Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Majaliwa Akutana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Qatar

Rais Dkt. Mwinyi Azungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji na wa Nchini Ethiopia

Majaliwa Afungua Mkutano Mkuu wa CAF

Barabara ya Njombe – Makete Kufungua Fursa za Utalii, Neema kwa Wananchi

Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Makete

Barabara ya Njombe – Maronga – Makete yenye urefu wa kilomita 107.4 ambayo thamani ya ujenzi wake ni Shilingi bilioni 243.4 inatajwa kufungua fursa za uchumi na utalii wa mkoa wa Njombe.

“Barabara hii itasaidia kufungua utalii pamoja na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, ombi langu kwenu ni kuilinda kwa vile kumekuwa na tabia ya watu kuchimba michanga kwenye barabara” Amesisitiza Rais Samia.

Akizungumza leo wilayani Makete mara baada ya kuzindua barabara hiyo, Rais Samia ameeleza namna ambavyo mkoa huo utanufaika na kukuza uchumi wake.

Rais Samia ameongeza kuwa Wilaya hiyo ya Makete itabadilika na hivyo wategemee wageni wengi watakaotembelea na kuwekeza.

Aidha, Afisa Tarafa wa Matamba, Bw. Bujo Mwakatobe ameeleza kuwa awali wananchi wa Makete walisafiri kwa tabu kwenda maeneo mbalimbali na kutopata huduma muhimu kwa wakati.

“Tulikuwa na basi moja tu linalosafiri kutoka Iringa, Mafinga, Makambako na Njombe kuleta abiria Ikonda na Makete na hakukuwa na usafiri mwingine. Pia, wakati wa masika tulikwama sana njiani hasa katika milima ya Mang’oto kwa sababu ya utelezi” Amesema Mwakatobe.

FIFA Kuendelea Kuisaidia Tanzania, Yaridhishwa na Utendaji wa Rais Samia

Na John Mapepele

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino  amesema  FIFA itaendelea kuisaidia Tanzania kutokana na kuridhishwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Michezo.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo Agosti 10, 2022 mara baada ya kupokelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Mohamed Mchengerwa katika kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro amesisitiza kuwa FIFA itaendelea kuisaidia Tanzania.

Akiongozana na wachezaji mahiri wa zamani waliopata kucheza katika makombe ya dunia na mwamuzi Corina amesema amefurahishwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tanzania.

“Tayari FIFA imeshatoa msaada wa ujenzi wa viwanja changamani Dar na Tanga lakini wako tayari kwa ajili ya kuongeza vituo katika kanda nyingine”, amefafanua Mhe. Mchengerwa

Aidha, Mhe. Mchengerwa amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa ambayo imesaidia Tanzania kupiga hatua duniani katika michezo.

Mhe. Mchengerwa amepokea viongozi mbalimbali wa juu kwenye mashirikisho ya Soka duniani na kufanya vikao vya kuendeleza michezo ambao leo wanahudhuria mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) jijini Arusha.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ametumia fursa hiyo kuendelea kuimarisha mahusiano na mashirikiano na nchi mbalimbali ambazo tayari ziliahidi kuendeleza mashirikiano katika sekta za michezo, Sanaa na Utamaduni.

Mkutano huu wa kihistoria unatarajiwa kuhudhuria na zaidi ya watu mia tano na waandishi wa habari zaidi ya mia moja huku ikitarajiwa kuangaliwa na zaidi ya watu bilioni moja.

Tayari viongozi wakuu wa mashirikisho yote ya Soka kutoka mabara yote wamewasili na Waziri Mkuu, Mhe. Kassimu Majaliwa anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan.

TET Kufanya Mapitio Makubwa ya Sita ya Mitaala Tangu Uhuru

Na Zaituni Hussein MAELEZO

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imesema tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961, imefanya mapitio makubwa sita ya mitaala ya elimu lengo likiwa ni kuwajengea wahitimu ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kutumia vema fursa zinazopatikana nchini, hususani kwa kujiajiri, kuajiriwa na kumudu maisha yao ya kila siku pale wanapohitimu mafunzo.

Kati ya mapitio hayo, matano tayari yalishafanyika mpaka kufikia mwaka 2014, na sasa kazi ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya pitio la sita inaendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Aneth Komba amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam kuhusu uetekeleza wa shughuli za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na mwelekeo wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

“Mapitio ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 kwa lengo la kuondoa mitaala ya kibaguzi ya wakoloni, mapitio ya pili yakafanyika mwaka 1979 kwa lengo la kuhimiza matumizi ya nadharia, na kupitia mapitio hayo kulianzishwa masomo ya michepuo, mapitio ya tatu yakafanyika mwaka 1997 ambayo lengo lake lilikuwa  kukidhi matakwa ya sera ya mwaka 1995 pamoja na kuingiza mapendekezo ya tume ya makweta ya mwaka 1982, mapitio ya nne yalifanyika mwaka 2005 ambayo yalipelekea kuanzishwa kwa mtaala ambao ulilenga kujenga umahiri, na mapitio ya tano yalifanyika mwaka 2014 ambayo yalikuwa na lengo la kuingiza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia elimu ya awali.” amesema Dkt. Komba.   

Serikali Kuwekeza Katika Makazi ya Kuwatunza Wazee

Na WMMJW Morogroro

Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kuwekeza katika Makazi ya Wazee nchini ili kuwa na miradi mbalimbali itakayozalisha mazao na kuchangia katika mapato ya Serikali.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani hapa mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa na Makazi ya Wazee katika Mikoa ya Singida, Manyara, Kilimanjaro na Morogoro.

Alisema kuwa ziara hiyo imefanyika kimkakati ikiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wengine wa Wizara, imelenga kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi 14 yenye Wazee 271 yanayosimamiwa na Wizara ili kuweka mikakati na mbinu mbalimbali zitakazosaidia makazi hayo kuwa na huduma bora na kuwekeza nguvu katika miradi mbalimbali ya kilimo, mifugo na uzalishaji mali katika makazi hayo.

Akizungumza kuhusu uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika Makazi hayo nchini amesema mfano Makazi ya Wazee Fungafunga yenye ekari 10 yanaweza kutumika katika shughuli za kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa kuku na miradi mingine ya kimkakati.

“Makazi haya ndio tunatoa huduma kwa wazee wasiojiweza na wasio na ndugu ila hamkatazwi kuzalisha, hapa nilipo katika Makazi haya ya Wazee Fungafunga Afisa Mfawidhi wa hapa amekuwa mbunifu na kutumia eneo kulima mbomboga zinazosaidia wazee na pia kuongeza kipato”, alisema Dkt. Chaula.

Aidha, ametoa rai kwa jamii kuwajibika katika malezi ya wazee kwani sehemu salama na ya kwanza ya wazee ni katika familia zao ili waweze kupata huduma bora na uangalizi mzuri kutoka kwa ndugu na familia zao.

Pia alisisitiza wananchi kujitokeza kuhesabiwa tarehe 23/08/2022 ili kusaidia kupata takwimu sahihi hasa za wazee nchini kwa ajili ya kusaidia kuweka mikakati stahiki ya kuwahudumia wazee katika utoaji wa huduma hasa za Afya na huduma nyingine muhumu kwa wazee.

ev eşyası depolama