Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Bodi Mpya ya Mfuko wa PSSSF Yazinduliwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisistiza umuhimu wa Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kusimamia rasilimali fedha kwa kutekeleza miradi ya kimkakati katika mfuko huo wakati akizindua Bodi hiyo leo Jijini Dodoma.

Frank Mvungi- MAELEZO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  amezindua Bodi  mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kuiagiza Bodi hiyo kutekeleza miradi ya kimkakati ili lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo litimie.

Akizungumza leo Jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi huo amesema kuwa wanachama wana matarajio makubwa na utendaji wa Bodi hiyo, hivyo jukumu lake ni kuhakikisha kuwa inafanya tathmini ya miradi yote iliyokuwa inatekelezwa na mifuko iliyounganishwa ili kuona namna bora ya kuiendeleza.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mhandisi Mussa Iyombe akisisitiza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuzindua Bodi mpya ya Mfuko huo leo Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi wa mfuko huo wakati wa hafla ya kuzindua Bodi mpya ya mfuko huo ambapo tayari umeshafungua Ofisi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Ofisi moja Tanzania Visiwani ikiwa ni moja ya hatua za kuwahudumia wanachama wake katika mikoa yote hapa nchini.

“Jukumu lenu kama Bodi ni kuhakikisha kuwa miradi kama ule wa Kiwanda cha kuzalisha viatu Karanga inaendelezwa kwa maslahi ya nchi yetu, sambamba na miradi yote ya kimkakati iliyopo ni vyema mkaharakisha mchakato wa kuifanya ianze mara moja kwa kuwa matarajio ya Serikali ni kuona mfuko huo unakuwa imara, endelevu na unatoa huduma bora ya Hifadhi ya Jamii”; Alisisitiza Mhe. Mhagama.

Akifafanua amesema kuwa sekta ya hifadhi ya Jamii imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kuwekeza shilingi Trilioni 11.79 katika vitega uchumi ikiwemo miundombinu, daraja la Kigamboni, Ujenzi wa Hospitali, Vifaa tiba na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, ushirikiano, nidhamu, uadilifu na weledi wa hali ya juu, uongozi wenu ndiyo utakaowezesha PSSSF kukidhi matarajio ya wanachama”; Alisisitiza Mhagama.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe leo Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) mara baada ya kuzindua Bodi hiyo leo Jijini Dodoma. kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo Mhandisi Mussa Iyombe na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga.

Akizungumzia uwajibikaji kwa menejimenti na wajumbe wa Bodi, Waziri Mhagama amewaasa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za matumizi ya fedha na rasilimali za mfuko huo ili kuleta tija kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Aliongeza kuwa jukumu jingine la mfuko huo ni kuboresha mafao ya wanachama ili yaendane na hali ya maisha na mabadiliko ya kiuchumi na pia kulipa mafao hayo kwa wakati ili kuondoa malalamiko ya wanachama.

Pia aliwaasa watumishi wote wa mfuko huo kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na sheria taratibu na kanuni za utumishi kwa kuwahudumia wanachama wote bila kubagua kama ilivyo azma ya kuanzishwa kwa mfuko huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi vitendea kazi Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga wakati wa hafla ya kuzindua Bodi mpya ya mfuko huo leo Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa SSRA Dkt. Irene Isaka akisalimiana na wajumbe wa Bodi mpya ya PSSSF kabla ya kuzinduliwa kwa Bodi hiyo leo Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo Mhandisi Mussa Iyombe amesema kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi,uadilifu, uaminifu, taratibu, Sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo.

Aliongeza kuwa Bodi hiyo imejipanga vizuri kwa kushirikiana na menejimenti kutekeleza majukumu yote na kuhakikisha kuwa mfuko huo unatimiza azma ya kuanzishwa kwake kwa kulipa mafao kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga amesema kuwa mfuko huo umeshafungua Ofisi katika mikoa yote Tanzania Bara na Ofisi moja Tanzania Visiwani.

Sehemu ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) uliofanyika leo Jijini Dodoma.(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO)

Pia alimhakikishia Waziri Mhagama kuwa Menejimenti itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa taratibu , sheria na kanuni .

Mfuko huo tayari umeshahakiki mali zake zote na utahakikisha kuwa unalipa madeni yote ya wanachama kwa wakati.

Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa PSSSF umefanyika leo  tarehe 14 Septemba 2018 Jijini Dodoma ikiwa ni hatua mojawapo kwa kuanza rasmi kwa mfuko huo unaotokana na kuunganishwa kwa mifuko ya GEPF, PSPF, LAPF na PPF.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail