Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tume Kuweka Bei Elekezi ya Madini

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma

Serikali itapanga bei elekezi ya madini ili kuwawezesha wachimbaji wadogo na wakubwa kunufaika na kazi yao.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Nchini, Prof. Idris Kikula akiwa katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji wa madini Mkoani Dodoma.

Imebainika kuwa wachimbaji wa madini ya jasi (Gypsum) wanalipwa fedha kidogo kwa tani moja kiasi kwamba gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko bei wanayopewa.

Mchimbaji wa madini katika kijiji cha Manda, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, Saimon Msanjila amesema kuwa gharama ya uchimbaji wa madini ya jasi tani moja na kuisafirisha hadi Dar es Salaam inafikia Shilingi 65,000 na bei anayopewa ni Shilingi 77,000.

“Kwa kweli bei tunayopewa na wawekezaji wa viwanda vya saruji ni ndogo sana, hivyo tunaiomba Serikali itusaidie katika hilo”, alisema Msanjila.

Katika ziara hiyo wanakijiji cha Manzase, Wilayani Chamwino walisimamisha msafara wa Tume ya Madini ili kueleze dukuduku lao kwa uwekezaji unaoendelea katika eneo lao.

Hoja zao zilikuwa ni kumtaka mwekezaji atimize ahadi yake ya kuwajengea daraja na kukarabati shule ya msingi.

Baada ya kuwasikiliza, Prof. Kikula alimtaka mwekezaji huyo kufika kwenye ofisi ya madini kesho yake kwa hatua zaidi.

Wanakijiji wa Manzase na Manda kwa pamoja waliishukuru Tume kwa kuwajali na kubaini changamoto walizonazo ili kuzipatia ufumbuzi.

Aidha, Prof. Kikula amemtaka mwekezaji  wa mawe ya nakishi kutangaza bidhaa zake kwani zinaonekana zina ubora na zinafaa kwa ujenzi, hasa katika Makao Makuu.

Rai hiyo ameitoa katika kijiji cha Mapanga, Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino.

Kwa upande wake, Mwekezaji katika mgodi huo, Sisti Mganga amesema soko la ndani ni dogo hivyo akaonyesha umuhimu wa kupata masoko ya nje.

“Tunapanga kutafuta masoko nje na pia tutajenga kiwanda cha kutengeneza mapambo ili tusipoteze chochote tunachochimba, na tumepanga kuajiri watu wengi kwani kazi hii inahitaji nguvukazi kubwa”,alisema Mganga.

Sisti amesema anaunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli za ujenzi wa viwanda

Ziara hiyo ni endelevu kwani changamoto za wachimbaji hasa wadogo ni nyingi na pia Serikali inataka ikusanye maduhuli yake kupitia sekta ya madini.

 

Mfuko Mpya wa Hifadhi ya Jamii PSSSF Kuanza Kazi Agosti Mosi Mwaka Huu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kutangaza tarehe ya kuanza rasmi kufanya kazi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa  Watumishi wa Umma(PSSSF) leo Jijini Dodoma.Kulia ni Mkurugenzi mkuu wa SSRA Dkt. Irene  Isaka.

Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dodoma

Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) kuanzia Agosti 1, mwaka huu.

Akizungumza  na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali imekamikisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.

“Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF”, alisisitiza mhe. Mhagama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitangaza rasmi leo Jijini Dodoma tarehe ya kuanza  kufanya kazi kwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  ambapo mfuko huo unaanza kazi Agosti Mosi mwaka huu.Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera na Uratibu Prof. Faustine Kamuzora.

Waziri Mhagama amefafanua kuwa, kutokana na hatua hiyo wafanyakazi wote watakaoajiriwa katika sekta ya umma watasajiliwa katika Mfuko wa PSSSF na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF.

Anaongeza kuwa, Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera  Bunge  Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF)  unaanza  kutekeleza majukumu yake bila kuathiri huduma kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa.

Akizungumzia rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa  Waziri Mhagama amesema itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.

Pia Waziri Mhagama amewatoa hofu ya kupoteza ajira watumishi wote wa mifuko iliyounganishwa  kwa kuwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa taasisi.

Kuondoa sintofahamu Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) imeandaa mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria na kanuni za PSSSF ili kuhakikisha kwamba wanachama na wadau wote wa sekta ya hifadhi ya jamii wanakuwa na uelewa sahihi wa sheria hizo na mabadiliko yaliyofanyika.

Mbali na hayo, Waziri Jenista ameteua wajumbe wa Bodi ya Mfuko huo ambao ni Bi. Leah Ulaya, Bw. Rashidi Mtima, Dkt. Aggrey Mlimuka, Bi. Stella Katende, Bw. Thomas Manjati, Bw. Henry Katabwa, Bi. Suzan Kabogo pamoja na Bw. Jacob Mwinula.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma  (PSSSF) Bw. Eliud Sanga (katikati) akisisitiza kuhusu hatua watakazochukua kuhakikisha kuwa mfuko huo mpya unatatua changamoto zilizokuwepo awali katika mifuko iliyounganishwa kuunda mfuko huo.

(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO)

MKURABITA Yakabidhi Hati 600 za Kimila Wilayani Chamwino Leo

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Balozi Daniel Ole Njolay akikabidhi a Hati za Hakimiliki za Kimila wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo. Kutoka kushoto ni Mratibu wa MKURABITA, Bibi. Seraphia Mgembe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahamha Andrea Lukuna na Mwenyekiti Mstaafu wa MKURABITA, Kapteni mstaafu John Chiligati.

Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Bibi. Seraphia Mgembe akifafanua jambo wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahamha Andrea Lukuna na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Balozi Daniel Ole Njolay.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi aliyemaliza muda wake Kapteni Mstaafu John Chiligati akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mahamha wilayani Chamwino Bi. Ester Gerson akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Balozi Daniel Ole Njolay akipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kurasimisha ardhi kuotoka kwa Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.

Baadhi ya watendaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wakiwasalimia wanchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.

Mmoja wa wazee akisoma hati yake aliyokabidhiwa wakati wa hafla ya kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Balozi Daniel Ole Njolay akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliokabidhiwa kukabidhi Hati 600 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Mahamha na Membe wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo. (Picha zote na: Frank Shija, MAELEZO, Chamwino, Dodoma).

Matukio Katika Picha Ziara ya Viongozi wa TAGCO na Idara ya Habari MAELEZO Peramiho, Songea

Mmoja wa wajumbe wa  Ujumbe wa Chama Cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini Bw. Jerald   Chami akisisitiza umuhimu wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kutumia mbinu za kisasa kuwasiliana na wananchi hasa kuhusu miradi inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi katika Halmashuri ya Wilaya ya Songea Vijijini.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Peramiho Bw.Godfrey Chipakapaka  akisisitiza kuhusu mikakati ya Halmashuri hiyo kumjengea mazingira wezeshi afisa Habari wa Halmashuri hiyo ili atekeleze majukumu yake kwa weledi na tija kwa maslahi ya wananchi hasa katika kutoa taarifa za miradi ya maendeleo.

Mwakilishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Casmir Ndambalilo akitoa maelezo kwa Afisa Habari wa Halmashuri ya Wilaya ya Songea Vijijini Bi. Jaclin Moyo kuhusu mifumo inayotumiwa na Idara ya Habari MAELEZO kuwasiliana na wananchi kuhusu miradi  mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali  katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Ujumbe kutoka Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini na Idara ya Habari (MAELEZO) ukiongozwa na Bi.Gaudensia Simwanza ukisisitiza jambo kwa Afisa Habari wa Halmashuri ya Wilaya ya Songea Vijijini  Bi. Jaclin Moyo (kulia) mara baada ya ujumbe huo kufanya ziara kujionea jinsi  maafisa Habari katika Halmashuri ya Wilaya ya Peramiho wanavyotekeleza majukumu yao.

(Picha zote na Idara ya Habari MAELEZO)

 

TAGCO na Idara ya Habari MAELEZO Chachu Mageuzi Utendaji wa Maafisa Habari

Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Songea Bi.Tina Sekambo akisisitiza kuhusu namna Manispaa hiyo inavyomuwezesha Afisa Habari wake kutekeleza jukumu la kuisemea Serikali kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Frank Mvungi- MAELEZO, Ruvuma

Moja ya Hatua zilizochukuliwa na Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Seriklini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) ni kuweka utaratibu wa kufuatilia namna Maafisa Habari na Mawasiliano wanavyotoa taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali  katika Mikoa na Halmashuri .

Akizungumzia jinsi Halmashuri ya Manispaa ya Songea inavyoweka mazingira wezeshi kwa Afisa Habari kutekeleza jukumu hilo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi. Tina Sekambo amesema kuwa dhamira yao ni kumpatia nyenzo zote muhimu katika kutekeleza majukumu yake ya kutoa taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi na wamekuwa wakifanya hivyo kadiri rasilimali zinavyopatikana.

Mwakilishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Casmir Ndambalilo akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Songea Bi.Tina Sekambo  wakati wa ziara ya ujumbe kutoka chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO).

”Mimi natambua umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu miradi ya maendeleo na katika hili Halmashuri yetu imeweka mkazo katika kumpatia vitendea kazi Afisa Habari wetu ili atekeleze jukumu la kutoa taarifa kwa wananchi” Alisisitiza Bi. Sekambo

Akifafanua amesema kuwa Halmashuri  hiyo itaendelea kuwekeza katika kuimarisha mfumo wa mawsiliano kati ya Serikali na wananchi kwa kutambua numuhimu wa suala hilo wamekuwa wakimshirikisha Afisa Habari katika kila jambo ili kumjengea uwezo katika kutoa taarifa kwa wananchi hasa za miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Songea Bi.Tina Sekambo (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) mara baada ya ziara ya ujumbe huo katika manispaa hiyo, ziara hiyo imelenga kukagua na kuona utendaji wa Maafisa Habari na Mawasiliano katika manispaa hiyo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika Halmashuri hiyo.

Naye Kiongozi wa ujumbe huo Bi. Gaudensia Simwanza alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuwaruhusu maafisa hao kushiriki katika mafunzo mbalimbali na kikao kazi ili kuwaongezea ujuzi katika kuisemea Serikali.

Ziara ya ujumbe huo imefanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikilenga kuhamasisha maafisa Habari kuongeza kasi katika kuisemea Serikali hasa kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa  inasisitiza utoaji wa huduma bora kwa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati na ikilenga kunufaisha wananchi wanyonge.

Kiongozi wa ujumbe wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Gaudensia Simwanza akisisitiza umuhimu wa Halmashuri kuwaruhusu maafisa Habari kushiriki katika Kikao Kazi cha mwaka ili wajengewe uwezo zaidi katika kutekeleza jukumu la kuisemea  Serikali hasa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

 

( Picha zote na Idara ya Habari MAELEZO)

Viongozi wa TAGCO na Idara ya Habari MAELEZO Waendelea na Ziara Mjini Lindi

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Bw. Babtista Kihanza akisisitiza jambo kwa ujumbe wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari MAELEZO wakati wa ziara ya ujumbe huo katika Manispaa hiyo mapema wiki hii ikilenga kuweka mikakati ya pamoja katika kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma katika kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Frank Mvungi- MAELEZO,  Lindi

Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Idara ya Habari (MAELEZO) wameanzisha utaratibu wa kufuatilia utendaji wa maafisa habari katika ngazi zote  na kuweka mikakati ya pamoja katika kuimarisha mawasiliano  kati ya Serikali na Wananchi.

Akizungumza Mjini Lindi Kiongozi wa Ujumbe kutoka  TAGCO  na Idara ya Habari MAELEZO Bi. Gaudensia Simwanza amesema kuwa dhamira ya ziaraa katika Halmashuri ya Manispaa hiyo na maeneo mengine hapa nchini ni kuona changamoto zinazowakabili maafisa Habari katika kutekeleza jukumu la kuisemea Serikali na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia katika kutatua changamoto zilizopo.

Mwakilishi wa Idara ya Habari MAELEZO  Bw. Casmir Ndambalilo akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha Maafisa Habari kwa kuwapatia vitendea kazi ili waweze kutekeleza majukumu ya kutangaza miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi hali itakayochochea maendeleo na ustawi wa wananchi.

“ Ziara yetu inalenga kuona namna maafisa Habari wanavyotekeleza jukumu la kuisemea Serikali katika Manispaa ya Lindi hasa kutangaza miradi inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi” Alisisitiza Simwanza

Akifafanua Bi. Simwanza amesema kuwa Halmashuri zinalo jukumu la kuwawezesha maafisa hao ili waweze kutekeleza jukumu la kuisemnea Serikali katika maeneo yao hasa kutoa taarifa za miradi inayotekelezwa akitolea mfano wa ujenzi wa barabara za Lami katika Manispaa hiyo ambao umefanyika kwa kiwango kikubwa na kubadili taswira ya mji huo na kuwa ya kuvutia.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Bw. Babtista Kihanza (watatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) wakati wa ziara ya ujumbe huo mkoani  Lindi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Lindi Bw. Babtista Kihanza amesema kuwa Ofisi yake iko tayari kuweka mazingira wezeshi kulingana na upatikanaji wa rasilimali ili kuwezesha mawasiliano kati ya wananchi na Serikali kuimarika hasa katika kutangaza miradi ya maendeleo.

“ Sisi tuko tayari kumuwezesha afisa habari wetu  kadiri rasilimali zitakavyoruhusu ili aweze kufanikisha jukumu la kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.” Alisisitiza Babtista

Kwa upande wake mwakilishi wa Idara ya Habari MALEZO Bw. Casmir Ndambalilo amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wanapata taarifa za miradi ya maendeleo kwa wakati muafaka ili waweze kutumia fursa za miradi hiyo kujiletea maendeleo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Lindi Bw. Babtista Kihanza akisisitiza jambo kwa kiongozi wa msafara wa ujumbe wa Viongozi wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini  (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Gaudensia Simwanza wakati wa ziara ya ujumbe wa chama hicho katika Manispaa hiyo ikilenga kujionea utendaji kazi wa Maafisa Habari na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mawasiliano hasa katika kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelelezwa na Serikali.

Aliongeza kuwa ni vyema maafisa habari katika Mikoa na Halmashauri wakatumia mbinu za kisasa katika kuwasiliana na wananchi katika maeneo yao kwa kutoa taarifa za miradi yote inayoteklezwa na ile inayotarajiwa kutekelezwa.

Mmoja wa Viongozi kutoka Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) ambaye ni sehemu ya ujumbe uliofanya ziara katika Manispaa ya Lindi  Bw. Ndimmyake Mwakapiso akiagana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Bw. Babtista Kihanza mara baada ya ziara ya ujumbe huo katika manispaa hiyo.

(Picha zote na Idara ya Habari MAELEZO)

 

MKURABITA Yakabidhi Hati Miliki 661 za Ardhi Wilayani Ikungi

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Balozi Daniel Ole Njolay akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu mara baada ya kuwasili wilayani hapo kwa ajili ya zoezi la kukabidhi Hati 661 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Kimbwi na Nkununkhana kata ya Puma wilayani Ikungi jana. Hati hizo zimetolewa ikiwa ni muendelezo wa zoezi la urasimishaji wa mashamba katika maeneo hayo lililoanza mwaka 2011 na kufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilitolewa hati 405. Katikati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bibi. Rustika Turuka.

Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Bibi. Seraphia Mgembe akijadiliana na jambo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu (katikati) mara baada ya kuwasili wilayani hapo kwa ajili ya zoezi la kukabidhi Hati 661 za Hakimiliki ya Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Kimbwi na Nkununkhana kata ya Puma wilayani Ikungi jana. Hati hizo zimetolewa ikiwa ni muendelezo wa zoezi la urasimishaji wa mashamba katika maeneo hayo lililoanza mwaka 2011 na kufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilitolewa hati 405. Kulia ni Mtaalam wa Mawasiliano wa MKURABITA, Bibi. Gloria Mbilimonywa na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA, Bw. Emmanuel Mayeji (wapili kushoto).

Read more