Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Iringa
Serikali imefikia uwamuzi wake wa kutekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo Iringa ili kusaidia shughuli za biashara na utalii kwa lengo la kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Akizungumza leo wakati akiweka jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uwanja huo utakaogharimu takribani shilingi bilioni 63.7 utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa zitakazotua, ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira 150 wakati wa ujenzi wake.
“Imani yetu kuwa baada ya miezi 18 hadi 20 Iringa sasa zitatua ndege kubwa zenye idadi ya kuanzia abiria 70 na kwa vile nyie ni wazalishaji wa mazao kama vile chai sasa itakuwa rahisi kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya nchi”. Amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa uwanja huo utafungua mkoa huo kwa fursa za utalii sambamba na kuendeleza maeneo ya utalii.
Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wa Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati amesema kuwa ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege utafungua fursa za kiuchumi kupitia utalii.