Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Hatua kali Kuchukuliwa kwa Madereva Wazembe: Kamanda Muslimu

Na Eliphace Marwa.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu Jijini Dar es Salaam limetahadharisha, madereva kuwa makini wakati wakiendesha vyombo vya moto ili kuepuka ajali zinazosababishwa na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani SACP Fortunatus  Muslimu wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama barabarani katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mpaka Mei mwaka huu ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka jana.

Akisoma taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Kamanda Muslimu amesema kuwa ajali za barabarani zimepungua ukilinganisha na mwaka jana kwani katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Mei jumla ya ajali za magari zilikuwa 4,177, vifo 1,286 na majeruhi 3,882 ukilinganisha na ajali 2,411, vifo 1,034 na majeruhi 2,291 katika kipindi kama hicho mwaka huu.

Aidha kwa upande wa ajali za pikipiki Kamanda Muslimu amesema kuwa katika kipindi cha Januari mpaka Mei mwaka jana jumla ya ajali za pikipiki zilikuwa 1,110, vifo 347 na majeruhi 950 ukilinganisha na ajali 607, vifo 302 na majeruhi 455 katika kipindi kama hicho mwaka huu.

Pamoja na kupungua kwa ajali nchini Kamanda Muslimu amesema kuwa ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja mwendokasi wa madereva, kupita magari bila ya tahadhari, ulevi pamoja na kubeba abiria kupita kiasi kwa njia zilizo hatarishi.

Kamanda Muslimu aliongeza kuwa kwa sasa ukamataji wa makosa ya barabarani yatakuwa kipaumbele, hivyo dereva atakeyekiuka sheria atachukuliwa hatua palepale ili kujenga utii wa sheria bila ya shuruti.

“Ukamataji wa makosa utakuwa ni moja ya kipimo cha utendaji wa askari barabarani  ili waweze kukamata makosa mengi mpaka pale madereva watakapoacha kukiuka sheria”, alisema Kamanda Muslimu.

Aidha Kamanda Muslimu amesema kuwa jeshi hilo halitomuonea mtu wala kumbambikia mtu makosa kwani ukamataji huo wa makosa ya barabarani unalenga kuzuia ajali na sio kukusanya mapato na hivyo kuwataka askari kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali wafanye kazi kwa nidhamu na maadili ya jeshi hilo.

Kamanda Muslimu amewataka watumiaji wa barabara kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima ambazo husababisha vifo na majeruhi na kupelekea kuathiri uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla kutokana na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

 

66 thoughts on “Hatua kali Kuchukuliwa kwa Madereva Wazembe: Kamanda Muslimu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama