Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

GCLA Watoa Mafunzo kwa Wasimamizi 60 wa Kemikali

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, Bw. David Elias (kushoto) akizungumza na washiriki wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa shughuli za kemikali viwandani na kwenye makampuni yanayojihusisha na shughuli za kemikali katika Ukumbi wa CEEMI, Dar es Salaam. Mafunzo hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Mashariki.

Na Jacquiline Mrisho.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa mafunzo kwa wasimamizi wanaohusika na shughuli za kemikali wapatao 60 wa Kanda ya Mashariki yatakayowasaidia kuzuia matatizo yanayosababishwa na uelewa mdogo wa masuala ya kemikali.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefunguliwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma ya Vinasaba, David Elias kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Fidelice Mafumiko.

Mkurugenzi Elias amesema kuwa kemikali zina umuhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu lakini pamoja na faida hizo, kemikali zikitumiwa vibaya zinaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya usimamizi salama wa kemikali wakifuatlia mada mbalimbali zilizokuwa zinatotolewa na wawasilishaji kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Mashariki kwa wasimamizi wa shughuli za kemikali kwenye Viwanda, Taasisi na Makampuni mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za kutumia, kuhifadhi, kusafirisha, kuagiza na kuuza kemikali mbalimbali nchini.

“Ili kudhibiti madhara yanayosababishwa na matumizi yasiyo salama ya kemikali mbalimbali Mamlaka imepewa jukumu la kutoa mafunzo kuhusu usimamizi na udhibiti wa kemikali kwa wasimamizi wa shughuli hizi hivyo Mamlaka imeshatoa mafunzo kwa wasimamizi 86 kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu,”alisema Elias kwa niaba ya Dkt. Mafumiko.

Elias amefafanua kuwa kabla ya kuwekwa sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani, kemikali zilikuwa zikiingizwa nchini kiholela na kutumika pasipo usimamizi lakini baada ya sheria kupitishwa na kuanza kutekelezwa Mamlaka hiyo imepunguza madhara mbalimbali yanayoweza kusababishwa na matumizi ya kemikali.

Amewataka wahusika wakuu wa shughuli za kemikali kuhakikisha kampuni zao zinasajiliwa na Mamlaka hiyo kabla ya kujihusisha na shughuli yoyote ya kemikali pia wasambazaji wanatikiwa kuhakikisha wanasambaza kemikali kwa wale tu wanaotambulika na mamlaka hiyo.

Wakurugenzi na Meneja wa Kanda ya Mashariki kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (waliokaa) wakiwa pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya usimamizi salama wa kemikali yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa CEEMI, Dar es Salaam. Mafunzo hayo yamefunguliwa leo na kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba Bw. David Elias (aliyekaa katikati), kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara, Bw. George Kasinga (aliyesimama) akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya usimamizi salama wa kemikali yaliyoandaliwa na Kanda ya Mashariki na kuanza leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa CEEMI, Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali, Christopher Anyango ametoa rai kwa wahusika wanaoshiriki katika mafunzo hayo kuwa ni vizuri wakihudhuria viongozi wa viwanda kuliko kuwatuma wawakilishi kwani ni rahisi kiongozi kuwalekeza maafisa walio chini yao.

Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa wanaofanya shughuli za kemikali hivyo wajitahidi kuhudhuria kwa wingi katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka hiyo.

109 thoughts on “GCLA Watoa Mafunzo kwa Wasimamizi 60 wa Kemikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *