Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

DPP Afuta Kesi 59 Zaidi Jijini Mbeya

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na afisa wa magereza wakati wa ziara ya kikazi katika gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe Jijini Mbeya. Kushoto ni Mkuu wa Gereza la Tukuyu ASP. Samwel J. Kaluwa akiwatambulisha Staff wa gereza hilo mbele ya Waziri.

Na: Mwandishi Wetu

Katika mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) kwenye mikoa ya kusini, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga amefuta jumla ya kesi 59 katika mahakama za Mkoa wa Mbeya.

Mkurugenzi Biswalo ameyafanya hayo katika gereza la Ruanda mjini Mbeya na gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe alipoambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Mahiga ili kujionea hali halisi ya mazingira ya utoaji haki jinai katika magereza hayo na taasisi mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Polisi, Mahakama na Magereza yenyewe.

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) kulia akiwa na mwenyeji wake Kamishna Msaidizi wa Magereza Mkoa wa Mbeya Mathias Mkama (ACP) katikati, alipotembelea Gereza Kuu la Ruanda Mbeya 27 Nov. 2019. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ruanda Mbeya Vendeline Tesha wakati wa ziara ya kikazi jijini humo.

“Niliowafutia Kesi nendeni mkawe raia wema, msirudie makosa, badala yake mkawe mabalozi wema mtakaofanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Maguli katika kauli yake ya hapa kazi tu.”

Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) aliwataka wote waliofutiwa mashitaka kwenda kufurahi na familia zao huku wakimshukuru Mungu na kujutia makosa yaliyosababisha kushitakiwa kwao. Aidha, aliwaonya kutokurudia makosa hayo badala yake watumie nguvu na akili walizonazo kuzalisha mali kwa maendeleo yao na familia zao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na afisa wa magereza wakati wa ziara ya kikazi katika gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe Jijini Mbeya. Kushoto ni Mkuu wa Gereza la Tukuyu ASP. Samwel J. Kaluwa akiwatambulisha Staff wa gereza hilo mbele ya Waziri.

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) katikati akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mh. Chalya J. Nyangidu (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Biswalo Mganga (wa pili kulia), walipotembelea Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya leo tarehe 28 Nov. 2019 wakati wa ziara ya kikazi wilayani humo.

“Mliosamehewa leo nendeni mkafurahi na familia zenu sambamba na kuwa watu wema katika jamii inayowazunguka kwani ni matumaini yangu kuwa mmejifunza mengi na mmebadilika. Kuna watu hapa nikiwatizama misuli yao, walipaswa wakaitumie kufanya kazi na kuzalisha mali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla badala ya kuitumia kufanya uhalifu.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo 2002, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka anayo mamlaka ya kuwafutia mashitaka watuhumiwa wa makosa ya jinai katika magereza mbalimbali nchini. Mpaka sasa katika ziara hii ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria katika mikoa mitatu DPP Biswalo ameshafuta  jumla ya kesi 120 na bado ziara inaendelea katika Wilaya ya Kyela na baadae mkoa wa Njombe.

51 thoughts on “DPP Afuta Kesi 59 Zaidi Jijini Mbeya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *