Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

JKCI Yaibuka Mshindi wa Kwanza kwa Utoaji wa Huduma za Afya na Matumizi ya Teknolojia Katika Tiba

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa maonesho hayo mara baada ya kukabidhiwa kombe la ushindi wa kwanza kwa utoaji wa huduma za afya na matumizi ya Teknolojia katika tiba kwenye maonesho ya 43 ya Kibiashara ya kimataifa ya Dar es Salaam.

Na Mwandishi Maalum

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeibuka mshindi wa kwanza kwa utoaji wa huduma za afya na matumizi ya Teknolojia  katika tiba  kwenye  maonesho ya 43 ya Kibiashara ya  kimataifa ya Dar es Salaam.

Kombe hilo la ushindi ilitolewa jana na Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua maonesho hayo yanayofanyika katika uwanja wa Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa  jijini Dar es Salaam.

Tangu kuanza kwa maonyesho hayo tarehe 28/06/2019 katika banda la Taasisi hiyo jumla ya wananchi  660 wamefanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo ambapo asilimia 60 wamegundulika kuwa na uzito mkubwa asilimia 40 shinikizo la juu la damu na asilimia 4 wana kiwango kikubwa cha sukari katika damu (hyperglycemia).

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 43 ya Kibiashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika uwanja wa Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa.
Picha na JKCI

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizo Maria Samlongo ambaye ni  Afisa Lishe wa Taasisi hiyo alisema wananchi wengi hawapati mlo ulio kamili na wenye virutubisho vya kutosha hivyo basi wameona watoe elimu ya lishe ili wananchi wafahamu jinsi ya kuandaa chakula bora katika jamii zao .

Maria alisema baada ya kufanyiwa vipimo  watu wengi walionekana  uwiano wao wa urefu na uzito haulingani hivyo kupelekea wengi wao kuwa na uzito mkubwa zaidi.

“Watu wengi nilioonana nao wanaamini viywaji vyenye sukari kama soda, juisi na pombe haviongezi uzito kitu ambacho siyo kweli nimewashauri kuachana na vinywaji hivyo na kupendelea zaidi kutumia matunda kama yalivyo ,” alisema Maria.

Mtaalamu huyo wa lishe aliendelea kusema kuna baadhi ya watu  wanaamini wakiacha kula mlo wa  asubuhi na mchana watapungua uzito kitu ambacho siyo sahihi kwasababu ikifika jioni wanashikwa na  njaa kali na kuwafanya kula kiasi kikubwa cha chakula kuliko uhitaji wakati wa usiku hali inayowapelekea ongezeko kubwa la uzito.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi kombe la ushindi wa kwanza kwa utoaji wa huduma za afya na matumizi ya Teknolojia katika tiba Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 43 ya Kibiashara ya kimataifa ya Dar es Salaam.

Wanachotakiwa kufanya ni kugawa milo yao vizuri kuanzia asubuhi hadi jioni  kitu cha kuzingatia ni mlo wa jioni kuwa mwepesi hasa kula mboga za majani, matunda na vyakula vya protini kidogo.

Kwa upande wake  Gasper Minja aliyefika katika banda hilo kwa ajili ya kupima afya aliishukuru Taasisi hiyo kwa kutoa huduma za ushauri na upimaji  wa magonjwa ya moyo bila malipo yoyote.

“Ninawaomba wananchi wenzangu watumie fursa hii na  wajitokeze kwa wingi kupima afya zao ili wajue kama wanamatatizo ya moyo au la na kama watakutwa na matatizo hayo watapewa dawa za kutumia na rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo”, alisisitiza Minja.

Katika banda hilo wanatoa bila malipo huduma za upimaji wa urefu na uzito, kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu (BP), vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  (Echocardiograph) na mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography -ECG ), elimu ya ushauri wa lishe bora, dawa kwa wagonjwa wanaokutwa na matatizo ya moyo   na kutoa rufaa ya moja kwa moja wa watu watakaokutwa na matatizo ya moyo ili waende kutibiwa katika Taasisi hiyo.

211 thoughts on “JKCI Yaibuka Mshindi wa Kwanza kwa Utoaji wa Huduma za Afya na Matumizi ya Teknolojia Katika Tiba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama