyanja tatu: i) Kubaini umri sahihi wa kuvuna miti ya Misindano na ubora wa mbao kutoka katika mashamba ya miti ya Rubare (Bukoba vijijini), Rubya (Ukerewe) na Buhindi (Sengerema); na ii) Kubaini chanzo halisi cha kukauka kwa miti aina ya Misindano na Grevilea katika Kanda ya Kaskazini; na iii) Kufanya tathmini ya wadudu waharibifu wa miti aina ya Mikaratusi ya kloni Wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa: i) Umri wa uvunaji wa miti aina ya misindano kwa ajili ya matumizi ya mbao ni kati ya miaka 18 hadi 20 badala ya miaka 25, na miaka 11 kwa ajili ya kuzalisha karatasi; ii) Miti ya Misindano na Grevilea iliyopandwa kwenye Shamba la Miti Kilimanjaro Magharibi lililopo Wilaya ya Siha, inakauka kutokana na ugonjwa wa kuoza mizizi (Root rot disease) unaosababishwa na fangasi jamii ya Armillaria; na iii) Utunzwaji sahihi wa mashamba ya miti ya Mikaratusi na matumizi ya viatilifu vinavyoweza kuzuia na kuua wadudu.

 1. Mheshimiwa Spika, Taarifa za moto zilizokusanywa kwa njia ya satellite zinaonesha kuwa janga la moto kwa misitu bado ni kubwa na limeathiri eneo la misitu lenye kilometa za mraba 101,955 katika mikoa ya Katavi, Tabora, Kigoma na Mbeya. Kutokana na taarifa hizo, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuelimisha umma kuhusu kuchukua tahadhari na kuzuia moto wa misitu.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha kuwa wadau wanashiriki kwenye kusimamia na kuendeleza raslimali za misitu na nyuki, wadau mbalimbali wamewezeshwa kutekeleza miradi 204. Miradi hiyo inatekelezwa kwenye nyanja za: upandaji wa miti (65), ufugaji nyuki (92), upandaji miti na ufugaji nyuki (17), ushirikishwaji jamii katika usimamizi wa misitu (10), nishati mbadala na utumiaji wa majiko banifu (6), utafiti (10) na viwanda vya mazao ya nyuki (4).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Misitu Olmotonyi kimetoa mafunzo ya muda mrefu kwa wanafunzi 672, kati yao 405 ni wa Astashahada na 267 ni wa Stashahada. Aidha, Chuo cha Viwanda vya Misitu kimetoa mafunzo kwa wanafunzi 133, kati yao 113 ni wa Astashahada na 20 ni wa Stashahada. Vilevile, Chuo cha Ufugaji Nyuki kimetoa mafunzo kwa wanafunzi 201 katika ngazi za Astashahada (171) na Stashahada (30).

 

Sekta Ndogo ya Utalii

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jukumu kuu la Sekta Ndogo ya Utalii ni kuendeleza utalii nchini, na kuhakikisha inachangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa. Utekelezaji wa jukumu hilo unafanyika kupitia Idara ya Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na Chuo cha Taifa cha Utalii kwa kushirikisha wananchi, sekta binafsi, na wadau wengine.

Kuandaa Utambulisho wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding)

 

 1. Mheshimiwa Spika, Katika juhudi za kutangaza utalii, Wizara imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa Utambulisho wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding). Lengo la utambulisho huo ni kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii Duniani; kuvutia wageni wa kimataifa kuitembelea Tanzania; kuongeza wigo wa kutangaza vivutio; na kuvifanya vivutio vya utalii vya Tanzania vifahamike duniani. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara imeandaa Kauli Mbiu ya kuitangaza Tanzania katika masoko ya utalii ambayo ni Tanzania, Unforgettable. Hatua inayofuata ni kuandaa mionekano (visuals) ambayo itaelezea kwa undani na kwa urahisi vionjo vya vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Uanzishaji wa “Studio” na Chaneli ya Utalii Tanzania

 

Mheshimiwa Spika, Wizara inashirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuanzisha Chaneli maalum katika Televisheni ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii. Aidha, Wizara inaendelea na maandalizi ya kuanzisha “Studio” ya kutangaza utalii kwa njia ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Studio hiyo itawezesha kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja kwa moja na watu wanaofuatilia Tanzania na vivutio vyake kwa njia ya TEHAMA.

Majukumu Mengine Yaliyotekelezwa na Idara, Bodi, na Chuo cha Taifa cha Utalii

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jukumu la kuendeleza utalii limetekelezwa kwa kupanga daraja za ubora wa huduma za malazi na chakula kwa viwango vya kati ya nyota moja hadi tano; kufanya ukaguzi wa wakala wa biashara za utalii; na kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi. Upangaji wa daraja za ubora wa huduma za malazi na chakula 230 umefanyika katika mikoa ya Arusha na Manyara.

 1. Mheshimiwa Spika, Ukaguzi wa wakala wa biashara za utalii umefanyika katika mikoa nane na kwenye malango ya kuingilia wageni ya Hifadhi za Taifa Kilimanjaro, Mikumi, Ngorongoro, na Pori la Akiba Selous.  Aidha, kazi ya kutangaza utalii wa ndani  na wa nje imefanyika kupitia maonesho ya ndani (10) na ya nje (10); ziara za timu ya mpira, waandishi wa habari na watu mashuhuri; mabango; machapisho; vyombo vya habari; na mabasi ya abiria.

 1. Mheshimiwa Spika, Kampeni maalum ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutumia kauli mbiu “Utalii wa ndani unaanza na mtanzania mwenyewe” ilifanyika kupitia redio na televisheni. Aidha, onesho la kimataifa la utalii “Swahili International Tourism Expo – S!TE” limefanyika tarehe 13 hadi 15 Oktoba 2017, jijini Dar es Salaam.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Taifa cha Utalii kimedahili jumla ya wanafunzi 228 kati ya hao 209 ngazi ya Astashahada na 19 ngazi ya Stashahada. Aidha, wanafunzi 102 wamedahiliwa programu ya uanagenzi (apprenticeship). Wanafunzi 154 wamehitimu katika ngazi za Astashahada na Stashahada.

Sekta Ndogo ya Mambo ya Kale

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jukumu kuu la Sekta Ndogo ya Mambo ya Kale ni kufanya utafiti, kutambua, kuhifadhi, kulinda, kuendeleza na kutangaza malikale. Utekelezaji wa jukumu hilo umefanyika kupitia Idara ya Mambo ya Kale na Shirika la Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na wananchi, sekta binafsi, na wadau wengine.

Kuendeleza Vituo vya Mambo ya Kale

 

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kuendeleza vituo vya mambo ya kale, Wizara imeandaa Mkakati wa Kuendeleza Maeneo ya Malikale. Maeneo ya kipaumbele ni: Laetoli, Engaruka, Mumba, Nasera na Engaresero; Mapango ya Amboni na Magofu ya Kunduchi. Maeneo mengine ni Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, Caravan Serai na Kaole; Michoro ya Miambani ya Kondoa; Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Isimila, Kalenga na Kimondo cha Mbozi; Tembe la Kwihara na Old Afya Building; na Kituo cha Livingstone Ujiji.

 1. Mheshimiwa Spika, Mkakati huo utahusisha kuweka huduma muhimu kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususan vituo vya kumbukumbu na taarifa, ofisi, mabanda ya kupumzika watalii na barabara ili viwe na muonekano unaovutia na kufikika kwa urahisi. Kazi nyingine zitakazotekelezwa ni kujenga vituo vya taarifa pale ambapo vitahitajika, kuandaa vionyeshwa, maonyesho na kutangaza vituo. Aidha, Mkakati huo utatekelezwa kwa ushirikiano na Mashirika ya TANAPA, NCAA, TAWA, TFS, TTB na NMT. Vilevile, wadau hususan sekta binafsi na wananchi watashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wake.

Tamasha la Urithi wa Taifa  (Urithi Festival: Celebrating Our Heritage)

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imebuni maadhimisho ya Tamasha la Urithi wa Taifa (Urithi festival). Lengo la Tamasha hilo ni kunadi urithi na utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi. Tamasha litajielekeza zaidi kwenye historia, utamaduni, malikale, lugha, chakula, mavazi, imani, mila na desturi. Wizara kwa kushirikiana na wadau imeanza maandalizi ya maadhimisho ya Tamasha hilo yatakayofanyika Septemba kila mwaka katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika kutekeleza azma hiyo, Kamati ya Kitaifa imeundwa ili kuratibu maandalizi ya Tamasha hilo. Aidha, Tamasha litaongeza wigo wa mazao ya utalii kwa kunadi vivutio vya urithi wa taifa, kuongeza uelewa wa wageni kuhusu Tanzania na idadi ya siku ambazo watalii watakaa nchini.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara kupitia Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Tamasha imekamilisha kazi zifuatazo: kuandaa mwongozo wa kufanikisha tamasha kila mwaka; kuainisha shughuli zitakazotekelezwa; na kuwashirikisha wadau katika maandalizi na ufanikishaji wa Tamasha.

Majukumu Mengine Yaliyotekelezwa na Idara na Shirika la Makumbusho ya Taifa

 

 1. Mheshimiwa Spika, Utafiti wa malikale umefanyika katika mikoa 15 kwenye nyanja 74 za: akiolojia; palentolojia; biolojia; na utafutaji wa tunu. Matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuongeza idadi ya vivutio vya utalii wa malikale na kupata taarifa sahihi za kuweka kwenye maonesho ndani ya kumbi za makumbusho na kwa ajili ya kuboresha program za elimu. Aidha, kazi zilizotekelezwa katika kutambua, kulinda na kuhifadhi malikale ni pamoja na: kutangaza maeneo ya malikale kuwa Urithi wa Taifa; kumairisha mipaka; kuanzisha makumbusho mapya; na kuimarisha ulinzi wa mikusanyo. Aidha, Mji wa Kihistoria wa Mikindani umetangazwa kuwa Urithi wa Taifa na mipaka ya Kituo cha Mapango ya Amboni imeimarishwa kwa alama za kudumu (vigingi).

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kuboresha miundombinu, ujenzi wa kituo cha Kumbukumbu na Taarifa katika eneo la Kimondo cha Mbozi, Songwe umekamilika. Kazi nyingine zilizofanyika ni: kuboresha kituo kipya cha Engaruka ambacho kinahifadhi historia ya mfumo wa umwagiliaji wa kijadi wa karne ya 13 hadi 17;  kujenga uzio wa ukuta katika Makumbusho ya Dkt. Rashid M. Kawawa, Bombambili (Songea); kujenga na kukarabati nyumba sita za asili katika kijiji cha makumbusho.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Uendelezaji na utangazaji wa malikale umefanyika kwa kuhamasisha utalii wa malikale; kuboresha maonesho; na kufanya maadhimisho. Vipindi vinne vya televisheni kuhusu ushiriki wa wadau katika matumizi endelevu ya malikale viliandaliwa na kurushwa. Aidha, maonesho ya muda na ya kudumu  katika makumbusho saba yameboreshwa kwa kubadili vioneshwa, mipangilio ya maonesho na maelezo ya vioneshwa.  Vilevile, maonesho mawili ya kudumu kuhusu Chimbuko la Binadamu Afrika na Uzalendo katika Vita vya Majimaji yamefunguliwa.

 

 Miradi ya Maendeleo

 

 1. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2017/2018 jumla ya Shilingi 51,803,284,000 ziliidhinishwakwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo 12. Miradi 10 imetekelezwa kwenye Sekta Ndogo za Wanyamapori (4), Misitu na Nyuki (5), na Utalii (1). Kati ya fedha ziliidhinishwa, Shilingi 33,803,284,000 ni fedha za ndani na Shilingi 18,000,000,000 fedha za nje. Hadi mwezi Machi 2018, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 27,946,780,919 sawa na asilimia 54 ya fedha zilizoidhinishwa. Kati ya hizo, Shilingi 11,353,250,489 ni fedha za ndani na Shilingi 16,593,530,813 fedha za nje.

Masuala Mtambuka

Utawala na Raslimaliwatu

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo watumishi 17 kwa kuwawezesha kupata mafunzo ya muda mfupi (3) na muda mrefu (14) ndani na nje ya nchi.

 

 Mifumo na Matumizi ya TEHAMA

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kutengeneza mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA unaoitwa “MNRT Portal wa kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii. Mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa Serikali wa malipo wa Ki-elektronik – Government electronic Payment Gateway (GePG) na kuhuishwa na mifumo mingine ya Serikali kama vile, ya Uhamiaji, NIDA, TIRA, BRELA, TRA, na NBS.

Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza mikataba ya East African Community (EAC), Southern African Development Community (SADC), Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora (CITES), United Nations – World Tourism Organisation (UNWTO), United Nations Development Programme (UNDP), United Nations Educational, Scientific and Cultural Organisation (UNESCO), International Council of Museums (ICOM), International Center for the Study of the Preservation and Resoration of Cultural Property (ICCROM), International Council on Monument and Sites (ICOMOS), na Lusaka Agreement Task Force (LATF) katika kutekeleza majukumu yake. Kupitia ushirikiano huo, Wizara inanufaika na misaada ya kitaalam na fedha, kubadilishana uzoefu, kupata vifaa mbalimbali na kuimarisha ushirikiano.

Utatuzi wa Migogoro

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutatua migogoro kati ya wananchi na hifadhi kwa kuweka vigingi vya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi. Hadi Machi 2018, jumla ya vigingi 27,942 vimesimikwa ikiwa ni sawa na asilimia 79.4 ya malengo. Kazi hiyo inatekelezwa na TANAPA, NCAA, TAWA, na TFS kwa kuwashirisha wananchi walio karibu na Hifadhi za Taifa, Hifadhi ya Ngorongoro, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu, na Hifadhi za Misitu.

Majukumu ya Kimkakati

Kutekeleza Agizo la Serikali la kuhamia Dodoma

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza Agizo la Serikali la kuhamia Dodoma, Wizara imewahamisha watumishi 201. Wizara inatumia Ofisi iliyopo eneo la Kilimani Barabara ya Askari na Ofisi ya Chuo Kikuu Dodoma (University of Dodoma – UDOM). Aidha, watumishi 46 waliobakia Ofisi ya Dar es Salaam watahamia katika mwaka wa fedha 2018/2019.

 Mradi wa Kuzalisha Umeme Rufiji

 1. Mheshimiwa Spika, Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji (Rufiji Hydropower Project) unatekelezwa na Wizara ya Nishati, ambapo eneo la mradi liko katika Pori la Akiba Selous. Katika utekelezaji wa Mradi huu, Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa jukumu la kukata miti katika eneo ambapo bwawa hilo litajengwa. Aidha, Wizara imepewa jukumu la kuimarisha ulinzi wa maeneo ya lindimaji na kutoa wataalam kwenye eneo la Mradi. Katika mwaka huu wa fedha, Wizara imeanza kufanya tathmini ya maliasili zinazopatikana kwenye eneo la Mradi. Tathmini hiyo inalenga kupata thamani ya mazao ya misitu yatakayovunwa na kuuzwa kibiashara na kutambua spishi za mimea na wanyamapori zinazoweza kuwa hatarini kutoweka ili kuweka mikakati ya kuzihifadhi.

Kuwezesha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwenye Sekta

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imehusika katika kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Comprehensive Action Plan for Improvement of Business Environment and Investment Climate). Katika kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, Wizara inazingatia azma hiyo kwenye mapitio ya sera, sheria na kanuni za usimamizi wa maliasili, malikale na uendelezaji utalii.

Mafanikio, Changamoto na Utatuzi  Wake

 

Mafanikio

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili, biashara haramu ya misitu na wanyamapori, uvamizi wa maeneo ya hifadhi na matukio ya moto. Mafanikio haya yamechangiwa hasa na uimarishaji wa mipaka ya hifadhi, ulinzi na intelijensia, na ushirikishaji wananchi na wadau wengine katika uhifadhi.

 1. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 1,284,279 (mwaka 2016) hadi kufikia watalii 1,327,143 (mwaka 2017). Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 3.3. Aidha, mapato yatokanayo na Utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 2,131.57 (mwaka 2016) hadi kufikia Dola za Marekani milioni 2,250.3 (mwaka 2017). Ongezeko hilo la mapato ni sawa na asilimia 5.6.

Changamoto

 1. Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali; uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kibinadamu. Aidha, kumekuwepo na matatizo ya moto, ongezeko la uchimbaji wa madini ndani ya maeneo ya uhifadhi na ukataji miti kwa ajili ya biashara ya mkaa.

Utatuzi wa Changamoto

 1. Mheshimiwa Spika, Kutokana na changamoto hizo, Wizara itaendelea kuchukua hatua stahiki wakati wa kutekeleza Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019. Aidha, Wizara itaendelea kuwashirikisha wananchi na wadau wengine, hususani sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo, Asasi za Kiraia na marafiki wa uhifadhi katika kutekeleza majukumu yake.

MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019

 1. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara itatekeleza mpango na bajeti ambao umezingatia majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Sehemu ya Pili ya Hotuba hii. Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza majukumu ya Taifa ya Kimkakati na maagizo mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuzingatia mikakati ya kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2017/2018.

          Ukusanyaji Maduhuli

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara na Taasisi zake inakadiria kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 2 kutokana na vyanzo vya Idara na Taasisi zilizo chini yake. Aidha, Mashirika yaliyochini ya Wizara (TANAPA, NCAA, TAWA, na TFS) yanakadiria kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 623.5. Makadirio haya ya mashirika ni ongezeko la Shilingi Bilioni 167.4 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka 2017/2018.

Matumizi ya Kawaida na Maendeleo

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara inakadiria kutumia Shilingi Bilioni 8 kwa Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 85.8 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 30 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/2019 umefafanuliwa kama ifuatavyo:-

Mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu (1998), Ufugaji Nyuki (1998) na Utalii (1999). Kazi hii itatekelezwa sanjari na kutayarisha Mikakati ya Utekelezaji wa Sera hizo. Aidha, Wizara itaendelea kupitia Sheria za Usimamizi wa Maliasili, Malikale na Utalii. Vilevile, Wizara itaendelea kukamilisha mapitio ya Kanuni za Biashara ya Nyara; na usimamizi wa Mkataba wa CITES.

Majukumu ya Wizara na Taasisi zake

 

Sekta Ndogo ya Wanyamapori

Idara ya Wanyamapori

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kulipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu.

Shirika la Hifadhi za Taifa

 1. Mheshimiwa Spika, Miundombinu ya kuhifadhi maji wakati wa kiangazi itawekwa katika Hifadhi za Taifa tano. Kazi nyingine zitakazofanyika ni kuwezesha utayarishaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 95 kati ya 392 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa sita; na kujenga vituo vinne vya askari kwenye maeneo yenye matukio ya mara kwa mara ya wanyamapori wakali na waharibifu, hususan, Bunda, Tarime, Itilima na Serengeti. Aidha, Shirika litatekeleza mkakati wa kuendeleza vivutio vya kihistoria na kitamaduni vilivyo jirani na hifadhi za Taifa.

 

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro

 1. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaboresha mtandao wa miundombinu ya barabara ikiwemo ujenzi wa barabara ya Loduare hadi Golini yenye urefu wa kilomita 88 kwa kiwango cha lami; na kukarabati viwanja vya ndege. Aidha, Mamlaka itaongeza wigo wa shughuli za utalii; kujenga vituo viwili vya askari kwenye maeneo yenye changamoto za kiusalama; na kununua vifaa vya kisasa vya ulinzi na kutoa mafunzo kwa askari.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, itaimarisha ulinzi wa wanyamapori kwa kuendesha doria na kutoa mafunzo kwa watumishi. Aidha, Mamlaka itafanya tathmini na kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi ndani ya Pori la Akiba Mkungunero. Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na kuboresha mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 1,192 katika Mapori ya Akiba sita; na kujenga ofisi na kukarabati nyumba tano.

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania itaendelea kufanya, kuratibu na kusambaza matokeo ya miradi 126 ya utafiti wa wanyamapori. Miradi hiyo imejikita kwenye ikolojia, tabia za wanyamapori, mwenendo wa magonjwa, ufugaji nyuki, na migongano kati ya binadamu na wanyamapori. Aidha, Taasisi  itakamilisha ujenzi wa maabara ya kisasa ya ufugaji   Vilevile, Taasisi itafanya sensa ya wanyamapori katika mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi na sensa ya mamba na viboko katika maeneo mengine.

 

Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori

 

 1. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori vitaendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa wanafunzi 1,021 na muda mfupi kwa wanafunzi 720.

Sekta Ndogo ya Misitu na Nyuki

 

Idara ya Misitu na Nyuki

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuratibu siku za kitaifa za kupanda miti na kutundika mizinga; kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Misitu za Vijiji na kuratibu mikutano minne ya Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Misitu (NAFAC).

 Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania utapanda miti kwenye mashamba yenye ukubwa wa jumla ya hektari 9,683 ikiwa ni pamoja na hektari 1,550 kwenye mashamba mapya sita ya miti. Aidha, Wakala utawezesha wananchi kuotesha na kupanda miche ya miti 8,481,000 katika vijiji vinavyozunguka hifadhi za misitu na mashamba ya miti. Vilevile, Wakala utaendelea kuimarisha mipaka ya hifadhi za misitu kwa kusafisha mipaka yenye kilometa 10,546.57 na kusimika vigingi 3,318. Pia, Wakala utaendelea kusimamia manzuki (apiaries) 143 zenye jumla ya mizinga 6,214.

 

Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wakala utazalisha na kuuza miche 4,600,000 ya miti; na utakusanya tani 25 za mbegu bora za miti na kuuza tani 20. Aidha, Wakala kwa kushirikiana na Mfuko wa Misitu Tanzania utaanzisha bustani ya miti yenye uwezo wa kuzalisha miche 1,000,000 mjini Dodoma kwa ajili ya mahitaji ya Jiji la Dodoma na viunga vyake.

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania itaanzisha majaribio ya kiutafiti ya upandaji sahihi wa miti kwenye eneo la jumla ya hektari 100 katika Kanda za Ziwa, Kati, Mashariki, Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini; na kusimamia majaribio mapya ya utafiti. Matokeo ya majaribio haya yataongeza wigo wa spishi za miti ya asili itakayokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

 

Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki

 

 1. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Misitu na Ufugaji Nyuki vitaendelea kutoa mafunzo kwa kudahili jumla ya wanafunzi 1,254.

Mfuko wa Misitu Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Misitu Tanzania utawezesha miradi 294 inayoendelea na miradi mipya 62 ya uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa raslimali misitu.

 

 

 

 

Sekta Ndogo ya Utalii

 

Idara ya Utalii

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kuboresha huduma za utalii, Wizara itaendelea kuweka huduma za malazi katika daraja la ubora wa nyota katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Mwanza. Aidha, vivutio vipya vya utalii vitabainishwa katika mikoa ya Simiyu, Geita, Kigoma, Kagera, Tanga na Manyara. Vilevile, Wizara itaanza  maandalizi ya kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Uendelezaji wa maeneo ya fukwe.

Bodi ya Utalii Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuitambulisha Tanzania Kimataifa (Destination Branding) na kukamilisha uanzishwaji wa “Studio” ya kuutangaza utalii kwa njia ya TEHAMA. Aidha, Bodi itakamilisha Mkakati wa Kukuza Utalii wa Mikutano.

Chuo cha Taifa cha Utalii

 

 1. Mheshimiwa Spika, Chuo kitadahili wanafunzi 215 wa Astashahada, 100 wa Stashahada na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa washiriki 800.

Sekta Ndogo ya Mambo ya Kale

Idara ya Mambo ya Kale

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kupima maeneo manne ya malikale katika vituo vya Mtwa Mkwawa – Kalenga na Zana za Mawe – Isimila (Iringa); Mapango ya Amboni (Tanga); na Magofu ya Kaole – Bagamoyo (Pwani). Aidha, Wizara itajenga kituo cha kumbukumbu na taarifa katika eneo la Mapango ya Amboni na kukarabati  ofisi ya kituo cha Engaruka. Vilevile, Wizara itakarabati Nyumba Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Magomeni na kukusanya taarifa za kina kuhusu  nyumba hiyo.

Shirika la Makumbusho ya Taifa

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika litaratibu Tamasha la Urithi wa Taifa (Urithi Festival) litakalofanyika Septemba 2018 na maandalizi ya awali ya kuanzisha Makumbusho ya Marais, Dodoma yatafanyika. Aidha, Shirika litaboresha na kuhakikisha usalama wa mikusanyo; kutangaza Makumbusho na vivutio vyake vya utalii na kufanya Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania. Vilevile, utafiti utafanywa kwenye nyanja 13. Pia, Wizara imepanga kupanua Makumbusho ya Elimu Viumbe, Arusha ili yajumuishe ukumbi utakaokuwa na onesho la tembo.

 

Miradi ya Maendeleo

 1. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2018/2019 Wizara itatumia jumla ya Shilingi 29,978,082,000 kutekeleza miradi 11 ya Maendeleo. Miradi hiyo itatekelezwa kwenye Sekta Ndogo za Wanyamapori (3), Misitu na Nyuki (5), na Utalii (3). Fedha zinazombwa zinajumuisha Shilingi 3,000,000,000 fedha za ndani na Shilingi 26,978,082,000 fedha za nje.

 

 

Masuala Mtambuka

Utawala na Raslimaliwatu

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara na Taasisi zake itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii. Aidha, Wizara itaendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwawezesha kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu.

 

 

Kuanzisha Jeshi Usu

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kukamilisha uanzishaji wa Jeshi Usu (Paramilitary) kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa taaluma za wanyamapori, misitu na nyuki; na kujenga uwezo kitaasisi kwa kuongeza vitendea kazi na matumizi ya teknolojia.

         Mifumo na Matumizi ya TEHAMA

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itafanya tathmini ya miundombinu ya TEHAMA katika vituo vyote vya kutolea huduma vilivyoko kwenye Wizara na Taasisi zake. Aidha, miundombinu ya TEHAMA itaanza kufungwa kwenye vituo kulingana na mahitaji.

        Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutekeleza Mikataba mbalimbali ya ushirikiano ya kikanda na Kimataifa kwenye Nyanja za maliasili, malikale, na utalii ambayo nchi imeridhia.

Majukumu ya Kimkakati

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake ili kufanikisha mradi wa kuzalisha umeme Rufiji na kuwezesha mazingira ya biashara na uwekezaji. Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza maagizo ya viongozi wa Kitaifa yatakayotolewa wakati wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti.

SHUKRANI

 1. Mheshimiwa Spika, Kipekee napenda kushukuru nchi, mashirika, taasisi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliotoa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu. Nachukua fursa hii kutaja baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali za China, Denmark, Finland, Hispania, Kanada, Marekani, Norway, Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, Uswisi na Jumuiya ya nchi za Ulaya. Mashirika na Taasisi ni pamoja na NORAD, AFB, ASEP, EAC, WB, UNDP, SADC, UNESCO, WWF, UNWTO, ICOM, ICCROM, ICOMOS, CITES, USAID, KfW, GIZ, LATF na PAMS Foundation.

MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019

 

 1. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2018/2019, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 115,794,740,000 kwa matumizi ya Fungu 69 – Wizara ya Maliasili na Utalii. Kati ya fedha hizo, Shilingi 85,816,658,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 29,978,082,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

 1. Mheshimiwa Spika, Fedha za Matumizi ya Kawaida zinajumuisha Shilingi 47,758,514,000 za Mishahara na Shilingi 38,058,144,000 za Matumizi Mengineyo. Aidha, fedha za maendeleo zinajumuisha Shilingi 3,000,000,000 fedha za ndani na Shilingi 26,978,082,000 fedha za nje.

 1. Mheshimiwa Spika, Ninaomba kuhitimisha kwa kukushukuru wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.  Hotuba hii itapatikana pia katika  tovuti ya Wizara ya Maliasili na Utalii – mnrt.go.tz.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ninaomba kutoa hoja.

 

22 thoughts on “Hotuba ya waziri wa maliasili na utalii mheshimiwa Dkt. Hamisi a. Kigwangalla (mb) wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa fedha 2018/2019

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *