Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt. Mpango Atoa Wito wa Kuondolewa kwa Upinzani Dhidi ya Ufadhili wa Kimataifa katika Utekelezaji wa Miradi ya Mageuzi katika Nchi za Afrika

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amehutubia Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaondelea Jijini New York nchini Marekani. Makamu wa Rais ametoa hotuba hiyo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Akitoa hotuba hiyo, Makamu wa Rais amesema Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla zinahitaji mabadiliko ya haki na ya utaratibu katika kufikia matumizi ya nishati mbadala kwa kuzingatia hali za maisha ya watu wa bara hilo wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa nishati hizo. Ametoa wito wa kuondolewa kwa upinzani dhidi ya ufadhili wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi katika nchi za Afrika ambayo inalenga kutumia rasilimali ikiwemo gesi kwa ajili ya nishati na matumizi mengine katika kufikia maendeleo.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba biashara ya hewa ukaa barani Afrika inapaswa kufanyika kwa uwazi na kuwanufaisha wananchi waliotunza mazingira na misitu inayozalisha hewa hiyo kwa matumizi ya dunia huku akiitaja Tanzania kama nchi iliowekeza zaidi katika uhifadhi wa misitu ambapo asilimia 30 ya eneo la ardhi ya taifa hilo imehifadhiwa.

Katika kudumisha amani na usalama, Makamu wa Rais amesema Tanzania siku zote inaamini kuwa diplomasia na meza za mazungumzo ndiyo chombo bora cha kutatua migogoro duniani. Amesema licha ya migogoro iliyopo duniani mataifa yanapaswa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake pamoja na ustawi wa watu. Aidha, ameongeza kwamba ni muhimu kushiriki katika kutafuta utatuzi wa migogoro kwa amani ili kukabiliana na athari zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko kubwa la bei za chakula na mafuta pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na viwanda duniani kote.

One thought on “Dkt. Mpango Atoa Wito wa Kuondolewa kwa Upinzani Dhidi ya Ufadhili wa Kimataifa katika Utekelezaji wa Miradi ya Mageuzi katika Nchi za Afrika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama