Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Fahamu Kuhusu Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Faida Zake kwa Taifa.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (wa tatu kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Ndaki ya Sayansi na Elimu Kampasi ya Solomon Mahlangu Prof. Allen Malisa (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa kuhusu makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini yaliyopo Kampasi ya Solomon Mahlangu Mazibu mkoani Morogoro.

Na Anitha Jonas – WHUSM

Dar es Salaam.

Katika historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika,Tanzania baada ya kupata uhuru ndiyo nchi iliyosimamia kupatikana kwa uhuru katika baadhi ya nchi za bara hilo .

‘Tanzania haitakuwa huru hadi nchi zote za afrika zitakapokuwa huru,” alisema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hivyo aliungana na wanaharakati wenzake kama akina Samora Machel, Nelson Mandela,Kenneth Kaunda,Joaquim Chissano na wengine.

Hivyo katika kuenzi historia ya viongozi hawa namna walivyokomboa bara hili kutoka kwa wakoloni ambapo mwaka 2003 wazo la utekelezaji wa programu hii lilibuniwa na Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO lengo ikiwa ni kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Pamoja na hayo Tanzania ndiyo ilikuwa mwenyeji wa vikundi vingi vya wapigania uhuru na kutoa hifadhi ikiwemo Makao ya Kamati ya Ukombozi ya Bara la Afrika ambayo yapo Jijini Dar es Salaam ambayo iliratibu harakati zote za ukombozi.

Mratibu wa Programu hii ya Ukombozi wa Bara la Afrika kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Ingiaedi Mduma katika mahojiano alieleza kuwa Mwaka 2004 UNESCO iligharamia ujumbe wa Philip Mangula na wenzake ambao walikwenda Angola, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe kupata maoni ya wadau katika nchi hizo juu ya wazo hili.Ujumbe huo ulipokelewa vema na nchi zote tano na ikapendekezwa kwamba mradi huo ujumuishe nchi zote za kusini mwa Afrika na utekelezaji wake usimamiwe na Tanzania kwa sababu, Tanzania ilitambuliwa na inatambuliwa kuwa ni mdau mkubwa wa harakati hizo.

Ameeleza kuwa Lengo la programu hii ni kuanzisha kituo cha Kikanda cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambacho kwa mujibu wa makubaliano kitajengwa Jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambako Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika utatekelezewa, kuenziwa na kuoneshwa kwa ulimwengu.

Kituo hiki kitakuwa na Makumbusho, Maktaba, Nyaraka, Sehemu ya Watafiti na Ukumbi ambapo katika kituo hicho kutakuwa na uhifadhi kumbukumbu zote (picha, filamu, simulizi, barua, machapisho, maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru, nyimbo, sare, ambapo Tanzania ndio iliyopewa usimamizi wa zoezi hili .

Mwaka 2005 nchi 11 ziliungana na Tanzania kuwasilisha pendekezo la kuanzishwa kwa programu hiyo kwa UNESCO ambapo nchi hizo ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia, Swaziland, Zambia na Zimbabwe na baadae Mwezi Mei, 2010 Viongozi Wakuu wa vyama vya Siasa vilivyokuwa vya kupigania uhuru kusini mwa Afrika walikutana Jijini Dar es Salaam ili kuijadili Programu na hatimaye Mwezi Januari, 2011 Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika waliijadili Programu hii na kuipitisha.

Katika ziara ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Ally Possi aliagiza Idara ya Maendeleo ya Utamaduni na Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuhakikisha wanarasimisha Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.

Dkt.Possi alitoa agizo aliitaka ofisi hiyo kuandaa Mpango Mkakati pamoja na Maandiko ya kuomba ufadhili wa programu na mpango huo uwe unatoa dira ya namna Programu itakavyotekelezwa sababu ni ya kimataifa na siyo wa Tanzania pekee kwani kuna nchi za Afrika zinahusika na nchi za ulaya hivyo ni vyema kuwa na mpango madhubuti wa utekelezaji wa Programu hii.

Kaimu Katibu Mkuu Dkt.Possi alimtaka Mratibu wa Programu kuwa na Kanzi data ya Mawasiliano ya kila nchi iliyohusika katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kuanzia katika ngazi za Kitaifa mpaka Kimataifa na hii itarahisisha utekelezaji wa shughuli za programu na usambazaji wa taarifa.

Hata hivyo Bibi.Mduma aliezeza changamoto za utekelezaji wa programu hiyo na kusema kwa sasa kuna nchi ambazo tayari zimeonyesha nia ya kuchukua Programu hiyo ambazo ni Afrika Kusini Namibia na Angola, hivyo anaomba Serikali kusaidia kuwezesha mradi kwa kuwa una faida nyingi ikiwemo kuongeza ajira na fursa za utalii wa kihistoria.

Halikadhalika Programu hii ilizinduliwa rasmi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa Mlimani City- Dar es Salaam tarehe 08 Desemba, 2011 katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Pamoja na hayo katika eneo la Mabwepande kumepatikana ekari 25 ambapo kitajengwa Kituo cha Kikanda cha Programu, na katika ukusanyaji wa taarifa kwa watu waliyoshiriki Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika wazee 227 wamehojiwa kutoka maeneo mbalimbali na yamehifadhiwa kwa nja ya kidijitali.

Vilevile Jumla ya Maeneo 255 yanayohusu programu hiyo yamebainishwa hapa nchini na yanaandaliwa utaratibu wa kukarabatiwa ili kuhifadhi historia iliyomo katika maeneo hayo,baadhi ni Mazimbu,Dakawa,Kongwa,Lindi Farm 17,Kihesa Mgagao etc, Pia picha 4000 kuhusu historia ya ukombozi wa bara la Afrika zimekusanywa na kuhifadhiwa na Mafaili 900 yenye nyaraka mbalimbali zinazohusu programu hiyoa yamepatikana na kuhifadhiwa.

Pia Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) wameiboresha Studio ya (external service) iliyotumika kurusha matangazo wakati wa harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika imekarabatiwa na kwa sasa imefanywa kuwa Makumbusho ya historia ya Ukombozi wa Afrika.

Ukarabati wa Jengo lililotumiwa na Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika unaendelea na jengo moja kwasasa ndiyo linatumiwa kama ofisi za Sekretarieti ya Programu.

Katika kuhakikisha programu hii inaendeshwa vyema serikali imeamua kuanzisha mchakato wa kutunga Sheria ya kusimamia na kuhifadhi maeneo yenye historia ya ukombozi unaendelea kutekelezwa.

Na nimatarajio ya serikali kuwa baada ya kufanya mapitio na kubaini mapungufu yaliyopo katika Mitaala ya Shule za Sekondari kuongeza mtaala wa historia ya Ukombozi wa Afrika na kuhakikishwa inafundishwa kikamilifu katika shule za Sekondari hapa nchini na mapitio hayo yalifanywa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

205 thoughts on “Fahamu Kuhusu Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Faida Zake kwa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama