Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

BRELA Yaweka Mazingira Bora ya Biashara Kupitia Mfumo wa Taarifa za Biashara

Mkurugenzi wa Idara ya Leseni kutoka Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Andrew Mkapa

Na Mwandishi Wetu

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni BRELA imebainisha wazi kuwa imeweka mazingira mazuri na rafiki kwa Wafanyabiashara wanaotoa bidhaa nje ya nchi, wanaoingiza au kupitisha mazao na bidhaa mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Leseni kutoka Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Andrew Mkapa katika mahojiano yaliyofanyika katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1.

“Mfumo huu ni utekelezaji wa mikakati kadhaa ya Taifa ya kurahisisha na kuboresha mazingira ya biashara, ili wafanyabiashara waweze kutumia gharama nafuu, kutumia muda mfupi lakini pia kupunguza Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo zinaonekana si za lazima sana na ni vikwazo katika ufanyaji biashara”, Amesema Bw. Mkapa.

Akieleza kuhusu lengo la kuwa na Mfumo wa Utoaji Taarifa za Biashara Bw. Mkapa amesema kuwa lengo ni kumsaidia mfanyabiashara aweze kuwa na taarifa za kutosha kabla ya kuanza kufanya utaratibu wa ama kuuza bidhaa nje ya nchi, kupitisha au kuingiza nchini.

Mfumo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha ufanyaji biashara hapa nchini lakini pia utarahisisha upatikanaji wa taarifa hizi kwa wafanyabiashara kutoka nchi nyingine ambao wangependa kufanya biashara hapa nchini.

Aidha Bw. Mkapa amefafanua kwamba kwenye Dirisha la Taifa la biashara (the Tanzania National Business Portal) Mfanyabiashara anaweza kufahamu taratibu za usafirishaji nje ya nchi, uingizaji nchini na upitishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nchini.

“Mtu anapoingia kwenye Mfumo huo , kule anaweza kuona taarifa za hatua kwa hatua ambazo mfanyabiashara anapaswa kuzipitia na kuzifuata ili kupata leseni na vibali vinavyohitajika toka Taasisi mbalimbali ili aweze kusafirisha nje ya nchi, kuingiza na au kupitisha nchini bidhaa na mazao mbalimbali . Kwa mfano Tanzania tumeshaweka taarifa hizo zinazohusiana na usafirishaji nje ya nchi wa mazao makuu ya kimkakati kama vile, Kahawa, Karafuu, Korosho, chai na mengine. Zinazohusiana na uingizaji nchini wa Madawa, Vipodozi, Vifaa tiba, Magari na vinginevyo.

Sasa mfanyabiashara akiingia kwenye huo mfumo anaweza kuona ni hatua gani na ngapi anapaswa kupitia, vibali au leseni gani anatakiwa awe navyo ili aweze ama kusafirisha nje ya nchi, kuingiza ndani au kupitisha nchini bidhaa hizo” alisema Bw. Mkapa.

Katika hatua ya mwisho Bw. Mkapa ametoa wito kwa wafanyabiashara kutembelea Taarifa hizo kupitia ama tovuti ya BRELA yani www.brela.go.tz kisha kubonyeza katika mahali palipo andikwa ‘Trade Information Module’ ambapo mfumo utampeleka katika dirisha la taifa la biashara, au moja kwa moja kwenye Dirisha la biashara kwa anwani pepe ya www.business.go.tz.

188 thoughts on “BRELA Yaweka Mazingira Bora ya Biashara Kupitia Mfumo wa Taarifa za Biashara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama