Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

FIFA Yakunwa na Utendaji wa Rais Magufuli

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Kinyango Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani(FIFA)Bwana Gianni Infantino katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu February 22/2017Jijini Dar es salaam Tanzania

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea Bandera ya FIFA kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani(FIFA)Bwana Gianni Infantino katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu February 22/2017Jijini Dar es salaam Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ameondoka nchini huku akionesha kufurahishwa na juhudi za Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa na ufisadi katika kujenga uchumi wa Tanzania.

Rais huyo wa FIFA alionyesha kuukubali utendaji wa Rais Magufuli wakati akiongea na jopo la wahariri wa habari za michezo nchini baada ya Mkutano wa Mkuu wa FIFA uliofanyika hapa nchini siku ya Alhamisi.

Infantino amesema moja ya mambo aliyokabiliana nayo alipoingia tu katika uongozi wake ni kupambana  na rushwa na ufisadi katika shirikisho hilo na hivyo juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania chini ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa zinamvutia sana.

“Kama inavyotokea hapa Tanzania na sisi tunapambana na rushwa. Kwa yeyote atakayetumia vibaya fedha za maendeleo ya soka, hatutamvumilia,” alisisitiza Infantino.

Imani hiyo ya Rais wa FIFA kwa Tanzania inakuja wakati ambapo Ripoti ya Tathmini ya Hali ya Rushwa (Corruption Perception Index) iliyotolewa juzi Februari 21, 2018 na Taasisi ya Transparency International, ikionesha kuwa juhudi za Serikali ya Dkt. Magufuli katika kupambana na rushwa zimezidi kuzaa matunda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Taarifa hiyo iliyokusanya takwimu za mwaka mzima wa 2017 zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopanda kwa kiasi kikubwa katika kupambana na rushwa huku nyingi nyingi zikishuka au kubaki pale pale.

Wakati mwaka 2016 Tanzania ilikuwa ya 116 duniani, katika ripoti hiyo mpya Tanzania imepanda kwa nafasi 13 na kuwa ya 103 huku ikizizidi kwa mbali nchi kadhaa kubwa duniani katika utafiti huo uliohusisha mataifa 180.

Aidha, kwa eneo la Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa nchini ya pili baada ya Rwanda iliyoongoza kwa kupunguza rushwa ambapo katika alama za mtazamo wa rushwa Tanzania imepata 36, alama ambazo ni nyingi kuwahi kufikiwa na nchi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Tanzania, kufikia nafasi hiyo ya juu, imeonesha kufanikiwa katika kufanyiakazi mianya mingi ya rushwa, kwa mujibu wa vigezo vya rushwa kupungua katika taasisi mbalimbali za Serikali na kwa mujibu pia wa mtazamo wa wafanyabiashara na wawekezaji.

Ripoti hii inakuja ikiwa ni hivi karibuni tu Tanzania chini ya juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano ilitajwa na ripoti ya jarida la The Economist kuongoza katika EAC kwa utawala bora na demokrasia (Democracy Index).

Akizungumzia ripoti hii jijini Dar es Salaam jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema ripoti hiyo ni sehemu tu ya kuonesha kuwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini inafanikiwa.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail