Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

China Yaipatia Tanzania Msaada wa Bilioni 146, Kujenga Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Usafirishaji

Na Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania imetiliana saini na Serikali ya China mkataba wa msaada wa kiasi cha Shilingi Bilioni 146.47. Mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James na Balozi wa China nchini Wang Ke  Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu alisema kuwa fedha hizo ni msaada na siyo mkopo na zitatumika katika miradi miwili ya miundombinu. Mradi wa kwanza ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) ambacho kitajengwa Mabibo Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62 sawa na takriban Shilingi bilioni 138.3.

Mradi wa pili ni kwa ajili ya kusaidia upembuzi yakinifu na upembuzi sanifu wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambapo kiasi cha Sh. bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili hiyo.

Bw. Doto James alisema kwa sasa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa umeanza kwa awamu mbili ambazo moja ni kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, na kuanzia Morogoro hadi Makutopora-Dodoma, upembuzi yakinifu utakaofanywa na Serikali ya China ni kwa maeneo mengine ya ujenzi wa Reli hiyo kuanzia Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Kuanzia Kaliua hadi Kigoma.

“China imetusaidia miradi mingi ikiwemo mradi wa maji Chalinze, Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Taifa, Mradi wa teknolojia za Kilimo mkoani Morogoro, Kituo cha upasuaji wa moyo na mafunzo, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Nyerere pamoja na misaada ya dawa na vifaa tiba” alieleza Bw. James

Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, Alisema kuwa China inategemea kuona kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha maendeleo na kuisaidia Tanzania kupata maendeleo haraka.

Aidha alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawasaidia Watanzania na kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Balozi Wang Ke, amesema Pia Serikali ya China na Tanzania zinaendelea majadiliano kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, na kuongeza kuwa majadiliano hayo yatakapokamilika nchi yake itasaidia ujenzi wa bandari hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) Prof. Zacharia Mganilwa ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kusema kuwa msaada huo utaisaidia chuo hicho kuweza kutoa wataalamu wa kutosha kuweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo sekta ya anga.

Amebainisha kuwa Chuo hicho Kikuu kitatoa mafunzo kwenye fani muhimu na zinazohitajika ikiwemo ufundi wa reli, masuala ya anga na sekta nyingine mtambuka kwa kutoa wataalamu waliobobea watakao changia kufanikisha azma ya Serikali ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania-TRC, Bw. Focus Msasani ameeleza kuwa msaada huo wa shilingi bilioni 3.22, utasaidia kuipunguzi serikali gharama ilizokuwa izitumie kwa kazi hiyo kenye mradi mkubwa wa kihistoria wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa.

44 thoughts on “China Yaipatia Tanzania Msaada wa Bilioni 146, Kujenga Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Usafirishaji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *