Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Magonjwa ya Moyo Huua Watu Milioni 17 Duniani – Dk. Sanga

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Lugendo akimpima shinikizo la damu (BP) Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa Leyla Faiz wakati wa maadhimisho ya siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Taasisi hiyo elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo na kutoa dawa bila malipo kwa kushirikiana na makampuni yanayotengeneza dawa za binadamu na Shirikisho la Magonjwa yasiyo kuwa ya Kuambukiza (TANCDA).

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Louiza Shem akitoa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya moyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Taasisi hiyo. Pamoja na kutoa elimu ya afya bora Taasisi hiyo imetoa huduma ya upimaji afya bila malipo na kutoa dawa bila malipo kwa kushirikiana na makampuni yanayotengeneza dawa za binadamu na Shirikisho la Magonjwa yasiyo kuwa ya Kuambukiza (TANCDA).

Read more

Serikali Yasaini Mkataba Ujenzi wa SGR Awamu ya Pili

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) Masanja Kadogosa (kulia) na pamoja na Mjumbe wa Bodi kutoka Kampuni ya Ukandarasi ya Yapi Merkezi Insaat ya nchini Uturuki wakisaini Mkataba wa ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Morogoro- Makutopora (Dodoma). Halfa hiyo ilifanyika leo Septemba 29, 2017.

Na. Neema Mathias- MAELEZO.

Serikali imeendelea kutekeleza ahadi ya ujenzi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma baaada ya leo kusaini mkataba na kampuni ya Yapi Markezi ya Uturuki kujenga sehemu ya pili ya reli hiyo kutoka Morogoro mpaka Makutupora, Dodoma.

Mkataba huo umesainiwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Yapi Markezi, Mr.Erdem Arioglu.

Kabla ya kusaini mkataba, Kadogosa alieleza kuwa mkataba huo wa ujenzi wa reli yenye urefu wa kilometa 336 kutoka Morogoro mpaka Makutupora-Dodoma, unahusisha ujenzi wa kilometa 86 za njia ya kupishania treni na maeneo ya kupangia mabehewa 422 kwa uzani wa tani 35 kwa wekeli. Read more

Watumiaji Mitandao ya Kijamii Walaumiwa Kudhalilisha Wanawake

Mjumbe wa Sekretarieti toka Taasisi ya Ulingo wa Wanawake Bi. Saum Rashid akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitoa karipio juu udhalilishaji wa wanawake katika mitandao kwa kisingizio cha siasa, katikati ni Bi. Angelina Mutahiwa na kulia ni Bi. Dominata Rwechungura wajumbe wa Sekretarieti hiyo.

Na: Thobias Robert

Taasisi isiyo ya kiserikali inayoundwa na Jumuiya za Wanawake wa Vyama vyote vya siasa (Ulingo) imelaani vitendo vya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya viongozi wanawake wana siasa pamoja na serikali kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Saum Rashid alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwaaajili ya kulaani watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wanawake. Read more

Serikali Kuzichukulia Hatua Taasisi Zilizokiuka Taratibu za Manunuzi 2016/2017

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Serikali imesema itazichukulia hatua Taasisi zote zilizokiuka sheria na kanuni za manunuzi ya Umma pamoja na zile zenye viashiria vya rushwa ambazo zimebainika katika ripoti ya tathmini ya utendaji iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa mwaka wa Fedha 2016/17.

Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma  na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipokuwa akipokea ripoti ya tathimini ya utendaji  wa Taasisi za Serikali katika sekta ya Manunuzi iliyofanywa na PPRA kwa mwaka wa Fedha 2016/17.

“Tutazichukulia hatua na kuziwajibisha taasisi zote ambazo zimebainika katika ripoti hii kuwa na viashiria vya rushwa au kufanya  malipo yenye utata katika manunuzi yao,” alisema Dkt. Mpango. Read more

JPM Atoa Milioni 260 Kujenga Makazi ya Polisi Waliounguliwa Nyumba

Na: Prisca  Libaga – Maelezo/  Arusha.

RAIS wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ametoa kiasi cha Shilingi milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya za askari wa Jeshi la Polisi  Wilaya ya Arusha,zilizoungua Septemba 27 majira ya saa moja usiku na kusababisha familia 14 zenye watu 44 kukosa mahali pa kuishi.

Mkuu wa jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amesema mbali na fedha za rais pia jeshi la Polisi limetoa Shilingi milioni 40  kwa ajili ya  ujenzi wa nyumba hizo ambazo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Aidha IGP, amesema jeshi la Polisi limetoa Shilingi milioni moja za kujikimu kwa kila familia iliyounguliwa nyumba.

Akizungumza na askari waathirika wa ajali hiyo ya moto IGP, Sirro alisema Mh.rais ameagiza waathirika hao wapewe nyumba za wakala wa majengo TBA zilizoko Tengeru wilayani Arumeru ili wajisitiri wakati mchkato wa ujenzi wa nyumba zao ukiendelea

Amesema kuwa  kwenye maisha kuna changamoto hivyo ajali hiyo ni sehemu ya changamoto  na ni ajali kama zilivyo ajali nyingine.

IGP Sirro aliwaambia kuwa ametumwa kuwapa salamu za Rais Magufuli pamoja na kuwapa pole  na hivyo watambue kuwa jeshi la Polisi lipo pamoja nao wakati wowote.

Amewaambia kuwa rais alitaka kuwaletea mahema lakini ameamua waathirika wote wakakae kwenye nyumba za Wakala wa majengo zilizopo Tengeru wakisubiri nyumba zao zijengwe.

Amesema hilo tukio lisiwarudishe nyuma wala kuwakatisha tamaa bali  waendelee kuchapa kazi na kutekeleza majukumu yao kama kawaida.

Amewaomba Raia wema kutoa  michango  yao ikiwemo vyakula kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ajali hiyo ya moto kwani ni jambo la kiungwana na kistaarabu kwa binadamu kusaidiana hasa katika wakati wa shida.

Katika hatua nyingine IGP Sirro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo, wametembelea nyumba za wakala wa majengo ya serikali  TBA zilizopo Tengeru ‘wilayani Arumeru ambazo ndizo zitatumika kwa muda kuhifadhi askari polisi na familia zao waliounguliwa nyumba zao.

Dkt. Mwakyembe Apiga Marufuku Matumizi ya Takwimu za Kampuni ya Geopoll

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa ukusanyaji na usambazaji wa takwimu zinazohusu sekta ya utangazaji jana Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bibi. Albinus Chuwa na kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Raynold Mfungahema

Na: Neema Mathas

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amepiga marufuku matumizi ya takwimu zinazotolewa na kampuni ya GeoPoll zinazohusu Kiwango cha wananchi kusikiliza na kutazama vituo vya Redio na Televisheni hapa nchini kwa kuwa takwimu hizo zina mapungufu makubwa.

Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na makampuni ya ukusanyaji na usambazi wa takwimu kwa upande mmoja na watumiaji wa takwimu ambao ni vituo vya Redio na Televisheni kwa upande mwingine. Read more

Tanzania Yakabidhiwa Mashine ya Kutoa Dawa ya Usingizi Wakati wa Upasuaji.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kupokea msaada wa mashine ya kutoa dawa za usingizi zilizotolewa na Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania (WRATZ). Mashine hiyo yenye thamani ya Sh. Mil.55 imetolewa na Kampuni ya Kas Medics Limited ikiwa ni matokeo ya uhamasishaji wa kupunguza vifo vya wakina mama na watoto leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Idara kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya na Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama (WRATZ) Rose Mlay.

Na: Paschal Dotto

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa mashine maalumu ya kutoa dawa za usingizi kwa mama wajawazito wenye uzazi pingamizi  wakati wa upasuaji  kwaajili ya kuokoa maisha yao.

Akizungumza katika makabidhiano hayo leo Jijini Dar es Salaam Waziri mwenye dhamana ya Afya Mh.Ummy Mwalimu alisema kuwa, hiyo ni hatua kubwa katika kupambana na vifo vya  wakina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga. Read more

Dkt. Mwakyembe Apiga Marufuku Matumizi ya Takwimu za Kampuni ya Geopoll

Na. Neema Mathas

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amepiga marufuku matumizi ya takwimu zinazotolewa na kampuni ya GeoPoll zinazohusu Kiwango cha wananchi kusikiliza na kutazama vituo vya Redio na Televisheni hapa nchini kwa kuwa takwimu hizo zina mapungufu makubwa.

Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na makampuni ya ukusanyaji na usambazi wa takwimu kwa upande mmoja na watumiaji wa takwimu ambao ni vituo vya Redio na Televisheni kwa upande mwingine.

Katika kikao hicho cha pamoja, makampuni ya IPSOS Tanzania, Push Observer na GeoPoll walifafanya mawasilisho ya namna wanavyokusanya takwimu wakati Ofisi ya Taifa ya Takwimu yenyewe ilifanya wasilisho la kuonesha njia bora na sahihi za ukusanyaji na usambazaji takwimu. Hata hivyo kamapuni ya Geopoll haikuhudhuria kikao hicho. Read more