Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt. Madeni Afadhili Safari ya Kitalii kwa Walimbwende Miss Journalism World

Washiriki wa shindano la urembo la Miss Journalism World 2018 kutoka katika Mataifa 13 duniani wakiwa katika picha ya pamoja walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire leo tarehe 14 Disemba, 2018.

Na Fatuma S. Ibrahimu- Arusha Jiji

Katika kuhamasisha Utalii wa ndani na wa nje Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dr. Maulid Suleiman Madeni amedhamini Safari ya kitalii kwa Washiriki wa Mashindano ya urembo ya Miss Journalism World 2018 kutoka Mataifa 13 duniani kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Dkt. Madeni amesema kuwa utalii ni chanzo kimoja wapo kikubwa kinachochangia pato la Serikali na fedha za kigeni hivyo kila mtanzania kwa nafasi yake anapaswa kuzipa kipaumbele shughuli za kitalii na kuenzi tamaduni zetu.

“Naamini mashindano haya yanakwenda kuwa chachu ya kukuza utalii kwa nchi yetu hivyo nitumie fursa hii kuwaomba washiriki wote wakatangaze utalii wetu watakapofika katika nchi zao baada ya mashindano haya kuisha ” . Alisema Dkt. Madeni.

Miss Journalism World 2018 ni shindano jipya lililobuniwa kwa mara ya kwanza barani Afrika na kijana wa kitanzania Bw. Samwel Chazi na pia ni shindano la 7 kwa ukubwa Duniani katika tasnia ya urembo.

lengo kuu la mashindano haya ni kutangaza vivutio vya utalii kimataifa hasa Bonde la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Olduvai gorge pamoja na kutangaza utalii wa kitamaduni katika nchi yetu .

Kilele cha mashindano hayo kinatarajiwa kuwa kesho Tarehe 15/12/2O18 katika ukumbi wa Mount Meru Hotel ambapo atakayeibuka mshindi katika mashindano hayo atapata fursa ya Kuwa balozi wa kimataifa wa Mlima Kilimanjaro na atakuwa na majukumu ya kutangaza Mlima Kilimanjaro duniani kote.

25 thoughts on “Dkt. Madeni Afadhili Safari ya Kitalii kwa Walimbwende Miss Journalism World

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *