Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wafanyakazi nchini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na Viongozi wanawake kutoka vyama vya wafanyakazi Mkoani Morogoro kuhusu kuwahimiza wafanyakazi kuchangamkia fursa za shughuli za kimaendeleo zilizopo nchini.

Na Mwandishi Wetu.

Serikali imewahimiza wafanyakazi  kote nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi ili kujiletea maendeleo  na kuchangia katika ujenzi wa Taifa.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alipokuwa akiongea na viongozi wanawake wa Mkoa wa Morogoro kutoka vyama vya wafanyakazi ikiwemo TAMIKO, CWT, TUICO, TALGU, TULGE, TPAWU na CHODAWU.

Waziri Mhagama amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wafanyakazi kwa kuhakikisha wanashirikishwa kwenye dhana ya uchumi wa viwanda. Lengo likiwa ni kuwawezesha wafanyakazi wanashiriki katika mipango ya maendeleo ya taifa kwa kufuata kanuni na taratibu ya dhana nzima ya uchumi wa viwanda.

Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamuhoke akielezea jambo wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alipokutana kwa lengo la kuzungumza na Viongozi Wanawake kutoka kwenye Vyama vya Wafanyakazi Mkoani Morogoro.

“Mnao uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na mkawa chachu ya maendeleo ya viwanda kwenye uchumi wa taifa letu, kwa kuweza kutoa ajira, vilevile kuwasaidia ninyi kupiga hatua za maendeleo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na weledi kwa kutumia sera ya viwanda” ameeleza Waziri Mhagama.

Aidha, aliongeza kuwa, Sera ya uchumi wa viwanda iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni jambo jema linalolenga kuboresha maisha ya watanzania.

“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza azma ya kujenga Tanzania ya viwanda, hivyo nitafurahi sana kama Waziri mwenye dhamana ya wafanyakazi kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wafanyakazi.” Alisema Mhagama.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’i Issa akizungumzia Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa viongozi kutoka vyama vya wafanyakazi walipokutana Mkoani Morogoro.

Alitoa rai kwa viongozi wanawake kuhakikisha wanaratibu na kusambaza ujumbe huu wenye habari njema kwa wanawake nchi nzima waliopo kwenye sekta ya ajira kuchangamkia fursa hii kwa kuanzisha miradi mbalimbali itakayowawezesha kuwakomboa kiuchumi.

Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa alifafanua juu ya sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo imelenga kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji ili kuwawezesha wananchi.

“Wanawake wanamchango mkubwa katika jamii, hivyo ni vyema mkatumia vizuri fursa hii kwa kuanzisha shughuli zitakazo wasaidia kuongeza vyanzo vya mapato na kuleta maendeleo kupitia ushirika wenu na hivyo kuwarahisishia kupata mikopo ya kuendeleza shughuli hizo.” Alisema Bi. Issa

Baadhi ya viongozi kutoka kwenye Vyama mbalimbali vya Wafanyakazi wakisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alipokutana nao kuzungumzia ushirikishwaji wa wafanyakazi kwenye dhana ya uchumi wa viwanda.

Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhoke aliungamkono rai iliyotolewa na Waziri kwa kuhaidi suala hili watalifikisha na kulifanyia kazi kwenye shirikisho la vyama vya wafanyakazi.

Mmoja wa washiriki kutoka (TALGU) Bi. Elizabeth Ngaiza aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hii wafanyakazi kuweza kuanzisha shughuli za kimaendeleo zitakazowaongezea kipato ambacho kitawasaidia kuendesha majukumu ya kifamilia tofauti na hapo awali walikuwa wakitegemea mshahara ambao ulikuwa hautoshi kutekeeza baadhi ya majukumu.

Katika mkutano huo Waziri Mhagama aliambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wawakilishi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya NMB na SIDO ambao waliweza kuelezea fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotolewa katika mashirika hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza jambo na Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamuhoke kuhusu kuwawezesha wafanyakazi kushiriki katika mipango ya maendeleo ya taifa. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake (TAMIKO) Bi. Veneranda Seif.

Meneja Kanda ya Kati kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. George Nyamrunda akielezea kuhusu mikopo ya kilimo inayotolewa na benki ya maendeleo ya kilimo.

Meneja Kanda ya Kati kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. George Nyamrunda akielezea kuhusu mikopo ya kilimo inayotolewa na benki ya maendeleo ya kilimo.

(Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)

Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa wingi wa gesi – Waziri Kalemani

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018. Pamoja naye ni viongozi mbalimbali wa Serikali, TPDC na Kampuni ya Dangote.

Na Veronica Simba – Mtwara

Imeelezwa kuwa Tanzania ina kiwango kizuri cha gesi asilia kinachofikia futi za ujazo trilioni 57.54, ambacho kinaipa nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki kwa wingi wa gesi kwa sasa.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, Septemba 27 mwaka huu, mkoani Mtwara wakati akizindua awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.

Waziri Kalemani alisema kwamba, kati ya futi hizo za ujazo trilioni 57.54; Serikali imepanga kutumia futi za ujazo trilioni 8.8 kwa ajili ya matumizi ya viwandani, kikiwemo Kiwanda cha Dangote.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018. Kulia ni Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Jani mstaafu Josephat Mackanja na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda.

Alisema kuwa, kazi ya Serikali ni kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali hiyo adhimu ili iwe na tija kwa uchumi wa nchi.

“Mpaka sasa ziko kampuni 39 nchi nzima zinazotumia gesi; Dangote inakuwa ya 40. Tunaendelea kuhamasisha kampuni zaidi zitumie gesi katika kuendesha shughuli zao za uzalishaji ili pamoja na mambo mengine, wapunguze gharama za uzalishaji, waongeze tija na hivyo kuendelea kulipa kodi zote stahiki za Serikali,” alifafanua Waziri.

Akifafanua zaidi, Dkt Kalemani alisema kuwa, kwa kupunguza gharama za uzalishaji, wawekezaji wanakuwa na uwezo wa kuongeza ajira kwa watanzania hivyo kukuza kipato chao na hata uchumi wa nchi kutokana na kulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.

Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni inayojishughulisha na uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya gesi hapa nchini; ambayo ni Kampuni-tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Baltazari Mrosso, akiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (Meza Kuu – katikati), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018.

Akizungumzia zaidi kuhusu tija ambayo Serikali itapata kupitia mpango huo wa matumizi ya gesi katika Kiwanda cha Dangote, Waziri Kalemani alisema kuwa, punguzo la asilimia 40 la gharama za uzalishaji ambalo wawekezaji hao watapata, litawawezesha kulipa kodi stahiki kwa Serikali, kuwepo na uwezekano wa kupunguza bei ya saruji, kuongeza ajira na faida nyingine mbalimbali.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa Waziri; Mtendaji wake Mkuu hapa nchini, Jagat Ralthee alisema kuwa, kabla ya matumizi ya umeme wa gesi, Kampuni ilikuwa ikitumia lita zinazofikia 160,000 za mafuta ya dizeli kwa siku, ambazo zinagharimu takribani shilingi milioni 315,000. Kwa matumizi ya gesi, watapunguza asilimia 40 ya gharama hizo.

Naye Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni inayojishughulisha na uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya gesi hapa nchini; ambayo ni Kampuni-tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Baltazari Mrosso, alimweleza Waziri Kalemani kuwa, Mradi husika utazalisha megawati 45 za umeme kutokana na gesi, ambao utatumika katika shughuli za uzalishaji wa Kiwanda cha Dangote pekee.

Msimamizi wa Usambazaji wa Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwanaidi Rashid (kushoto), akimweleza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) na Ujumbe wake, namna gesi inavyopokelewa na kutolewa katika Toleo Namba 1 la gesi katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mtwara, muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Kalemani aliwaeleza miradi mingine mikubwa ambayo Serikali inapanga kutekeleza katika Mkoa huo, ambayo ni pamoja na Mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawati 300 unaotarajiwa kuanza Mei, 2019.

“Tutausafirisha umeme huo kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, umbali wa kilomita 502 ili kuuingiza kwenye Gridi ya Taifa.”

Vilevile, alitaja Mradi mwingine utakaoanza kutekelezwa mwakani, kuwa ni wa kuzalisha umeme wa gesi wenye megawati 330 na kuusafirisha kutoka Somanga Fungu  hadi Kinyerezi, umbali wa kilomita 98.2 na kuuingiza kwenye Gridi ya Taifa pia.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mtwara, muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.

Aidha, Waziri alisema Serikali inapanga pia kuanzisha Mradi mwingine wa Kinyerezi III mwezi Julai, 2019 wa kuzalisha umeme wa megawati 600 utakaotekelezwa kwa awamu mbili. Alisema awamu ya kwanza (Kinyerezi III (1) itazalisha umeme wa megawati 300, na ile ya pili (Kinyerezi III (2) itazalisha megawati nyingine 300.

“Kwahiyo, ni matumaini yetu kuwa, ndani ya miaka miwili hadi mitatu ijayo, tutaongeza kwenye Gridi ya Taifa, takribani megawati 1,012 za umeme kutokana na rasilimali ya gesi,” alisema.

Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilianza kazi hapa nchini Agosti, 2015 ambapo kina uwezo wa kuzalisha Tani 2500 za Saruji kwa siku, sawa na Tani 75,000 kwa mwezi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akijadiliana jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote hapa nchini, Jagat Ralthee (kulia), wakati akikagua mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.

Sehemu ya umati wa wananchi wa Kijiji cha Hiari mkoani Mtwara, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Septemba 27, 2018.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kiwanda cha Saruji cha Dangote, baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Hiari, Mtwara baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Septemba 27, 2018. Kijiji cha Hiari ndipo kilipo Kiwanda hicho.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa mkoani Mtwara, baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.

(Picha zote na Veronica Simba)

DAWASA yaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam Kupata Maji ya Uhakika

Na ; Georgina Misama

Mamlaka ya Maji  Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) imenza kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali kuimarisha huduma ya maji safi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuweka Bomba kubwa  zaidi ya lililopo sasa.

Kwa mujibu wa Mamlaka hiyo lengo la upanuzi wa miundo mbinu ya kufikisha maji Bandarini hapo ni kuwezesha meli zote za abiria na mizigo zinazotia nanga kupata huduma hiyo kulingana na mahitaji na kwa wakati wote.

“Kazi hii ya kupanua miundo mbinu ya maji yanayotumika katika Bandari yetu ni maagizo ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa alilolitoa wakati wa ziara yake iliyolenga kutambua wateja wakubwa wa maji Jijini Dar es Salaam”. Inasisitiza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Taarifa hiyo imefafanua kuwa kuimarishwa kwa miundo mbinu ya kupeleka maji katika Bandari hiyo kutasaidia kuongeza tija kwa watumiaji wa huduma hiyo katika Bandari hiyo.

Kwa mujibu wa DAWASA dhamira yake ni kuwafikia wananchi wote katika maeneo yao kwa kufikisha huduma ya maji safi na salama kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisistiza utoaji wa huduma bora kwa wananchi wote.

DAWASA imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa kutekleza miradi ya kimkakati katika Jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani kwa maslahi ya wanachi  wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.

TAARIFA KWA UMMA


TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaratibu maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani, yatakayofanyika Jumatatu ya tarehe 01 Oktoba, 2018 ambapo wadau watashiriki ikiwa ni pamoja na wananchi.  Maadhimisho hayo yatatanguliwa na Salamu za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William V. Lukuvi (MB) zitakazorushwa na Luninga ya TBC zikipeleka ujumbe huo kwa wananchi.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia makazi duniania (UN Habitat) hutoa kaulimbiu itakayoongoza tafakari ya kila mwaka. Mwaka huu, 2018 maadhimisho hayo yataongozwa na Kaulimbiu isemayo: “Managing Municipal Solid Waste”; Tafsiri ya kauli mbiu hiyo ni “Udhibiti wa takangumu kwenye Miji yetu”: Kauli mbiu hii inatuelekeza tutafakari namna tunavyoweza kuelimisha Umma kuhusu namna tunavyoweza kukusanya na kutupa taka ngumu kwa usahihi na kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na mrundikano wa taka ngumu ambao ni changamoto ya miji mingi duniani.

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kutoa mwongozo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutafakari kwa pamoja masuala yanayohusu miji, majiji na haki za msingi za wakazi katika miji yetu na kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo ili kushirikishana mbinu na namna bora ya kutayarisha mikakati endelevu ya kupambana nazo.

Uzalishaji wa taka ngumu kutoka kwa wakazi wa mijini hukua kila siku na kusababisha mamlaka za upangaji na usimamizi wa miji kuingia gharama kubwa kuzikusanya, kuziondosha, na kuziteketeza. Aidha, ukusanyaji na uteketezaji wa taka ngumu uliozoeleka wa kutupa katika majalala ya taka (Dumping Sites)  na kuzichoma ama kuzifukia kumeleta athari nyingi za kiafya kwa wananchi waishio maeneo jirani zinazotokana na uchafuzi wa hewa (Air Pollution)  na uharibifu wa mazingira pia. Aidha, changamoto ya uchafuzi wa vyanzo vya maji umesababisha pia mlipuko wa magonjwa  yanayoenezwa kwa njia ya maji (Water borne Diseases) mfano kipindupindu (Cholera), kuhara / kuhara damu (dysentery) hususan wakati wa mvua.

Matokeo ya maadhimisho hayo ni matarajio ya kubuni njia mbadala na nyepesi za ukusaji na utupaji wa taka ngumu ambao utapunguza: gharama kubwa za ukusanyaji, usafirishaji na uteketezaji zinazoingiwa na mamlaka za miji; wenye kupunguza athari za kiafya na mazingira kwa wakazi wa mijini na wenye manufaa kwa jamii kama vile uzalishaji wa nishati na matumizi mengine ya kujirudia.

Tanzania inaungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani kwa kufanya tafakari ikiongozwa na Kaulimbiu iliyotolewa na kushirikisha wadau muhimu ili kujadili namna bora ya kushughulikia changamoto ya uzalishaji na utupaji wa takangumu katika miji yetu. Mabadiliko ya tabia kwa kila mwananchi katika kuzalisha na kutupa taka ni muhimu na yanaweza kupunguza gharama kubwa zinazoingiwa na mamlaka za miji kuondosha takangumu na kupunguza athari zinazotokana na uwepo wa mrindikano wa taka hizo.

Baadhi ya nchi na miji duniani hutumia njia mbadala ya kutenganisha aina ya taka ngumu kuanzia zinapozalishwa ili kuweza kuzichakata na kurudia katika matumizi mengine (Recycling) ama kuzitumia kuzalisha nishati (Source of energy), ama kuzalisha vifaa na bidhaa zinazoweza kutumika katika ujenzi, bustani kama mbolea n.k.

Uthibiti wa taka ngumu kuanzia zinapozalishwa, zinaposafirishwa na zinavyoangamizwa kunaweza kubadili kabisa taswira ya miji yetu endapo mbinu za kisasa zitatumika kuzichakata na kutumika kama fursa badala ya kuwa kero kwa wakazi wa mijini. Baadhi ya watu wamejipatia kipato kutokana na taka ngumu (ukusanyaji chupa za plastiki, vyuma chakavu n.k.) huku miji yetu ikiendelea kupunguziwa kero ya taka hizo.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kila Jumatatu ya kwanza ya Mwezi Oktoba. Chimbuko la maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani ni Azimio Namba 40/202 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 1985 na kuanza kuadhimishwa rasmi mwaka 1986. Mwaka huu maadhimisho hayo ya 33 yatafanyika Jijini Nairobi, nchini Kenya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

DAWASA kuwaunganisha wananchi 40,000 na huduma ya maji

Mafundi wakiendelea na kazi ya uchimbaji mtaro tayari kwa kulazwa mabomba ili kuwaunganisha wateja elfu 40,000 katika eneo la Salasala Jijini Dar es Salaaam.

Sehemu ya mabomba yanayotumika katika mradi huo wa kuwaunganisha wateja elfu 40,000 na huduma ya maji.

Na; Mwandishi wetu

 Jumla ya wateja wapya 40,000 wanatarajiwa kuunghanishiwa huduma  ya maji katika eneo la Salasala Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya hatua za Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mamlaka hiyo, Dhamira yake ni kuhakikisha kuwa  kazi hiyo inafanywa kwa weledi  na kuzingatia maslahi ya wananchi na ustawi wa Jamii.

Awamu ya kwanza itaanza kwa kuwaunganisha wananchi wanaoishi eneo la Sasasala Jijini Dar es Salaam kwani eneo hilo tayari lina mtandao na maji kutoka mtambo wa ruvu chini. Read more

Mapinduzi Makubwa Sekta ya Madini Yazidi Kuongeza Mapato

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Serikali katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita leo.

Na Mwandishi wetu, Geita.

Mageuzi makubwa katika sekta ya madini nchini yameifanya sekta hiyo kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kutoka bilioni 194.6 ilizopanga kukusanya mwaka 2017/18 hadi kufikia shilingi bilioni 301.6 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 55.

Hayo yameelezwa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi mkoani Geita wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Serikali.

Dkt. Abbasi ameeleza kuwa ongezeko hilo la mapato katika sekta ya madini limechagizwa na mabadiliko  katika sheria za madini, kujengwa kwa ukuta wa Mirerani na kuzuia kwa usafirishaji wa mabaki (kaboni) ya dhahabu nje ya mkoa yanapochimbwa madini. Read more