Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Watoa Huduma wa NHIF Acheni Udanganyifu- Gambo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akifungua Mkutano wa Wadau wa NHIF, Mkoa wa Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

SERIKALI imewataka Watoa Huduma waliosajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuachana na udanganyifu katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake kwa kuwa jambo hilo ni kurudisha nyuma maendeleo ya Mfuko ambao ni nguzo kubwa katika utoaji wa huduma za matibabu.

Akifungua kikao cha Wadau wa NHIF, Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo amesema kuwa udanganyifu katika huduma ni adui mkubwa wa uimarishaji wa chombo hicho ambacho kwa sasa kinahudumia wananchi wengi na wanaohitaji huduma ambazo gharama zake ni kubwa.

“Niwaombe sana wadau wote hususan wanachama wa Mfuko, ni vyema kila mmoja kwenye nafasi yake akawa mlinzi wa huduma anazopata ili Mfuko huu uwe imara zaidi na uendelee kuhudumia wananchi, mimi binafsi nikiri tu kwamba bila ya kuwa na kadi ya NHIF nisingeweza kumudu gharama za matibabu, nimemuuguza Mama yangu na alihitaji matibabu yenye gharama kubwa lakini kwa kuwa na kadi ya NHIF ilinisaidia kwa kiasi kikubwa sana, hivyo ili Mfuko huu uendelee kuwepo ni lazima sote kwa pamoja tuulinde,” alisema Bw. Gambo.

Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda akitoa salaam za Bodi kwa wadau wa Mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji ya Mfuko kwa wadau wake.

Kwa upande wa watoa huduma aliwataka kuwa wakweli na kuwa wazalendo katika vipimo na dawa wanazowaandikia wanachama ili Mfuko uweze kulipa gharama halisi  na sio kulipa fedha ambazo huduma zake hazikuwa sahihi.

“Lengo la Serikali inayoongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli  ni kuona kila wilaya nchini inakuwa na Hospitali na  kata inakuwa na kituo cha Afya na Kijiji kinakuwa na Zahanati ili upatikanaji wa huduma za matibabu uwe rahisi na bora zaidi na kwa kutumia mfumo wa Bima ya Afya wananchi watakuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote,” alisema Bw. Gambo.

 

Meneja wa NHIF Mkoa wa Arusha Bw. Isaya Shekifu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mkoa.

Wadau wa NHIF wakifuatilia taarifa mbalimbali za Mfuko.

Sehemu ya Wadau wa Mfuko wakiwa kwenye mkutano huo.

Sehemu ya Wadau wakifuatilia uwasilishwaji wa Mada.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi  ya NHIF, Bi. Anne Makinda amesema kuwa Mfuko umejipanga kuhakikisha mpaka ifikapo mwakani zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania iwe inahudumiwa na Mfuko na kwa upande wa huduma, Mfuko umejipanga kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma katika maeneo yao na kwa ubora unaotakiwa.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi wa NHIF, Bw.Bernad Konga amebainisha kuwepo kwa mifumo mizuri ya udhibiti wa udanganyifu ambayo mpaka sasa imeleta matokeo makubwa kwa kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 4 ambazo zingeweza kulipwa kutokana na vitendo vya udanganyifu vya baadhi ya watoa huduma.

66 thoughts on “Watoa Huduma wa NHIF Acheni Udanganyifu- Gambo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama