Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mashirika yasiyo ya kiserikali yapewa siku 30 kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha na miradi kwa mwaka 2016 na 2017

 

TARIFA KWA UMMA

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YAPEWA SIKU 30 KUWASILISHA TAARIFA ZA MATUMIZI YA FEDHA NA MIRADI KWA MWAKA 2016 NA 2017

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi duniani zinazozingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Misingi ya Utawala bora pamoja na mambo mengine inasisitiza uzingatiaji wa masuala ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa kila siku jambo ambalo Serikali yetu imekuwa ikilihimiza na kulitekeleza ipasavyo.

Tunapenda kufahamisha umma kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwa wabia muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa.  Kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikisajili, kuratibu na kufuatilia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na Taifa letu.

Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Mwaka 2001 inasisitiza misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Na. 24 ya mwaka 2002 ikisomeka pamoja na Marekebisho yake ya mwaka 2005 katika Kifungu cha 29 (a) na (b), Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana wajibu wa kuwasilisha taarifa za kazi na fedha kila mwaka kwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwa umma. Hata hivyo, takwa hili la kisheria limekuwa halizingatiwi ipasavyo.

Vile vile, Kanuni za Maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Code of Conduct, GN. No. 363, 2008) ambazo zimeundwa kwa mujibu wa kifungu Namba 27 zinasisitiza uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi, usimamizi wa masuala ya fedha na utawala. Hali kadhalika, wanufaika wa miradi hiyo, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanamofanyia kazi na vyombo vya habari wanayo haki pia ya kupata taarifa za shughuli zao. Aidha, NGOs pia zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sera na vipaumbele vya nchi katika maeneo wanayofanyia kazi.

Hata hivyo, baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini yamekuwa hayazingatii wajibu wao wa kisheria kama nilivyoeleza hapo juu. Hali hii imekuwa ikizusha malalamiko na manunguniko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wabia wetu wa maendeleo wanaotoa fedha zao kuchangia katika juhudi za nchi na wananchi kujiletea maendeleo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali inaagiza yafuatayo:

  1. Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali kuwasilisha kwa Msajili wa NGOs Taarifa za fedha (Audited financial statements) za miaka miwili iliyopita (2016 na 2017), wakati huo wanajiandaa kutoa taarifa ya mwaka 2018 mwishoni mwa mwaka huu.
  2. Mashirika yote kuwasilisha taarifa za vyanzo vya fedha, matumizi yake na miradi iliyotekelezwa na inayotarajia kutekelezwa kwa kipindi husika.
  • Kuwasilisha mikataba/ hati za makubaliano ya ufadhili wao kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa.
  1. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yahakikishe kuwa miradi wanayoitekeleza inazingitia vipaumbele, mipango na mikakati ya Serikali katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya ili kutoa mchango katika kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya jamii na Taifa.
  2. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yahakikishe kuwa kabla ya kutekeleza miradi yao ni sharti kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambaye yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sanjari; na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupata kibali ili kufanikisha jukumu la uratibu, ushirikishwaji na ufuatiliaji wa kazi za NGOs katika ngazi mbalimbali.
  3. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa (INGOs) yazingatie ushiriki wa wananchi na Mashirika ya ndani katika miradi wanayoitekeleza kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za NGOs hapa nchini.
  • Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa chini ya Sheria nyingine, mfano Sheria ya Makampuni Na.12 ya mwaka 2002; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini; Registration Insolvency and trusteeship Agency (RITA), Sheria ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Sura ya 337 ya Mwaka 2002  yanapaswa kuomba kupata cheti cha ukubalifu kwa mujibu wa kifungu 11 cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005. Aidha, kufanya kazi pasipo kusajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kosa kwa mujibu wa Sheria.
  • Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatume taarifa zao za fedha na miradi za kila mwaka kupitia barua pepe ifuatayo dngo@communitydevelopment.go.tz, au kuleta taarifa zao moja kwa moja kwenye ofisi ya Msajili wa NGOs.

Maagizo niliyotaja yanatekelezwa ndani ya kipindi cha siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya agizo hili na baada ya kipindi husika kukoma, Serikali itaanza kufuatilia na kuchukua hatua stahiki za kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta usajili kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatakayoshindwa kutekeleza agizo hili.

IMETOLEWA NA:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, DODOMA

28/9/2018

 

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Wadau Watakiwa Kuendelea Kufanya Tathmini ya Elimu Nchini

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR –TAMISEMI), Selemani Jafo akifunga Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.

Na Jacquiline Mrisho

Wadau wa Elimu wametakiwa kuendelea kufanya tathmini ya elimu kwa kujadili mafanikio na changamoto za sekta hiyo ili kuboresha na kukuza elimu nchini.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Elimu.

Read more


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Serikali yatoa siku 12 kukamilisha ujenzi wa miundombinu wezeshi mradi wa umeme wa mto rufiji

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mbele) akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali wa Serikali kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Na Veronica Simba – Rufiji

Serikali imeziagiza Taasisi zote zenye jukumu la kujenga miundombinu wezeshi kwa ajili ya Mradi wa Kufua Umeme wa Megawati 2100 kutokana na maporomoko ya Mto Rufiji, kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ifikapo Oktoba 10 mwaka huu.

Maelekezo hayo yalitolewa jana, Septemba 28 na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga, katika ziara ya kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu hiyo itakayowezesha kuanza ujenzi wa Mradi husika.

“Tumeridhishwa na kazi zinazofanyika ili kumwezesha Mkandarasi wa Mradi kuanza kazi yake, lakini tunataka kazi zote za ujenzi wa miundombinu wezeshi zikamilike ndani ya siku 12 kuanzia leo,” alisema.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia-mwenye miwani), akikagua zoezi la utandazaji mabomba ya kupitisha umeme chini ya ardhi, katika eneo lenye viwanja vya ndege; akiwa katika ziara kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Akifafanua zaidi, Waziri Kalemani alisema ni matarajio ya Serikali kwamba kufikia tarehe iliyotolewa, kazi zote zitakuwa zimekabidhiwa serikalini ili kumruhusu Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga Mradi husika, kuanza rasmi ujenzi.

Kufuatia maelekezo hayo, Waziri Kalemani pia aliwaagiza wakandarasi na mafundi wanaojenga miundombinu wezeshi ya Mradi huo, kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi kwa wakati.

Kalemani alimshukuru Naibu Waziri Hasunga kwa kutoa maagizo ya kuhakikisha wanaotekeleza kazi husika hawazuiliwi kufanya kazi usiku kwa kisingizio cha suala la usalama; na kuagiza askari wa wanyamapori waongezwe ili kuimarisha ulinzi utakaowawezesha wahusika kufanya kazi kama walivyoagizwa.

Awali, akielezea kazi za ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi, zinazoendelea kutekelezwa; Waziri Kalemani alisema ni pamoja na kuufikisha umeme katika eneo la ujenzi wa Mradi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto), akiwasalimia mafundi waliokuwa wakijenga Daraja, akiwa katika ziara kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

“Tayari wameshafikisha umeme kutoka Msamvu, wamekamilisha ujenzi wa vituo viwili vya kupooza umeme vilivyopo Dakawa na Pangawe na wanaendelea kutandaza mabomba yatakayopitisha umeme chini ya ardhi katika maeneo ya viwanja vya ndege viwili. Aidha, kazi ya kuweka nguzo za zege na za miti inaendelea.”

Waziri alitaja kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa barabara zote kuelekea kwenye Mradi ikiwemo inayotoka Ubena Zomozi, yenye umbali wa kilomita 178.4 pamoja na ya Kibiti – Lingungu yenye umbali wa kilomita 210. Alisema kazi hii iko katika hatua nzuri.

Nyingine, ni ujenzi wa mitambo ya maji pamoja na matenki makubwa mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita 22,500 hivyo kuweza kuhudumia wafanyakazi takribani 11,000; kazi ambayo imekamilika.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu-kulia) akizungumza na mafundi (kushoto), wanaojenga barabara eneo la Rufiji, alipokuwa katika ziara kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Aidha, Waziri alisema kazi nyingine ni ukarabati wa majengo ya nyumba za wafanyakazi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano kwa njia za simu, ambazo pia zinaendelea na ziko katika hatua nzuri.

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wenyewe wa kuzalisha umeme kutokana na maporomoko ya maji ya Mto Rufiji; Waziri Kalemani alisema utahusisha kazi kuu tatu, ambazo ni pamoja na kujenga Mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 2100.

Vilevile, alisema kuwa kazi nyingine kubwa itahusisha ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kupitia njia mbili; kutoka eneo la Mradi hadi Chalinze, umbali wa kilomita 178 wenye kilovoti 400 na kutoka eneo la Mradi hadi Kibiti kupitia Lungungu, umbali wa kilomita 210 na wenye msongo wa kilovoti 400 pia.

 

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu-kushoto) akitoa maelekezo kwa taasisi mbalimbali za Serikali zinazosimamia ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge. Waziri alikuwa katika ziara kukagua kazi hiyo Septemba 28, 2018. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga.

Aidha, alieleza kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa Bwawa lenye eneo la kilomita za mraba 914 lenye uwezo wa kuhifadhi maji kiasi cha mita za ujazo takribani bilioni 35.

Dkt Kalemani aliishukuru na kuipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ndani ili kutekeleza Mradi huo mkubwa ambapo alisema mpango wa utekelezaji wake ulipangwa ufanyike tangu miaka ya 1972 mpaka 1980 kwa awamu. “Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwakuwa sasa tutaujenga kwa mkupuo.”

Ziara hiyo pia iliwahusisha wabunge wa majimbo ya Rufiji (Omari Mchengelwa), Kibiti (Ally Ungando) na Mafia (Mbaraka Dau), ambao wote walipongeza jitihada za Serikali katika kuhakikisha Mradi huo unatekelezwa.

Msimamizi wa Miradi ya Ujenzi wa Barabara Mkoa wa Pwani, kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Zuhura Amani (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kulia) kuhusu hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Barabara, wakati wa ziara ya Waziri kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018. Wengine kutoka kushoto ni Mbunge wa Rufiji Omari Mchengelwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga.

Baadhi ya mafundi wanaojenga barabara katika eneo la Rufiji, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), aliposimama kuzungumza nao akiwa katika ziara kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Taswira ya sehemu ya Mto Rufiji kama ilivyokuwa ikionekana wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Kazi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya wafanyakazi ikiendelea kama taswira hii ilivyochukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Taswira ya Mtaro uliochimbwa ili kupitisha nyaya za umeme katika eneo la viwanja vya ndege rufiji, kama ilivyonaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

Kazi ya ujenzi wa daraja ikiendelea kama taswira hii ilivyochukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, Septemba 28, 2018.

( Picha na  Veronica Simba- Wizara ya Nishati)


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Serikali Kuendelea Kuwezesha Wananchi Wanyonge Kumiliki Ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akihutubia washiriki wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma ambapo alizindua taarifa ya utafiti huo .

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO Dodoma.

Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha wananchi hasa waishio vijijini wanapata haki za msingi za umiliki wa ardhi na makazi nchini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mheshimiwa Angelina Mabula wakati wa uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania  mwaka 2017/2018.

“Tunafahamu Watanzania walio wengi na ambao ni masikini wanaishi vijijini na wizara yangu inadhamana ya kusimamia eneo hili, kama Waziri mwenye dhamana nitajitahidi kadri ya uwezo wangu na kuendelea kushirikiana na viongozi wenzangu na wananchi wote kuhakikisha nyaraka rasmi za umiliki ardhi na makazi zinatolewa” ameongeza Dkt. Mabula.

PIX2. Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma ambapo alitoa taarifa fupi ya utafiti huo .

Aidha, akizungumzia kuhusu utoaji wa hati, Dkt. Mabula amesema kuwa kwa sasa utoaji wa hati umeongezeka kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Kanda nane nchini.

“Jumla ya Hati 25,463 zimeandaliwa katika Halmashauri mbalimbali nchini, Hati 17,680 zimewasilishwa ofisi za Kanda kwa ajili ya usajili na Hati 9,739 zimeshakamilika” amefafanua Dkt. Mabula.

hata hivyo Dkt. Mabula amesema kuwa, kwa mwaka 2018/2019 Wizara yake imejipanga kuandaa hati za hakimiliki za kimila 120,000 mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 30 na mpango kina wa vijiji na kupima viwanja 20,000 ikiwa ni kumuwezesha mwananchi kuwa na uhakika na salama ya miliki yake na kuepusha mgogoro.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akikata utepe kuzinduzi wa matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa utafiti huo umelenga kutoa viashiria mbalimbali kuhusu rasilimali ardhi, nyumba na makazi nchini na kutumika katika kufuatilia malengo yaliyopo katika Mpango kazi wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ijayo, Malengo endelevu ya Maendeleo na Afrika Ajenda 2063.

“Utafiti huu ulifanyika Tanzania Bara na Zanzibar na sampuli ilichaguliwa kwa utaalamu na ilitumika kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na kuendelea” ameongeza Dkt. Chuwa.

Utafiti wa Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2016/2017 na wa pili mwaka 2017/2018 na watatu mwaka 2018/2019 unaendelea na ukusanyaji wa taarifa za kitakwimu ambao matokeo yake yatazinduliwa mwaka 2019

Sehemu ya washiriki wa hafla uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma, Utafiti huo umezinduliwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akimkabidhi Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Kati Bw. Ezekiel Kitilya matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akionesha matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo.

Mwakilishi wa Shirika la Global Land Allience ya Marekani inayojishughulisha na masuala ya haki miliki ya Ardhi na Makazi Dkt. David Ameyaur akizungumzia faida za matokeo ya utafiti wa haki na usalama wa umiliki wa rasilimali ardhi na makazi Tanzania wa mwaka 2017/2018 leo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo.

(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma)


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Tanzania Yapewa Tuzo ya Kimataifa ya Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza

Na Fatma Salum

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepata Tuzo ya Kimataifa ya Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs) kwenye mkutano wa Viongozi wa Juu wa Umoja wa Mataifa (United Nations High Level Meeting on NCDs) unaoendelea mjini New York nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, Waziri Ummy Mwalimu alipokea tuzo hiyo jana tarehe 27 Septemba, 2018 kutoka kwa Kikosi Kazi Maalum cha Umoja wa Mataifa cha Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (UN Interagency Task Force on the Prevention & Control of NCDs- UNIATF).

Taarifa hiyo inaeleza kuwa tuzo hiyo imetokana na juhudi za Wizara ya Afya za kupambana dhidi ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs), hususan kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Aidha Waziri Ummy amelishukuru Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza la Tanzania (TANCDA) ambao waliandika andiko la kuitambulisha dunia kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na dunia ikaona umuhimu wa juhudi hizo.

“Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD) ndiyo yanayoongoza duniani kwa sasa kwa kusababisha ulemavu na vifo vingi.  Nchini Tanzania asilimia 34 ya vifo vilivyorekodiwa hospitali mwaka 2017 vimesababishwa na magonjwa haya, isitoshe kupambana na NCD ni miongoni mwa mikakakati ya Mpango wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (SDG) ya kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030,” alisema Waziri Ummy.

Pia alibainisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na TANCDA pamoja na wadau wengine inaamini kwamba afya za wananchi zitaendelea kuboreshwa kwa kuweka mikakati madhubuti, kuzingatia utekelezaji wa sera mbalimbali za afya na kuhakikisha Watanzania wanapata elimu sahihi ya kujikinga na kuyadhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa sugu au ya muda mrefu, ambayo hayawezi kuambukizwa kwa maana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Magonjwa hayo yapo mengi kama vile Kisukari, Saratani, Shinikizo la Damu na Mishipa ya Fahamu, Magonjwa Sugu ya Mfumo wa Hewa, Magonjwa Sugu ya Figo, Macho na Meno, Selimundu (sikoseli) na mengineyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 9 duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo ambayo imetolewa kwa mara ya kwanza katika ngazi ya kiserikali.

 

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Serikali Yanunua Mashine Mpya za Kisasa za Tiba ya Mionzi

Na Fatma Salum
Serikali kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imenunua mashine mbili mpya za kisasa zenye thamani ya shilingi bilioni 9.56 kwa ajili ya kutoa tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani hapa nchini.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumzia kuhusu utekelezaji wa wizara hiyo katika kipindi cha Tunatekeleza kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC.
“Mashine hizi za kisasa zimeboresha utoaji wa tiba ya mionzi hasa kupunguza muda kutoka wiki 6 hadi wiki 2 kwa mgonjwa mpya wa Saratani ambaye anapaswa kuanza tiba hiyo,” alisema Ummy. Read more


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Makamu wa Rais Azindua Kikosi Kazi cha Kutatua Changamoto za Viumbe Wageni/Vamizi

Makamu wa Rai, Mama Samia Suluhu Hassani akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, kuzindua kikosi cha Kutatua changamoto za viumbe wageni/vamizi, hafla iliyofanyika leo Ijumaa, Septemba, 28. 2018. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso, kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba.

Read more


FacebooktwittermailFacebooktwittermail

Dkt. Ndungulile Atoa Mwezi Mmoja Chuo cha Ustawi kutatua changamoto Zake

Na. Immaculate Makilika

Naibu waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto  Dkt. Faustine Ndugulile  amekitaka Chuo cha Ustawi wa Jamii kutatua changamoto zake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Hayo yamesemwa  leo Chuoni hapo alipokuwa akizungumza na menejimenti, wafanyakazi pamoja na viongozi wa  Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, ambapo pamoja na mambo mengine alisomewa taarifa ya maendeleo ya taasisi na mipango ya baadae.

Read more


FacebooktwittermailFacebooktwittermail