Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Yaagiza Wanafunzi Kuepuka Matumizi ya Dawa za Kulevya

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya akifurahia jambo na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Tabora jana alipokwenda kukagua shughuli za ukarabati wa majengo unaoendelea. (Picha na Tiganya Vincent-RS Tabora.)

Na: Tiganya Vincent, RS-TABORA

SERIKALI imewaonya wanafunzi kuepuka matumizi ya dawa za kulevya ambayo ndio wakati  mwingine yawasababisha kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na vurugu ambazo hatimaye zinawasababisha baadhi yao kusimamishwa masomo na kukatiza ndoto zao.

Agizo hilo limetolewa jana wilayani Tabora na  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya  wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Tabora ili kujionea maendeleo ya ukarabati chini ya utaratibu wa ukarabati wa Shule Kongwe hapa nchini.

Aliwaambia kuwa wanafunzi wote nchini wanatakiwa kufuata Sheria za Shule na za Nchi ili kuhakikisha anamaliza masomo yake bila kupata matatizo ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Unatakiwa kufuata Sheria na taratibu za shule kama ulivyoelekeza , ukitoroka shule na kwenda mitaani ukileta fujo …ukileta vurugu utashughulikiwa kama ulivyokutwa huko huko…kwa sababu mwanafunzi anatakiwa kuwa eneo la shule sawa “ alisisitiza Naibu Waziri huyo.

Akitoa taarifa ya ukarabati unaoendelea Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tabora Marwa Robert alisema kuwa hadi hivi sasa kazi mbalimbali zimekwisha fanyika

Hivi karibuni Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Milambo walitoroka shuleni usiku na kuvamia sherehe za mkazi wa Tabora

 

Dkt Pallangyo Akutana na Kampuni ya M & P Exploration Production Tanzania Limited

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akiongoza kikao kilichoshirikisha watendaji kutoka Kampuni inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi ya M & P Exploration Production Tanzania Limited, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akizungumza na Meneja Mkuu kutoka Kampuni inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi ya M & P Exploration Production Tanzania Limited, Christophe Maitre ( kushoto) katika kikao hicho.

Sehemu ya watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (hayupo pichani) katika kikao hicho.

Bandari Kavu ya Kwala –Vigwaza Kuanza Kutumika Januari Mwakani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia ya njano akiwa katika majukumu ya ukaguzi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza inayojengwa mkoani Pwani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Vigwaza Mkoani Pwani na kumtaka mkandarasi Suma JKT kuongeza kasi na kuzingatia ubora.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanaunganisha kwa haraka ili reli na barabara zinazoingia katika bandari kavu hiyo zinakamilika na hivyo kuiwezesha bandari kavu hiyo kuanza kutumika ifikapo Januari mwakani.

Read more

Makubaliano ya Kuwarejesha Nyumbani Wakimbizi wa Burundi Yatiwa Saini Dar Leo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba (Katikati), akisaini hati ya makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa Burundi waishio Tanzania wakati wa mkutano wa siku moja uliofanyika leo Jijini Dar es Salaa. Kutoka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Bw. Pascal Barandagiye, Mkurugenzi wa Huduma za Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison Mseke, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Tanzania (UNHCR), Bi. Chansa Ruth Kapaya na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Burundi Bw. Abel Mbilinyi.

Na: Mwandishi Wetu , MAELEZO

Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) wamepitisha mpangokazi wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi raia wa Burundi ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari kurejea nyumbani.

Mpangokazi huo ni sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini leo kufuatia Kikao cha 19 cha Kamisheni ya Pande Tatu kilichofanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na mawaziri wanaoshughulikia wakimbizi wa Tanzania, Burundi na mwakilishi wa UNHCR.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba akibadilisha hati ya makubaliano ya kuwarejesha makwao Wakimbizi kutoka Burundi waishio Tanzania na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Tanzania (UNHCR), Bi. Chansa Ruth Kapaya katika mkutano wa siku moja uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison Mseke baada ya kusaini hati za makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa Burundi waishio nchini Tanzania katika mkutano wa siku moja majadiliano kuhusu urejeshwaji wa wakimbizi hao uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Chini ya Mpangokazi huo wa kipindi cha karibu miezi mine (07 Septemba hadi 31 Disemba, 2017) wakimbizi 12,000 ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari watarejeshwa nyumbani huku ukitoa nafasi kwa wengine zaidi watakaojiandikisha kujumishwa.

Makubaliano hayo yalitiwa saini na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo wa Burundi Pascal Barandagiye na Mwakilishi wa UNHCR nchini Bibi Chansa Ruth Kapaya.

Chini ya Makubaliano hayo shirika la UNHCR na washirika wake wataweza kutembelea maeneo ya mipakani ya Tanzania na Burundi kwa lengo la kusaidia mchakato wa urejeshaji wa hiari wa wakimbizi hao na masuala mengine yanayohusu hifadhi ya wakimbizi na raia wengine wanaohitaji hifadhi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba (katikati) akiteta jambo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Tanzania (UNHCR) Bi. Chansa Ruth Kapaya, kulia ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi nchini Burundi (UNHCR) Bw. Abel Mbilinyi na kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Bw. Pascal Barandagiye na Mkurugenzi wa Huduma za Wakimbizi Tanzania Bw. Harrison Mseke (wapili kushoto) wakati wa mkutano wa siku moja wa kusaini makubaliano ya kuwarejesha makwao wakimbizi kutoka Burundi waishio nchini Tanzania leo Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na: Thobias Robert)

Pande hizo za makubaliano zimetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano katika kutekeleza zoezi la kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao na kulitaka shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kutoa chakula kwa wakimbizi wanaorejea kwa kipindi cha miezi mitatu.

Kikao hicho cha 19 cha Kamisheni ya Pande Tatu kimeeleza kutumbua na kuthamini ukarimu wa watanzania ambao umewezesha mamilioni ya wakimbizi kuishi Tanzania tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1961 na zaidi kuendelea kuwakarimu wakimbizi wapatao 350,000 miongoni mwao 256,850 wakiwa raia wa Burundi.

Wafanyakazi JKCI Watakiwa Kujituma

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma, kuongeza ufanisi  na kutoa huduma bora kwa wagonjwa ili epukana  na malalamiko yanayoweza kujitokeza.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika  jijini Dar es Salaam.

Prof. Janabi pia aliwahimiza wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kuendelea kutunza vizuri kumbukumbu mbalimbali zikiwemo za wagonjwa na utendaji wa kazi zao za kila siku ili pale zitakapohitajika zipatikane kwa haraka.

“Mjitahidi kujaza fomu ya wazi ya mapitio na upimaji utendaji kazi (OPRAS) kwa wakati ili kusiwe na malalamiko ya upandaji wa vyeo kwani ujazaji wa fomu hizo ndiyo unaowezesha mfanyakazi kupimwa utendaji wake kwa kipindi cha mwaka mzima”, alihimiza Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Godfrey Tamba aliupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha wafanyakazi  wanafanya kazi zao katika mazingira bora.

Tamba alisisitiza, “Wafanyakazi wenzangu tunaodai haki zetu tukumbuke kutimiza wajibu wetu wa kazi kwa wakati, kwani uongozi wa TUGHE hautawatetea watu ambao hawatimizi wajibu wao ipasavyo”.

Hiki ni kikao cha pili cha wafanyakazi wote kufanyika tangu kuanza kwa mwaka huu ambapo katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.

Mwigulu Afungua Kikao Cha Kujadili Urejeshaji wa Wakimbizi wa Burundi Walio Tayari Kurejea Nchini Kwao

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mwigulu Nchemba(watano kulia), Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi,Pascal Barandagiye, (wasita kulia), na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya (wanne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Kikao cha 19 kinachoshirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR), lengo ni kujadili na kuwekeana makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa katika makambi ya wakimbizi ambao wako tayari kurejea nchini kwao.Kikao hicho kimefanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.)

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha 19 kinachoshirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), lengo ni kujadili na kuwekeana makubaliano juu ya mpango wa kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa katika makambi ya wakimbizi ambao wako tayari kurejea nchini kwao. Kikao hicho kimefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Read more

Siku ya Wahandisi Kufanyika Mjini Dodoma

Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akieleza juu ya maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 7 hadi 8 mwezi Septemba.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi (kushoto) akionesha kwa Waandishi wa Habari picha yenye mashine ya kushindilia barabara ambayo imegunduliwa na wahandisi wa hapa nchini na kupewa jina la Magufuli One, kulia ni Msajili Msaidizi wa bodi hiyo, Mhandisi Benedict Mukama .

Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Benedict Mukama (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akieleza juu ya maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 7 hadi 8 mwezi Septemba, kushoto ni Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Mhandisi Patrick Barozi.
Picha na Eliphace Marwa