Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Dkt. Kalemani Aagiza Kituo cha Kupoza Umeme Nyakanazi Kikamilike Novemba

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati), akiangalia mchoro wa ramani ya kituo cha kupoza umeme kinachojengwa Nyakanazi, wilayani Biharamulo alipotembelea eneo hilo Februari 25, kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi husika.

Veronica Simba – Biharamulo

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme kilichopo Nyakanazi wilayani Biharamulo, kukamilisha kazi hiyo ifikapo Novemba mwaka huu badala ya Januari 2021, kama ilivyo kwenye mkataba.

Pia, ameagiza mradi mwingine unaotekelezwa sambamba na huo ukihusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi, ukamilike Januari 2021 badala ya Machi mwaka huo.

Alitoa maagizo hayo Februari 25 mwaka huu, alipotembelea eneo kinapojengwa kituo hicho cha kupoza umeme, ambacho ni sehemu ya mradi mkubwa wa kusafirisha na kusambaza umeme unaotekelezwa na serikali kutoka Kigoma – Nyakanazi – Geita – Bulyanhulu kwa gharama ya shilingi bilioni 93.27 za Tanzania.

Akifafanua sababu za kutoa maelekezo hayo, Dkt Kalemani alisema ni kutokana na umuhimu wa kukamilika kwa mradi huo mapema ambao unatarajiwa kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji umeme ambazo wamekuwa wakizipata wakazi wa maeneo husika.

Sambamba na hilo, pia Waziri alisema ni kutokana na imani aliyonayo kwa Mkandarasi husika (M/s Kalpataru Power Transmission Limited – India) kutokana na historia ya kazi alizotekeleza awali hapa nchini.

“Hii kampuni inayojenga mradi wa kusafirisha umeme, ndiyo ilijenga mradi wa Makambako – Songea na walikamilisha kazi mwezi mmoja kabla ya mkataba kuisha kama nilivyowaelekeza. Kutokana na uzoefu walionao, naamini hata kazi hii wana uwezo wa kuikamilisha kabla ya muda.”

Akieleza zaidi kuhusu mradi husika, Waziri Kalemani alisema ni kati ya miradi mikubwa ya vielelezo katika masuala ya kuzalisha, kufua, kusafirisha pamoja na kusambaza umeme ambayo inatekelezwa na serikali.

Kuhusu utekelezaji wake, Waziri alieleza kuwa umegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ikihusisha mikoa ya Iringa – Mbeya mpaka Tunduma (kilovoti 400), ambapo utekelezaji wake umeshaanza.

Alisema sehemu ya pili ni kutoka Sumbawanga kupitia Mpanda hadi Kigoma ambapo kwa upande wa Kigoma (Kidahwe) kutajengwa Kituo kikubwa cha kupoza umeme.

“Sehemu ya tatu ya mradi ndiyo hii kutoka Kigoma kuja hapa Nyakanazi umbali wa kilomita 280 na kutoka hapa mpaka Geita umbali wa kilomita 144, pamoja na kutoka Geita hadi Bulyanhulu, umbali wa kilomita 57.”

Aidha, aliongeza kuwa, mradi huo pia utaungana na mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo wenye megawati 27 kwa kila nchi husika (Tanzania, Rwanda na Burundi). Alisema, itajengwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi hadi Rusumo, umbali wa kilomita 96.

Vilevile, Waziri Kalemani alieleza kuwa, Mradi huo utasambazia umeme vijiji takribani 31 ambako unatekelezwa kutoka Nyakanazi kupitia Bwanga (Chato) na maeneo mbalimbali kwenda Katoro/Buseresere hadi Bulyahulu na kuongeza kuwa wananchi wataunganishwa kwa gharama ya umeme vijijini (REA), ambayo ni shilingi 27,000 tu.

Alitumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza katika maeneo yote  unakotekelezwa mradi akiwahakikishia kuwa kutakuwa na umeme wa uhakika, unaotabirika na baadaye wenye gharama nafuu.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Biharamulo Venance Martin, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya, alipongeza mikakati ya kusambaza umeme inayotekelezwa na serikali huku akitolea mfano wa mradi huo ambao alisema mbali na kuwanufaisha wananchi, utawezesha kukuza uchumi wa viwanda katika ukanda husika.

Msimamizi wa Mradi huo (Geita-Nyakanazi), Mhandisi Elias Makunga, alisema maagizo ya Waziri yanatekelezeka na alimhakikishia kuwa atasimamia utekelezaji wake ipasavyo.

Katika ziara hiyo Waziri alifuatana na viongozi na wataalamu mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Dauson Kamaka, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Raymond Seya,  na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale.

400 thoughts on “Dkt. Kalemani Aagiza Kituo cha Kupoza Umeme Nyakanazi Kikamilike Novemba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama