Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Daraja la Kigongo-Busisi Kukuza Biashara Kati ya Tanzania na Mataifa Jirani

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza kuhusu umuhimu wa ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi wilayani Misungwi,  Jijini Mwanza utakaogharimu Bilioni 699.2 likiwa ni daraja la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki na la sita Barani Afrika

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi Jijini mwanza  utakaogharimu Bilioni  699.2 utachangia kukuza biashara na mataifa jirani.

Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi  la ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita 3.2 ambalo litakuwa la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki na kati na la sita kwa urefu katika bara la Afrika, Rais Magufuli amesema kuwa mradi huo utakapokamilika utawezesha  ukuaji wa sekta za kilimo, biashara, viwanda, uchukuzi na ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Misungwi,Sengerema na Taifa kwa ujumla.

“Nikiwa uwanja wa CCM Kirumba wakati naomba kura niliahidi kujenga daraja hili, lakini wapo waliosema haiwezekani,niliona hili tukiamua sisi kama watanzania tutaweza”;Alisisitza Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiweka jiwe la msingi katika mradi wa  ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi wilayani Misungwi , Jijini Mwanza utakaogharimu Bilioni 699.2 likiwa ni daraja la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki  na la sita Barani Afrika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Rais Dkt Magufuli amesema mkandarasi wa mradi huo anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa ambao ni miezi arobaini na nane kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo ikiwemo za malipo ya awali.

Akizungumzia kuhusu fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo,  Rais Magufuli amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 3.145 zitatumika kuwalipa fidia ili kupisha  ujenzi wa  mradi huo wa kihistoria utakaochangia katika  kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.

“Mradi huu unatekelezwa na  Serikali ya Tanzania kwa fedha za watanzania,hizi ni kodi zenu, Tanzania sisi ni matajiri” Alisisitiza Dkt. Magufuli

Ujenzi wa daraja hilo unatajwa kuzalisha ajira kwa wananchi  ambapo Rais Magufuli amewataka wananchi watakaopata ajira katika mradi huo kuwa waadilifu na wazalendo kwa kujiepusha na vitendo vya wizi wa vifaa vitakavyotumika katika ujenzi wa mradi huo.

Sehemu ya wananchi walioshiriki katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa daraja la Kigongo- Busisi  wilayani Misungwi, Jijini Mwanza utakaogharimu Bilioni 699.2 likiwa ni daraja la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki  na la sita Barani Afrika.

“ Ndugu zangu Watanzania niko pamoja nanyi, mimi ni mtumishi wenu na nitaendelea kuwatumikia kadiri mtakavyoona inafaa,miradi hii ni matokeo ya ushirikiano wetu sisi kwa pamoja katika kuhakikisha tunailetea nchi yetu maendeleo” Alisisitiza Rais Magufuli.

Daraja hilo litajengwa na Kampuni ya China Railway 15th Bureau Group Corporation na  China Civil Engineering   Construction Cooperation (CCECC) ambapo mkataba wa ujenzi ulisainiwa mwezi Julai 29, 2019.

Aidha , Rais Magufuli  amewataka wananchi kuendelea kulipa kodi ili kuwezesha ujenzi wa miundo mbinu kama madaraja , na utoaji wa huduma muhimu za kijamii kama elimu bure, ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 552,ujenzi wa reli ya kisasa (SGR),bwawa la  kufua  umeme la Mwalimu Nyerere na miradi mingine ya maendeleo.

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano mhandisi Isack Kamwelwe akieleza faida za ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi wilayani Misungwi Jijini Mwanza

Kwa  upande wake, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa  kwa sasa wastani wa masaa mawili na nusu yanatumika kuvuka kwa kutumia kivuko ambapo baada ya daraja kukamilika wananchi watatumia wastani wa dakika 4 kuvuka katika daraja hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa  mradi wa daraja la Kigongo- Busisi Wilayani Misungwi , Jijini Mwanza utakaogharimu Bilioni 699.2 likiwa ni daraja la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki  na la sita Barani Afrika.

Aliongeza kuwa daraja hilo litatumika kwa zaidi ya miaka 100 baada ya kukamilika hivyo litawawezesha wananchi kuongeza kasi ya uzalishaji na ufanyaji wa biashara kwa kuwa kiungo muhimu kati ya nchi yetu na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, na Congo.

Naye mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa zaidi ya magari 1600 huvushwa katika eneo la Kamanga na Busisi kila siku hivyo kuna kila sababu ya kuwa na daraja hilo.

Alisema kuwa usanifu wa daraja hilo ulikamilika mwaka 2018 na hivyo kuanza kwa taratibu za ujenzi ikiwemo kutangaza zabuni na hatimaye kupatikana kwa mkandarasi wa daraja hilo.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika leo Disemba 7 , 2019 Jijini Mwanza katika Wilaya ya Misungwi na kuhudhuriwa na wananchi, viongozi wa Serikali wakiwemo Mawaziri, wakuu wa mikoa ya kanda ya ziwa.

Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale akizungumza wakati uzinduzi wa ujenzi wa  mradi wa daraja la Kigongo- Busisi wilayani Misungwi , Jijini Mwanza utakaogharimu Bilioni 699.2 likiwa ni daraja la kwanza kwa urefu katika nchi za Afrika Mashariki  na la sita Barani Afrika.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa daraja la Gigongo – Busisi wilyani Misungwi Jijini Mwanza

(Picha zote na Idara ya Habari- MAELEZO)

172 thoughts on “Daraja la Kigongo-Busisi Kukuza Biashara Kati ya Tanzania na Mataifa Jirani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama