Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Hospitali  ya  Benjamin Mkapa Yanga’ra Huduma za Kibingwa

 

Na; Frank Mvungi- Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa yawahakikishia wananchi huduma bora za kibingwa zinazowezesha Serikali kuokoa kiwango kikubwa cha fedha kinachotumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA, Mkurugenzi  Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt   Alphonce   Chandika amesema kuwa   wanavyo vifaa tiba vya kisasa na wataalamu waliobobea katika kutoa huduma za kibingwa zinazowawezesha wananchi kutokusafiri nje ya nchi kufuata huduma hizo.

“ Kujengwa kwa Hospitali hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoagiza kujengwa kwake ikiwa na hadhi ya kutoa huduma za kibingwa nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo figo, moyo na magonjwa ya ndani” Alisisitiza Dkt  Chandika.

Akifafanua amesema kuwa tayari wagonjwa saba (7) wameshapandikizwa figo, wagonjwa 35 wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kutokana na matatizo ya figo, wakati wagonjwa 41 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika Hospitali hiyo.

Aliongeza kuwa kwa sasa wanauwezo wa kufanya upasuaji kwa njia ya matundu madogo kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa vya Endoscopy. Aidha uwepo wa vifaa kama MRI, CT Scan, X-Ray, Mammograph na Cathlab vimeiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma bora kwa wananchi kwani vifaa hivi ni sawa na vile vinavyotumika katika nchi zilizoendelea hivyo kuifanya Hospital hiyo kuwa miongoni mwa sehemu bora za kutolea huduma za matibabu hapa nchini.

Alibainisha kuwa kwa siku hospitali inahudumia wagonjwa 350 hadi 400 wanaotoka katika mikoa mbalimbli hapa nchini.

Pia aliwahakikishia wawekezaji na Mabalozi  wa mataifa mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwa Hospitali hiyo inaouwezo wa kutoa huduma za kibingwa zinazokidhi vigezo vya kimataifa hali iliyowavutia wawekezaji na Makampuni mbalimbali ikiwemo ile inayojenga reli ya kisasa ya kwa kiwango cha Kimataifa ( SGR) kutoka Dar es Salaam  hadi Makutopora Dodoma.

 Aidha, Hospitali hiyo imekuwa ikitumika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma udaktari katika vyuo vikuu vya afya hapa nchini kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma ikiwa ni sehemu ya ushirikiano mzuri ulipo kati yake na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Kwa upande wake Daktari  Bingwa wa magonjwa ya figo  Dkt.  Kessy Shija amesema kuwa wanazo mashine 10 za kuchuja damu kwa wagonjwa wa figo.

Pia Dkt Shija aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuiwezesha Hospitali hiyo  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Hospitali ya Benjamin Mkapa iko Jijini Dodoma na imejikita katika kutoa huduma Bora za kibingwa kwa wananchi wote na wawekezaji watakaokuja kuwekeza jinini Dodoma na maeneo mbalimbali hapa nchini.

One thought on “Hospitali  ya  Benjamin Mkapa Yanga’ra Huduma za Kibingwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama